22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

NDUGAI AFUNGUKA KINACHOMUUMIZA BUNGENI

Na FREDY AZZAH

-DODOMA

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema hakuna kitu kinachomuumiza kama baadhi ya wabunge kusema ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria kuna ubaguzi, huku Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akisema endapo vifo vingekuwa vikitokea kila mara katika mhimili huo, wabunge wangejifunza unyenyekevu.

Kauli hizo walizitoa mjini hapa jana katika viwanja vya Bunge walipoaga mwili wa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Dk. Elly Macha, aliyefariki dunia Machi 31, mwaka huu katika Hospitali ya New Cross Wolverhampton, Uingereza na mwili wake unatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Kirua Vunjo, Wilaya ya Moshi Vijijini, Kilimanjaro.

NDUGAI

Akitoa salamu za Bunge kabla ya kuanza kuagwa kwa mwili huo, Ndugai, alisema: “Kifo cha Dk. Macha kinanikumbusha baadhi yetu tunaposimama bungeni tunasema kuna ubaguzi, jambo ambalo mimi huwa linaniuma sana, kweli kama kiongozi tunajitahidi kuhakikisha mambo yako sawa, lakini kwenye kila taasisi kuna changamoto, ila hili neno ubaguzi huwa ni kubwa sana kuliko mizani yake.

“Tungekuwa na ubaguzi mama Macha alikuwa Uingereza na matibabu yake yalikuwa ya kibinafsi hivi, lakini tangu tulipojua tu, tulishirikiana naye na ubalozi wetu nao ulishiriki kwa ukaribu sana.”

 Akizungumzia kilichofanya mwili wa Dk. Macha ubaki Uingereza kwa takribani wiki tatu, Ndugai, alisema ni kwa sababu Uingereza kuna taratibu zinazochukua muda mrefu mtu akifariki ili kuhakikisha hakuna ‘mkono wa mtu’.

“Ndiyo maana imetuchukua muda mrefu kidogo na ofisi ya Bunge tumeusafirisha kutoka Uingereza na wana familia na kuutoa Dar es Salaam kuja hapa na tutaupeleka kwenda kuuhifadhi, kipekee tumshukuru pia Balozi wetu, Dk. Migiro (Asha-Rose Migiro), Balozi wa Tanzania Uingereza) amekuwa kiungo muhimu licha ya taratibu nyingi za kirasimu,” alisema.

 

Akizungumzia kauli ya Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Mollel, aliyesema baada ya kufariki Dk. Macha, wabunge wenye ulemavu wamepata pengo kwa sababu sasa wamebaki watatu, Ndugai, alisema ndani ya Bunge walemavu wapo wengi tu.

“Amina Mollel alipokuja kusimama hapa kuzungumza alisema wamepungua na wamebaki watatu tu, mimi nakubaliana naye kabisa ni kweli wamepungua lakini nataka nimpe moyo kidogo mimi ninavyojua kama spika walemavu bungeni wapo wengi.

“Wale wote unaowaona bila kuvaa miwani hawaendi, wengine tulipokuja bungeni mara ya kwanza tulikuwa na nywele kamili na sasa hivi sijui zimeenda wapi huo nao ni ulemavu, kuna mwingine akiongea tu kichwani unasema eeeh.

“Kuna ulemavu wa aina nyingi lakini tunatofautiana katika hilo, kwa hiyo nampa moyo Mollel kwamba tupo wengi, waheshimiwa wabunge kweli si kweli, kweli na hao nao wapo,” alisema.

MBOWE

Kwa upande wake, Mbowe, alisema: “Nitoe shukrani kwa wabunge kupitia makundi mbalimbali, mmekuwa wepesi sana kutufariji si tu kwa michango lakini salamu pia, mama Macha licha ya kuwa mlemavu ingawa sioni ulemavu wake, kwa sasa tunapendana na kuheshimiana kwa kuogopa kifo.

“Lakini kungekuwa na kifo kila mara hapa tungependana, lakini tutumie kifo kama fumbo, mapenzi haya yasiwe mapenzi ya shaka, urafiki huu usikome baada ya kumlaza ya mama Macha,” alisema.

Mbowe pia alimshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kuwatia moyo Chadema pamoja na Dk. Migiro na ofisi ya Bunge kuweza kushirikiana nao hadi kufikisha mwili huo nchini.

Pia alisema Dk. Macha alifanya mambo mengi makubwa wakati wa uhai wake na alikuwa ni mtu wa kusaidiwa lakini alipigana kuwasaidia hata waliokuwa na viungo vyote.

“Amewasaidia watu wengi sana wakiwamo yatima na tuwaombee uvumilivu, mama yake mzazi tunamwombee uvumilivu kwa kumwona mwanawe anayemtegemea sana akiwa amemwacha. Amefanya mengi ya kimiujiza, ametuacha tukitafakari thamani ya maisha, asante Mungu kwa uhai wa Macha.

 “Msiba kila siku kwetu ni darasa na kwa namna ya kipekee niwashukuru spika, naibu spika na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila kwa namna walivyoubeba msiba,” alisema Mbowe.

Naye Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, aliyeenda kuupokea mwili wa marehemu Dar es Salaam na kuuleta Dodoma, alisema katika jambo ambalo hawakutarajia, walivyofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) walikuta kundi la walemavu waliofika kuaga mwili huo.

“Walikuwapo uwanjani kuja kumwaga ndugu yao, kwa maelezo waliyotupa wameelezea kwa uzito kuhusu sifa za Macha, wamesikitika pamoja nasi lakini wameonesha imani yao kwamba yale aliyokuwa akiyasema yatapata nafasi kwa Serikali kuyasemea,” alisema Dk. Tulia.

Kwa upande wake Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema moja ya eneo ambalo marehemu alilikazania akiwa bungeni mbali na kundi la walemavu, alitoa mchango wake kwenye sekta ya elimu.

“Tutaendelea kutekeleza yale aliyokuwa akiyapigania na kikubwa ni kumwombea ili kuweza kuiweka roho ya marehemu mahali pema peponi,” alisema Majaliwa.

Naye Mbunge wa Urambo (CCM), Magreth Sitta, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wabunge Wanawake (TWPG), alisema kifo cha Dk. Macha ambaye ameacha mtoto mmoja kimepunguza idadi yao kutoka 145 hadi 144.

Alisema maisha ya Dk. Macha bungeni ni kiashiria tosha kwamba inatakiwa wapendane wakati wote.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles