24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mambo ya Ndani yamwaga ajira

Ramadhan Hassan -Dodoma

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imewasilisha bajeti ya mwaka 2020/21 ya zaidi ya Sh bilioni 899, huku ikimwaga zaidi ya ajira 4,000 kwa Jeshi la Magereza, Uhamiaji, Polisi, Zimamoto na Uokoaji.

Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alisema kati ya ajira hizo 2,725 ni za Polisi, Uhamiaji 495, Magereza 685 na Zimamoto na Uokoaji 501.

Alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi, pia limepanga kuendelea kutoa mafunzo kwa maofisa, wakaguzi na askari 9,465 na watumishi raia 25.

“Katika mafunzo hayo, maofisa 9,051 watapata mafunzo ndani ya nchi kupitia vyuo vya polisi na 414 nje ya nchi kwa udhamini wa taasisi na nchi mbalimbali,” alisema Simbachawene.

 Alisema katika mwaka 2020/21 Idara ya Uhamiaji inatarajia kuajiri askari 495 na kuwapa mafunzo ya awali.

Pia, itaendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa maofisa, askari na watumishi raia ili kuwaongezea ujuzi wa utendaji kazi kwa ufanisi zaidi.

Simbachawene alisema katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa rasilimali watu, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatarajia kuwapandisha vyeo maofisa na askari 1,311 na kuajiri askari wapya 501 katika mwaka 2020/21.

“Askari hao watakaoajiriwa watapatiwa mafunzo ya awali ya kuzima moto na uokoji katika Chuo cha Zimamoto na Uokoaji kilichopo Chogo (Handeni) mkoani Tanga,” alisema Simbachawene.

Kuhusu mafunzo na ajira kwa watumishi wa Jeshi la Magereza, alisema katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 maofisa na askari 1,537 walipata mafunzo ya uongozi wa kijeshi katika vyuo vya Magereza na watumishi 951 walihitimu mafunzo ya taaluma mbalimbali katika vyuo vya ndani na nje ya jeshi.

”Jeshi linatarajia kuajiri askari 685 wenye fani mbalimbali watakaopatiwa mafunzo ya awali katika Chuo cha Magereza Kiwira (Mbeya),” alisema Simbachawene.

Alisema pia jeshi hilo linatarajia kutoa mafunzo ya uendeshaji wa magereza na taaluma ya urekebishaji kwa maofisa na askari 3,270 katika ngazi mbalimbali za uongozi.

BAJETI YAPUNGUA 

Katika mwaka wa fedha 2019/20, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliidhinishiwa bajeti ya Sh 921,247,033,279 na kati ya fedha hizo, Sh 517,040,341,000 ni kwa ajili ya mishahara, Sh 372,268,278,000 matumizi mengineyo na Sh 31,938,414,279 miradi ya maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles