24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wagonjwa wapya 19 wa kifua kikuu wabainika Temeke

Na AVELINE  KITOMARY – DAR ES SALAAM

WATU 1,626 wamejitokeza kupata taarifa sahihi, vipimo na elimu kuhusu ugonjwa kifua kikuu ambapo katika zoezi hilo watu 19 wameibuliwa kuwa na ugonjwa huo.

 Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalum wakati wa maonesho ya One Stop jawabu yanayoendelea katika Uwanja wa Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Manispaa ya Temeke, Dk Marry Chiryamkubi alisema wagonjwa hao waliibuliwa katika upimaji uliofanyika eneo la Kibonde Maji wiki iliyopita.

“Katika zoezi la One Stop Jawabu tulianza wiki iliyopita pale Kibonde Maji, zoezi ambalo Mkuu wa wilaya ameanzisha ili kutoa huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Temeke katika eneo moja.

“Tulitoa huduma kwa siku saba  ambapo tuliweza kuhudumia watu 1626 hawa tulitoa  elimu kuhusu kifua kikuu na kati hao  wanaume walikuwa 734 na wanawake 892.

“ Katika hao waliohisiwa kuwa na kifua kikuu  walikuwa 158 ambapo wanaume walikuwa 57 wanawake walikuwa 101,” alibainisha Dk Chiryamkubi.

Alisema kuwa baadaye walichukua sampuli za wahisiwa  ambapo majibu yake yalionesha kuwa watu  19 wamekutwa na maambukizi ya kifua kikuu na tayari wameshaanzishiwa dawa katika hospitali ya Zakhiem, Mbagala.

“Na Leo kuanzia juzi zoezi hili limeanza katika viwanja vya Mnazi mmoja ambapo  tunatoa huduma  hiyo ya kutoa elimu  kwa wananchi wote wanaokuja kutembelea banda letu hapa.

“Huduma hiyo tokea ilivyoanza juzi tumeweza kuhudumia watu 598 na tumepata wahisiwa 21 ambapo sampuli zimechukuliwa Temeke hospitali na majibu yatatoka leo(jana).

Alisema kuwa wanapochukua sampuli  majibu yanatoka na wagonjwa wanapogundulika wanaanzishiwa dawa na  matibabu  ya kifua kikuu yanatolewa bila malipo.

“Katika matibabu  mgonjwa anaamua aina ya matibabu  kwa hospitail ambayo iko karibu na yeye au nyumbani.

“Kwahiyo tunaendelea kutoa elimu tunawaambia kuhusu kifua kikuu kuwa ugonjwa huu sio wa kulogwa  unaambukizwa  kwa njia ya hewa,mtu akijihisi kuwa anakohoa zaidi ya wiki mbili, kupata homa za usiku na kutokwa na jasho jingi aende hospitali kupata matibabu mara moja,”alieleza Dk Chiryamkubi.

Alisema ni vyema watu wakajitokeza katika maonesho hayo ili kujua hali za afya zao .

“Watu wanajitokeza kwa wingi kama kule Kibonde Maji hatutegemei tena kama kuna watu wenye kifua kikuu mitaani kwasababu watu wamejitokeza wengi.

“Na inaonekana  katika jamii kifua kikuu bado ni changamoto haijafahamika vizuri kwahiyo hilo zoezi linatuambia kuwa tunahitaji kwenda ndani zaidi kwa jamii bila kusubiri wagonjwa kuja kwenye vituo vya afya,”alisema.

Dk Chiryamkubi alitoa wito kwa jamii wanapokuwa na matatizo yoyote ya kiafya ni vyema kuwahi hospitali ili kuokoa maisha yao.

“Kwa Kifua kikuu  matibabu ni bure na mgonjwa akianza matibabu anapona kabisa.

Kwa upandea wake Makamu Katibu wa Asasi ilisiyo ya kiserikali ya mapambano ya kifua kikuu na Ukimwi  Temeke(MUKUKUTA) Jafari Ndaza alisema taasisi hiyo imekuwa ikiibua wagonjwa wengi mitaani kutokana na kuifata jamii moja kwa moja.

“Mimi pia ni miongoni mwa wahanga ambao tayari wameshaugua  kifua kikuu na nimepona baada ya kuona kifua kikuu ni tatizo tukaamua kutengeneza taasisi hii ili kuishaidia jamii baada ya kuona kuwa uelewa wa jamii ni mdogo kuhusu kifua kikuu.

“Hivyo tumejitoa kuelimisha na kusaidia watu wenye kifua kikuu kupata matibabu katika jamii tunaenda sehemu mbalimbali na tumeibua wagonjwa wengi,”alisema Ndaza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles