23.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo TRA wakutwa na mamilioni nyumbani

MPANGO*Bosi mpya awataka watumishi wote kutaja mali zao

Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam

SIKU chache baada ya kigogo mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kubainika kumiliki nyumba 73, wafanyakazi wengine wa mamlaka hiyo wamekutwa na mamilioni ya shilingi waliyoficha majumbani mwao.

Taarifa kutoka ndani ya TRA zinapasha kuwa tangu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa awasimamishe kazi maofisa kadhaa wa mamlaka hiyo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na kitengo cha uchunguzi cha mamlaka hiyo, hivi sasa wapo kwenye msako wa kubaini ukwasi wa wafanyakazi wake.

Chanzo chetu cha kuaminika kilisema kuwa juzi maofisa wa kitengo cha uchunguzi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, walifika katika eneo la Tegeta Salasala wilayani Kinondoni na kuvamia nyumba mbili za wafanyakazi wa mamlaka hiyo.

Katika nyumba hizo, wafanyakazi hao kila mmoja alikutwa na kiasi kikubwa cha fedha ndani kuliko kiwango cha mshahara anaolipwa.

“Walivamiwa wafanyakazi wawili (majina yanahifadhiwa), ambapo katika kila nyumba zilikutwa fedha nyingi. Kwa mtu wa kwanza zilikutwa Sh milioni 200 na yule wa jirani yake pia alikuwa na zaidi ya shilingi milioni 150.

“Tangu kuanza kwa msako huu wafanyakazi wengi wamekuwa hawana amani kabisa, na hata wengine wanasema wazi kama wangekuwa na uwekezaji wa nje ya nchi wangeondoka kabisa nchini,” kilisema chanzo chetu.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wafanyakazi hivi sasa wamelazimika kuzikimbia nyumba zao na kuishia kulala hotelini huku wakienda kazini wakiwa na hofu.

Hivi karibuni, vyombo vya habari viliripoti kuwa Kamishna wa Forodha wa TRA, Tiagi Masamaki, aliyesimamishwa kazi pamoja na vigogo wengine wa mamlaka hiyo kutokana na upotevu wa kontena 349 zenye thamani ya Sh bilioni 80, amebainika kumiliki nyumba 73.

 

KAULI YA KOVA

MTANZANIA ilimpomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alisema hawezi kuzungumzia suala la uchunguzi ulipofikia kwani suala hilo lipo ngazi za juu.

“Siwezi kuzungumzia hilo kwani kwa sasa lipo ngazi za juu kwa ajili ya uchunguzi wa kina,” alisema Kova.

TAMKO LA MALI NA MADENI

Katika hatua nyingine, Kaimu Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Dk. Philip Mpango, ameibuka na kuwataka watumishi wote kuwasilisha fomu za tamko la mali na madeni yao kwa mwaka 2015 kabla ya Desemba 15.

Waraka huo umekuja siku chache baada ya Serikali kuwasimamisha kazi vigogo sita wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akiwamo Kamishna Mkuu, Rished Bade kutokana na upotevu wa kontena 349.

Taarifa za ndani ambazo MTANZANIA imezipata, zinasema kuwa kaimu kamishna huyo, amewaandikia watumishi hao waraka akiwataka kuwasilisha fomu hizo tarehe hiyo badala ya Machi 31 mwakani.

Gazeti hili lina nakala ya waraka huo ambao umesainiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Ndani, Stella Cosmas.

Waraka huo, ulieleza kuwa agizo hilo linajumuisha pia watumishi wanaowasilisha matamko yao Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

“Tafadhali zingatieni kwamba kwa maelekezo haya tarehe ya mwisho ya kuwasilisha fomu za tamko la mali na madeni imebadilika kutoka Machi 31 mwaka 2016 na kuwa Desemba 15, mwaka huu.

“Kama kawaida, matamko yote yawasilishwe kupitia mfumo wa ARUTI isipokuwa watumishi wanaowasilisha matamko yao Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,” ilisema sehemu ya waraka huo.

Kwa mujibu wa waraka huo, mtumishi yeyote ambaye atashindwa kuwasilisha au kuwasilisha tamko lisilo sahihi, atachukuliwa hatua kali za kinidhamu kama ilivyoainishwa kwenye kanuni za utumishi za Serikali na za Mamlaka ya Mapato.

Aidha waraka huo ulieleza kuwa kwa wale watumishi wapya, wanakumbushwa kuwasilisha matamko yao ndani ya wiki mbili baada ya kuripoti kazini.

 

ZIARA YA MAJALIWA

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alifanya ziara ya kushtukiza kwenye bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kukagua utendaji kazi, hasa kitengo cha kupokea mizigo kutoka nje ya nchi, kabla ya kufanya kikao na maofisa wa juu wa kitengo hicho na wale wa bandari.

Katika kikao hicho, alitangaza kuwasimamisha kazi maofisa watano wa TRA na kumwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu kuwakamata ili wasaidie upelelezi wa upotevu wa kontena 349 zenye thamani ya Sh bilioni 80 sambamba na kuzuia hati zao za kusafiria.

Baadaye, Rais Dk. John Magufuli alitangaza kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Bade kutokana na upotevu huo wa kontena.

Majaliwa alichukua uamuzi huo baada ya kuzungumza na viongozi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) pamoja na wa TRA, ambapo pia alimtaka Bade na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Lusekelo Mwaseba, washirikiane na polisi kufuatilia upotevu huo na kuhakikisha fedha hizo zinapatikana na kurudishwa serikalini.

Aliwataja maofisa waliosimamishwa kazi kuwa ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya.

“Hawa wanasimamishwa kazi. IGP ninaagiza hawa watu wakamatwe na kuisaidia polisi. Hati zao za kusafiria zikamatwe na mali zao zikaguliwe kama zinaendana na utumishi wa umma,” alisema Waziri Mkuu.

Maofisa wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari (hakutaja ni wa idara gani) na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD In-Charge), Eliachi Mrema.

Pia aliagiza watumishi watatu wa mamlaka hiyo wahamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani, ambao ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni ambao baadaye walitangazwa kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles