27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 21, 2023

Contact us: [email protected]

Makontena yaliyokwepa kodi zafika 2,431

IMGS3818NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amefanya tena ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kubaini kuwa idadi ya makontena yaliyotolewa bila kulipa kodi ya Serikali yamefika 2,431.

Novemba 27, Majaliwa alifanya ziara kama hiyo bandarini hapo na kubaini kuwapo makontena 349 yaliyotoroshwa bila kulipiwa kodi.

Mbali na hilo, alimtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Hebel Mhanga, hadi kufikia jana saa 11 jioni, kumpelekea ofisini kwake majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi huo.

Akiwa katika bandari hiyo, Majaliwa alisema taarifa za ukaguzi zilizopo zinaonyesha kuanzia Machi hadi Septemba 2014, makontena hayo yalipita bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu nne (ICDs) ambazo ni Jefang, DICD, PMM na Azam.

Pia, alimpa meneja huyo wiki moja kuhakikisha mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo kutoka kwenye ‘billing system’ badala yake waweke mfumo wa malipo wa kielektroniki uitwao e-payment.

Miongoni mwa mifumo aliyoiangalia ni ya upokeaji na utoaji mizigo pamoja na utozaji wa malipo, na aliikagua baada ya kupewa taarifa kwamba kuna makontena 2,431 yametolewa bila kulipiwa ushuru.

Majaliwa aliangalia mifumo hiyo jana wakati akikagua idara mbalimbali za Mamlaka ya Bandari na kuona ukaguzi wa mizigo unavyofanyika kwa kutumia mashine maalumu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni watumishi 10 tu ndio waliosimamishwa kazi kutokana na makosa hayo.

“Mmeamua kuwasimamisha kazi watu wadogo na kuwaacha wakubwa wanaendelea na kazi. Hatuwezi kuendelea kuikosesha Serikali mapato namna hii,” alisema.

Akiwa kwenye chumba cha scanner mojawapo, Waziri Mkuu alikuta manifest moja ikisema kontena limejaa diapers, lakini picha ya kwenye kompyuta ya scanner ilionyesha kuwa ndani ya kontena hilo kuna vitu kama vifaa vya umeme.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa Bandari upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ben Usaje ambaye pia ni msimamizi wa kitengo cha scanner, inapobainika taarifa kama hiyo, inapaswa itumwe kwa wenye bandari kavu ili wafanye ukaguzi kwa kulifungua kontena kuhakikisha mali zilizomo ndizo zilizoandikishwa kwenye manifest.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa alifanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) jijini Dar es Salaam na kukagua mabehewa yaliyokuwapo kisha alizungumza na baadhi ya wafanyakazi waliokuwa eneo la stesheni.

Akiwa hapo, Waziri Mkuu aligundua ‘madudu’ kwenye malipo ya mishahara na makato ya michango ya wafanyakazi.

Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa TRL, Elias Mshana, Waziri Mkuu alisema amefika hapo ili kujifunza utendaji wao wa kazi, lakini anazo taarifa za wao kupewa fedha na Serikali kiasi cha Sh bilioni 13.5 ili waendeleze miundombinu ya reli, lakini hawakufanya hivyo.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU), Boaz Nyakeke, alimwambia waziri mkuu kuwa wafanyakazi wanadai malimbikizo ya makato yao kwenye mifuko ya pensheni, makato kwenye SACCOS na malimbikizo ya mshahara kuanzia Julai hadi Novemba 2014.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles