27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

Makundi yapigana vikumbo kwa Lowassa

(FILES) An undated file photo shows TanzNa Mwandishi Wetu, Arusha
MAKUNDI ya watu wa kada mbalimbali yamezidi kutua nyumbani kwa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM), yakimtaka achukue fomu ya kuwania urais kupitia CCM muda utakapofika.
Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani, kwa wiki kadhaa sasa amekuwa akipokea wageni wa makundi mbalimbali nyumbani kwake wakimtaka awanie nafasi hiyo ya uongozi wa juu wa nchi.
Kutokana na joto hilo la urais ndani CCM, jana makundi mawili ya wana CCM yalibisha hodi nyumbani kwa kada huyo na kumshawishi kufanya hivyo pamoja na kumkabidhi fedha za kuchukulia fomu.
Kundi la kwanza lilikuwa ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arumeru ambao waliwasilisha ombi lao kwa mbunge huyo pamoja na kumkabidhi Sh milioni moja za fomu.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti Mstaafu wa Halmashauri ya Meru, John ole Saitabau, alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuona Lowassa ana sifa zote za kuwania nafasi hiyo ya uongozi wa nchi.
“Sisi tumekuja hapa kukushawishi uchukue fomu ya kuwania urais kupitia chama chetu cha CCM… uwezo huo unao na Tanzania inakuhitaji,” alisema ole Saitabau.
Naye Mathias Manga, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (MNEC), alisema zaidi ya asilimia 75 ya wajumbe wa NEC wanamshawishi Lowassa awanie urais kwa sasa kutokana na sifa yake ya uchapakazi mbele ya jamii.
Kundi la pili ambalo lilifika nyumbani kwa Lowassa ni la marafiki wa Lowassa, Kanda ya Kaskazini, ambako zaidi ya watu 500 kutoka kada mbalimbali wakiwamo walemavu wa macho na watu wenye albino, walimkabidhi Lowassa Sh milioni 2.5.
Akisoma risala kwa niaba ya vijana waliotoka katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, Protas Soka, alisema kwa sasa Watanzania wanamuhitaji Lowassa aweze kuliongoza Taifa.
“Kwa lugha nyingine Lowassa sasa tunakuomba utangaze nia ya kuingia kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwaka huu wa 2015 wewe ni tumaini la walio wengi hapa kwetu Tanzania,” alisema.
Vilevile, Jumamosi iliyopita Uongozi wa Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA), ulimtembelea Lowassa na kumkabidhi Sh milioni moja za kuchukulia fomo ya urais ndani ya CCM muda utakapofika.
Mwenyekiti wa shirika hilo, Matondo Masanja, akisoma risala yao kwa Lowassa, alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kumuona Lowassa ndiye mtu sahihi kumrithi Rais Jakaya. Kikwete.
Lowassa na maombi kwa Mungu
Akizungumza baada ya kupokea maombi hayo, Lowassa aliwashukuru kwa imani kubwa waliyoionyesha kwake na kuwaambia wamuombe Mungu jambo hilo liende salama.
“Naendelea kumuomba Mungu ajalie atimize ndoto ya safari ya matumaini,” alisema Lowassa.
Alisema anajivunia mafanikio aliyoyapata wakati akiwa mdhamini wa Umoja wa Vijana wa CCM ambako alisimamia Umoja huo kupata kitega uchumi kikubwa. Jengo hilo liko makao makuu ya Umoja huo Dar es Salaam.

Viongozi wa Serikali, Chama na wafugaji wa kutoka Wilaya ya Mkinga walifungua njia ya kumchangia fedha za kuchukulia fomu Lowassa kwa kumpatia Sh 200,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles