25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MALORI 600 YA TANZANIA YAZUILIWA ZAMBIA KWA MIEZI MIWILI

Na NORA DAMIAN-

DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wamiliki wa Malori nchini (TATOA), kimesema kimepata hasara ya zaidi ya Sh bilioni 15 kutokana na kushikiliwa kwa malori yao 600 nchini Zambia.

Malori hayo yaliyokuwa na magogo yalikuwa yakisafirishwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuja Tanzania.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa TATOA, Elias Lukumay, alisema hadi sasa ni miezi miwili tangu malori hayo yazuiliwe nchini humo.

“Tuna nyaraka zote halali na tulitoka Congo salama tukapita mpaka wa Kasumbalesa hadi Nakonde halafu wakaja kuzuia mzigo.

“Tunapata hasara kubwa kwa sababu hadi sasa malori yameshikiliwa kwa miezi miwili na safari za Congo kwa mwaka ni kama mara sita tu kwa hiyo  mpaka sasa tumeshapoteza safari mbili,” alisema Lukumay.

Kwa mujibu wa Lukumay, gari inapokwenda Congo huwa inalipwa Dola za Marekani 6,000 na ikirudi hulipwa Dola 4,000.

Naye Mwakilishi wa Kampuni ya Mature Logistic, Japhet Peter, alisema usalama wa madereva na wafanyakazi wengine walioko kwenye malori hayo uko hatarini kutokana na kukosa huduma muhimu za kibinadamu.

Alisema madereva na wafanyakazi 1,200 wanashikiliwa nchini humo na kwamba wanaishi katika mazingira magumu kutokana na kulala kwenye magari.

“Afya za madereva wetu zinazidi kutetereka kutokana na mazingira yalivyo na jana kulitokea vurugu.

“Tunaomba Serikali iongeze kasi ya kushughulikia suala hili kwa sababu linatuumiza sana yaani unafilisika huku unaona,” alisema Peter.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafirishaji ya Walker, Arnold Lema, alisema kutokana na kushikiliwa kwa malori hayo gharama zinazidi kuongezeka siku hadi siku kwani kontena moja hulipiwa Dola za Marekani 30 kwa siku.

“Sekta ya usafirishaji ina mchango mkubwa katika nchi yetu na kama malori yakiendelea kushikiliwa mapato ya kigeni yatapungua,” alisema Lema.

Alipoulizwa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, Mindi Kasiga, alisema suala hilo linashughulikiwa na ubalozi wa Tanzania nchini Zambia.

“Kuna watu wanashughulikia hilo suala wako kwenye ubalozi wetu wa Zambia,” alisema Kasiga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles