22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

WENYE MADUKA WAKABIDHI BIDHAA KWA MACHINGA

wamachinga

PATRICIA KIMELEMETA NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

WAFANYABIASHARA wakubwa wenye maduka  mitaa ya Kariakoo na Karume wamewapa  wamachinga bidhaa zao  waweze kuziuza nje ya maduka yao, MTANZANIA limebaini.

Hali hiyo imetokea ikiwa ni  siku ya pili baada ya Rais Dk John Magufuli kutoa agizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kutowafukuza wamachinga   katikati ya miji bila kuwapatia maeneo rafiki ya biashara.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA  jijini Dar es Salaam, umebaini kuwapo  shehena kubwa za bidhaa mbalimbali zinazouzwa na wamachinga kwa makubaliano maalum na wenye maduka.

Bidhaa hizo ni pamoja na nguo za aina mbalimbali, viatu, mikoba ya wanawake, vipodozi, nywele bandia, vyombo vya nyumbani na  vifaa vya umeme na ujenzi.

Vingine ni  vyakula na matunda ya kila aina ambayo yamemwagwa katika mitaa mbalimbali ya Kariakoo kusubiri wateja.

Uchunguzi huo umebaini kuwa bidhaa hizo zinauzwa kwa bei nafuu tofauti na madukani au kwenye masoko yaliyo rasmi.

Mathalani nguo zilizokuwa zikiuzwa kati ya Sh 30,000 hadi Sh 50,000 dukani hivi sasa zinauzwa kwa wastani wa Sh 10,000 hadi Sh 20,000.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya uchumi wameieleza hali hiyo kuwa inaweza kuporomosha uchumi kwa kuwa bidhaa hizo wanazopewa wamachinga kwa kile kinachoitwa ‘mali kauli’, hazitalipiwa kodi kama ilivyotarajiwa.

VYOO CHANGAMOTO

Wakati huohuo, uhaba wa vyoo katika mitaa ya inayozunguka eneo la Kariakoo ikiwamo Kongo, Nyamwezi, Tandamti, Swahili, Sikukuu, Narung’ombe Mchikichi na unaweza kuibua tatizo jipya la  afya.

Katika mitaa hiyo hakuna vyoo rasmi vinavyoweza kuhimili na kutosheleza wingi wa wafanyabiashara hao na wateja wao.

Katika uchunguzi huo imebainika kuwa  majengo mengi ya  biashara yaliyopo Kariakoo yana vyoo vichache kwa ajili ya wapangaji wao na mengine hayana.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya wafanyabiashara wanaamua kujisaidia haja ndogo kwenye chupa za plastiki na kuzitupa ovyo mitaani.

Katika Soko Kuu la Kariakoo miundombinu ya vyoo vyake ni ya zamani hivyo haikidhi mahitaji ya wateja wake.

HALMASHAURI YA ILALA

Akizungumzia hali hiyo, mmoja wa maofisa wa halmashauri ya Ilala ambaye hakutaka kutajwa jina lake  kwa sababu maalum, alisema vyoo vya umma katika halmashauri hiyo vimefungwa kwa sababu ya ubovu wa miundombinu yake ambayo ni ya zamani tofauti na mahitaji ya sasa.

“Miundombinu ya vyoo vyetu vya umma katika masoko ya Kariakoo, Karume imepitwa na wakati.

“Vimefungwa na havifai kwa matumizi ya binadamu ingawa awali vyoo hivyo vilikuwa vikichangia mapato ya ndani,“ alisema ofisa huyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na   Dar es Salaam jana, baadhi ya wasomi ambao walionyesha wasiwasi wao kuhusu wafanyabiashara hao kufurika katikati ya miji.

Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa uchumi na kuondoa umaskini nchini (REPOA), Profesa Samuel Wangwe alisema mpaka sasa huduma za vyoo na msongamano wa watu katika mitaa ya Kariakoo ni mbaya kuliko ilivyokuwa awali, jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya wananchi.

“Idadi ya vibaka na wezi imeongezeka kutokana na   msongamano mkubwa wa watu kwenye maeneo hayo.

“Kunaweza kutokea magonjwa ya mlipuko hivyo mamlaka husika zinapaswa kukaa na kuangalia hali hiyo,”alisema Profesa Wangwe.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Profesa Hajji Semboja alisema kauli ya Rais Magufuli kuhusu wamachinga imetafsiriwa vibaya na watendaji wake.

Alisema rais alimaanisha mamlaka husika kutenga maeneo maalumu ambayo yatakuwa na huduma zote zinazostahili kwa ajili ya kufanyia shughuli zao.

Alisema kitendo cha wamachinga kurudi kwenye maeneo yasiyo rasmi hadi barabarani kinaonyesha wazi kuwa bado kuna tatizo la uelewa kwa wafanyabiashara hao.

Katika maeneo hayo, lazima kuwe na utaratibu maalumu ambao utasaidia serikali kukusanya kodi kwa wafanyabiashara hao, alisema.

Hata hivyo, Dk. Honest Ngowi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, alisema   wamachinga wanapaswa kutengewa maeneo maalumu ya kufanya shughuli zao  kurahisisha ukusanyaji wa kodi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles