23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MANJI AONDOLEWA MUHIMBILI USIKU APELEKWA KEKO

Na WAANDISHI WETU

MFANYABIASHARA maarufu, Yusuf Manji, ameondolewa chini ya ulinzi mkali wa Polisi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alikokuwa akipatiwa matibabu na kupelekwa Gereza la Keko, lililopo jijini Dar es Salaam.

Taarifa za uhakika na ambazo zimethibitishwa na wakili wake, zinaeleza kuwa, Manji, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi na Usalama wa Taifa ambayo kimsingi hayana dhamana, aliondolewa hospitalini hapo juzi saa moja jioni.

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali ndani ya Gereza la Keko na ndani ya Taasisi ya JKCI, vililithibitishia MTANZANIA Jumamosi juu ya taarifa hizo za Manji.

“Ni kweli Manji walimwondoa jana usiku, alipelekwa moja kwa moja Gereza la Keko,” alisema mmoja wa watoa taarifa hizo.

Katika kuthibitisha hilo, MTANZANIA Jumamosi jana lilifika JKCI, lakini halikuwaona askari magereza waliokuwapo hapo kwa ajili ya kutoa ulinzi kwa siku zote ambazo Manji alikuwa amelazwa.

Gazeti hili lilimtafuta kwa njia ya simu Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Profesa Mohamed Janab, ambaye hata hivyo alikataa kuthibitisha taarifa hizo, kwa madai kuwa, hawezi kutoa taarifa za mgonjwa kwa kuwa si utaratibu.

“Si utaratibu wetu kutoa taarifa za mgonjwa…labda nikuambie tu jambo la msingi na kubwa sisi leo tupo katika viwanja vya Sabasaba, tumewapima watu takribani 420 hivi magonjwa ya moyo na wapo ambao walikuwa hawajui wanaumwa na tumewaambia waanze dawa,” alisema Profesa Janabi.

MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta kwa njia ya simu mmoja wa mawakili wa Manji, Alex Mgongolwa, ambaye alisema alikuwa hospitali akimuuguza mama yake, hivyo hakuwa na taarifa hizo.

Wakili Mgongolwa alimtaka mwandishi wa gazeti hili kumtafuta Wakili Hudson Ndusyepo, ambaye ni miongoni mwa wanaomtetea Manji, ili kupata taarifa za kina.

MTANZANIA Jumamosi liliwasiliana na Ndusyepo, ambaye alithibitisha taarifa za kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo.

“Ninaweza kuthibitisha ni kweli amekuwa discharged (ameruhusiwa) kutoka hospitali na ninaweza kuthibitisha kuwa ni kweli yupo Keko, ila suala la kama ametoka jana au juzi kupelekwa Keko silijui, kwa sababu leo ni mapumziko,” alisema Wakili Ndusyepo.

Manji (41) na wenzake watatu, Jumatano wiki hii (Julai 5) walisomewa mashitaka ya uhujumu uchumi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuhamia hospitalini hapo.

Mahakama hiyo ililazimika kuchukua uamuzi huo wa kuhamia katika hospitali hiyo kutokana na Manji kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo.

Mfanyabiashara huyo, ambaye kabla ya kusomewa mashtaka hayo alikuwa akishikiliwa na Jeshi la Polisi tangu Juni 30 mwaka huu, alikuwa amelazwa katika wodi namba moja na alisomewa mashitaka hayo huku akiwa kitandani.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda (28), Mtunza stoo, Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43), mkazi wa Chanika, ambao walisomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

 

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tulumanywa Majigo, alidai kwamba Juni 30, mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe A, wilayani Temeke, Dar es Salaam, washitakiwa wote kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na mabalo 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vyenye thamani ya Sh milioni 192.5.

 

Majigo alidai Julai mosi mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe A, wilayani Temeke, Dar es Salaam, washitakiwa wote walikutwa na askari polisi wakiwa na mabalo nane ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za JWTZ vyenye thamani ya Sh milioni 44.

 

Katika shitaka la tatu, inadaiwa Juni 30, mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe A, washitakiwa walikutwa wakiwa na mhuri wa JWTZ ambao uliandikwa “Mkuu wa Kikosi 121 Kikosi cha JWTZ” bila kuwa na uhalali, kitendo kinachohatarisha usalama wa nchi.

Pia inadaiwa tarehe hiyohiyo maeneo ya Chang’ombe, washitakiwa walikutwa na mhuri uliokuwa umeandikwa “Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupora Dodoma” bila kuwa na uhalali, kitendo kinachohatarisha usalama.

Baada ya kusomewa mashtaka, hawakutakiwa kuzungumza chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo.

Pia, upande wa mashtaka uliwasilisha hati kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ya kuzuia dhamana kwa washtakiwa.

Mawakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo, Malimi Seni na Emmanuel Safari, walipinga hati ya kuzuia dhamana wakiiomba mahakama isiipokee kwa sababu haina mamlaka na kesi hiyo.

Walidai kitendo cha DPP kuzuia dhamana hiyo ni mwendelezo wa matumizi mabaya ya madaraka na hawatendi haki kwa washtakiwa.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 19, kwa ajili ya kutajwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles