24.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

MIAKA 55 YA UHURU WA TANGANYIKA LEO

tanzania-independence

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

WATANZANIA leo wanaadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyika ambao huadhimishwa Desemba 9 ya kila mwaka,  huku viongozi mbalimbali wa ndani na nje wakitarajiwa kuhudhuria sherehe hizo.

Maadhimisho hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, ambapo mwaka jana alisitisha sherehe na kuamua fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo kujenga barabara ya Bagamoyo kutoka Morocco, Kinondoni hadi Mwenge.

Kwa mujibu wa taarifa  iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye ulemavu), Jenista Mhagama, aliwataka wananchi wote kushirikiana na kusherehekea uhuru wa Tanzania bara kwa kuunga juhudi za Serikali ya awamu ya Tano ya kupinga ufisadi na rushwa nchini.

“Kwa niaba ya Serikali natoa wito kwa wananchi wote nchini kusherehekea siku hii kwa kuwakumbuka waasisi wetu waliotetea na kutuletea Uhuru wa nchi yetu, niwaombe wananchi wote kuunga mkono juhudi za Rais wetu Dk. John Magufuli katika kuimarisha uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema Jenista.

Kauli mbiu ya mwaka katika kuadhimisha sherehe hizo ni. “Tuunge Mkono Jitihada za Kupinga Rushwa na Ufisadi na Tuimarishe Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo Yetu”.

Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo atakuwa Rais Dk. John Magufuli.

Polisi

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limejipanga kuhakikisha amani na utulivu vinatawala katika maadhimisho hayo yanayofanyika leo Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamishna wa Kanda Maalum, Simon Sirro, alisema maadhimisho hayo yatahudhuriwa na viongozi wa kitaifa , mabalozi, wanasiasa, wakuu wanchi za jirani pamoja na waliotumikia  kitaifa na kustaafu.

“Tunaomba wananchi wasiwe na shaka yoyote ya kiusalama na pia wajitokeze kwa wingi uwanjani ili kusherehekea sikukuu hiyo kwa utulivu na amani,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles