24.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

TAKUKURU watua bandari Dar

Na Masyaga Matinyi, Dar es Salaam
TAASISI ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) imeanzisha uchunguzi kubaini mianya ya rushwa na ukiukwaji wa taratibu katika mradi wa ujenzi wa mlango wa Bandari ya Dar es Salaam (Gerezani Creek).
Mradi huo ulisainiwa Septemba 6, 2014 na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Joseph Msambichaka na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Madeni Kipande, ambaye amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi yake.
Kipande alisimamishwa kazi na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Februari 16, mwaka huu baada ya kuwapo tuhuma nyingi kutoka kwa wafanyakazi wa TPA na wadau wa bandari kuhusu matumizi mabaya ya madaraka, ukiukwaji wa taratibu za utumishi na ubadhirifu.
Kwa mujibu wa mkataba huo, kampuni ya Impala Terminals Group ndiyo itasimamia na kujenga mradi huo ambao wanasheria wa TPA waliweka bayana kuwa hauna maslahi kwa Taifa na kukataa kusaini.

Mkataba huo unaelezwa kuwa ni sawa na kuuzwa kwa sababu unaeleza kuwa mbia atakayeshindwa kuongeza fedha za uwekezaji atapoteza hisa zake.
Mtanzania limebaini kuwa Januari 7, 2015, TAKUKURU walimwandikia Kipande barua yenye kumbukumbu PCCB/HQ/RB/63/2014, wakimtaka kuwasilisha nyaraka kadha wa kadha ambazo alitakiwa kuziwasilisha Makao Makuu ya taasisi hiyo Januari 14, 2015.
Miongoni mwa vielelezo ambavyo Kipande ametakiwa kuviwasilisha TAKUKURU ni barua yenye kumbukumbu DG/03/03/06 ya Juni 12, 2014 kutoka TPA kwenda kwa Waziri wa Uchukuzi, kumbukumbu za kikao Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu ya Bodi ya Wakurugenzi kilichofanyika Tanga, Septemba 17 na 18, 2014.
Nyaraka nyingine ni ripoti ya awali ya mchanganuo wa mradi huo kutoka Kitengo cha pamoja cha Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika Wizara ya Fedha, barua ya Oktoba 31, 2014 yenye kumbukumbu DG/03/03/06 kutoka TPA kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi na barua yenye kuonyesha kukubaliwa kwa pendekezo la mradi huo kutoka Wizara ya Uchukuzi.
Nyingine ni mkataba wa makubaliano kati ya kampuni ya Impala Terminal na TPA, kumbukumbu za vikao vyote kati ya Impala Terminal na TPA, barua ya Novemba 11, 2014 yenye kumbukumbu DG/4/1/01 kutoka TPA kwenda kwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi na taarifa ya Kamati ya Wataalamu wa TPA waliofanya utafiti kuhusu faida za mradi huo.
Eneo la Gerezani Creek linaanzia mahali ambako boti zinazoenda Zanzibar hupakia abiria na ile njia inayopita nyuma ya jengo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) maarufu kwa jina la Strong Room, Kituo cha Kati cha Polisi na kuingia bandarini.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo wiki mbili zilizopita, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPA, Joseph Msambichaka, alisema hawezi kusema lolote kwa sababu yeye ni Mwenyekiti wa Bodi na si mtendaji.
MTANZANIA pia ilimtafuta Kaimu Mkurugenzi aliyesimamishwa Kipande ambaye ingawa amekuwa akipokea simu, anapoulizwa tu hukata simu na pia hajibu ujumbe mfupi wa maandishi (sms).
Wakati Kipande akitakiwa kuwasilisha nyaraka hizo, gazeti hili awali liliripoti kuwa hadi sasa anakabiliwa na mashitaka ya ubadhirifu na rushwa na alipaswa kupandishwa kizimbani tangu 2010, lakini haijajulikana sababu ya kutofikishwa mahakamani.

Kabla ya kuteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu (TPA), Kipande alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani katika Wizara ya Miundombinu.

Taarifa zinasema kuwa akiwa Wizara ya Miundombinu mwaka 2008 alituhumiwa kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu kwa kushirikiana na mmoja wa aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).

Vyanzo vyetu vilisema; “Hawa walikuwa wakituhumiwa kutumia fedha za Serikali katika kutengeneza matangazo yanayotoa ujumbe wa usalama barabarani na kuyarusha katika Televisheni ya Taifa, matangazo ambayo gharama za utayarishaji zilipandishwa tofauti na gharama halisi na kuisababishia Serikali hasara ya mamilioni ya fedha.

“Tuhuma hizi ziliripotiwa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mwaka 2008 ziweze kufanyiwa uchunguzi na kubaini kama watuhumiwa walihusika katika ubadhirifu huo.

“Kama ilivyo kawaida, TAKUKURU tulianza kufanya uchunguzi wetu ambako watuhumiwa walihojiwa pamoja na baadhi ya mashahidi na jalada la uchunguzi lenye nambari PCCB/KND/ENQ/05/2008 lilifunguliwa.

“TAKUKURU tulifanya kazi yetu ya uchunguzi na kuikamilisha na kama ilivyo kawaida jalada husika lilipelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) tarehe 25/01/2010 kwa ajili ya kuombewa kibali cha mashtaka.

“Oktoba 23, mwaka 2012 jalada husika lilirudi kutoka kwa DPP likiwa na kibali cha mashtaka kwa maana kwamba Kipande pamoja na mwenzake walipatikana na tuhuma, hivyo kuruhusu TAKUKURU kuwafikisha mahakamani,” kilisema chanzo hicho.

Wakati akimsimamisha kazi Kipande, Waziri Sitta alinukuliwa akisema tangu ameingia wizarani hapo, amekuta matatizo makubwa ya utendaji yanayomhusisha Mtendaji Mkuu Kipande moja kwa moja.
Matatizo hayo ni pamoja na uhusiano mbaya kati yake na wadau na wateja wa mamlaka, kukiuka kwa makusudi kwa taratibu za ununuzi na uhusiano mbaya kati yake na wafanyakazi wa mamlaka kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles