26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Manyara yatajwa kinara wa ukeketaji

Na RAMADHAN HASSAN – DODOMA

RIPOTI ya hali ya ukeketaji nchini inaonesha kuwa Mkoa wa Manyara ni kidedea kwa kukeketa wasichana  huku ripoti hiyo ikieleza kuwa wasichana wanaozaliwa au kulelewa na mama aliyekeketwa hukeketwa pia.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza ukeketaji kwa Mikoa ya Kanda ya Kati iliyoandaliwa na Redio ya C-FM ya Jijini hapa jana, Msimamizi Mkuu  wa vipindi wa Redio hiyo, Emmanuel Likuda alisema kwa mujibu wa ripoti ya  Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria (TDHS) wa mwaka 2015-2016 inaonesha  Mikoa inayoongoza kwa ukeketaji nchini.

Kampeni  hiyo imepewa jina nisitiri nina haki ya kutimiza ndoto zangu,usinikekete,usinipe mimba utotoni ambapo  balozi wa kampeni hizo  ni Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Diana Exavery maarufu kwa jina la Malaika.

Likuda aliutaja Mkoa wa Manyara unaongoza kwa ukeketaji  kwa asilimia 58 ukifuatiwa na Dodoma kwa asilimia 47, Arusha asilimia 41, Mara 32 na Singida asilimia 31.

Alisema ripoti hiyo imefafanua kuwa ukeketaji hufanywa kwa asilimia 86 na mangariba au wakeketaji wa jadi na asilimia 25 hukeketwa  katika umri wa miaka 13 na zaidi.

“Ripoti hiyo pia imeeleza pia kuwa wasichana wanaozaliwa au kulelewa na mama aliyekeketwa hukeketwa pia na kuwa na asilimia 95 ya asilimia 86 ya wanawake waliokeketwa hawakubaliani na kitendo hicho na wanatamani kisiwepo kabisa,” alisema Likuda.

Alisema kutokana na hali hiyo ndio maana kituo cha CFM cha jijini hapa kimeamua kuja na kampeni hiyo lengo likiwa ni kusaidia wasichana  wasikeketwe hususani katika Mikoa ya Kanda ya Kati.

“Tumezindua kampeni yetu leo (jana) na tutaendelea kufanya hivyo kwa juhudi kubwa bila kuchoka lengo letu ni kuhakikisha tunafikia malengo ya kuhakikisha mwanamke hakeketwi,” alisema.

Kwa upande wake, Balozi wa kampeni hizo, Malaika alisema madhara ya ukeketaji ni makubwa  kiafya kwa mtoto wa kike  ikiwemo kupata athari za kisaikolojia kama msongo wa mawazo kwani wengi hufanya hivyo bila ridhaa yao.

“Madhara ya afya ya uzazi ambayo hupelekea kuongezeka  kwa vifo vya mama na mtoto  wakati wa kujifungua pia maumivu makali wakati wa kukeketwa,kumwaga damu nyingi, kovu la kudumu sehemu za siri pamoja na kutokufurahia tendo la ndoa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,734FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles