Makamba: Nimechoka yanayoendelea

0
1684
KATIBU Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba

FARAJA MASINDE Na RENATHA KIPAKA-DAR/ BUKOBA

KATIBU Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, amesema kuwa amechoka na yanayoendelea ikiwamo kusumbuliwa kwa kuulizwa kuhusu suala la wito wake wa kwenda kuhojiwa na Kamati ya Usalama na Maadili ya Taifa ya chama huku akitaka wahojiwe kamati hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya hivi karibuni, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kuagiza waitwe na wahojiwe makatibu wakuu wasaafu wa CCM, Yussuf Makamba, Abdulrahman Kinana na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bernard Membe.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana, akiwa kijijini kwake Mahezangulu wilayani Lushoto, Halmashauri ya Bumbuli, Makamba alisema kwa sasa wanaopaswa kuulizwa suala la barua ni wenye mamlaka ndani ya chama na si yeye.

 “Wewe bwana hebu sikiliza, unajua mimi nawaheshimu sana ninyi (vyombo vya habari) lakini sasa mnanichosha, mimi niko kwetu kijijini Mahezangulu Bumbuli nakula Krismasi, nafurahia kuzaliwa kwa Yesu Kristu ninyi mnanisumbua kila wakati barua barua…

“Sasa mimi nimesikia kama wewe, wanataka kuniona, mimi niko kwetu Bumbuli nakula Sikukuu unaniuliza mimi, waulize wao (CCM) waliosema wanataka kuniandikia, sasa hivi nimechoka na mimi naomba unisaidie kuwaambia kuwa ‘I’m very tired’ kuulizwa juu ya jambo moja tu kuna nini humu kwenye barua?.

“Inachosha sana, wenzenu wanasheherekea kuja kwa Yesu ninyi mnasheherekea barua, wenzenu Yesu amezaliwa wako kwenye Sikukuu ninyi mnahangaika na barua ni Mahakama Kuu? Kwamba mzee Makamba anaitwa Mahakama Kuu kwamba akishindwa ameuawa?..ah No (hapana),” alisema Makamba.

CHANZO CHA BARUA

Kiini cha mzozo uliosababisha viongozi hao kutaka kuketishwa kwenye kamati ya maadili ya viongozi wa chama hicho, ambapo Julai 14, mwaka huu, Makamba na Kinana kuandika waraka wakiuelekeza kwa Katibu wa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa chama hicho, Pius Msekwa.

Katika waraka huo walikuwa wakilalamikia udhalilishwaji uliodaiwa kufanywa na mwanachama wa chama hicho, Cyprian Musiba, ambaye alikuwa akijinasibu kama mtetezi wa Rais Magufuli, ambapo utetezi wake ulienda mbali zaidi kwa kutaja majina ya viongozi hao kama miongoni mwa wanaomhujumu Rais. 

Waraka huo si tu uliigawa CCM, bali pia ulileta taharuki kubwa ambapo baadhi ya makada wakiwamo wabunge, wakuu wa wilaya na mikoa, waliwapinga na kuwatusi wastaafu hao huku wengine wakiwaunga mkono.

Mzozo wa waraka huo ulisababisha udukuzi wa sauti zinazodaiwa kuwa ni za Kinana, Makamba na Membe.

Mbali na hao, wengine waliodukuliwa wakidaiwa kumtusi Rais John Magufuli ni Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

 Katika udukuzi huo ambao hadi leo haijafahamika kuwa ulitekelezwa na nani, sauti ya Nape ilisikika akizungumza na Kinana, Nape pia alinaswa na Ngeleja, Makamba na mwanae January wakiwa pamoja na Nape na Membe ambapo alisikika akizungumza na kada mmoja wa CCM ambaye bado hajafahamika.

 Lakini siku chache baadaye, Nape, January Makamba na Ngeleja kwa nyakati tofauti waliomba msamaha kwa Rais Magufuli na kusamehewa huku kikao cha NEC kilichofanyika hivi karibuni jijini Mwanza, kikibariki msamaha kwa wabunge hao, hata hivyo wakati wao wakiomba msamaha Membe hajajitokeza hadi sasa.

UAMUZI WA CCM

KATIBU Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba

Agizo hilo la kutaka kuandikiwa barua kwa makada hao wa CCM, Makamba, Kinana na Membe, ni kutokana na kukabiliwa na makosa ya kimaadili, ambapo wanadaiwa kutoa lugha isiyofaa dhidi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Magufuli baada ya sauti zao kudukuliwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii Julai 14, mwaka huu.

Maazimio hayo ya kutaka kuwaita Makamba, Kinana na Membe, yalipitishwa Desemba 13, mwaka huu na NEC, iliyoketi jijini Mwanza chini ya mwenyekiti wake Rais Dk.  Magufuli.

MAAZIMIO YAVYOFIKIWA 

Desemba 13, taarifa iliyosainiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, ilieleza kwamba  kikao hicho cha NEC kilikuwa ni cha kawaida kwa mujibu wa Katiba ya CCM.

Alisema pamoja na mambo mengine, NEC ilipokea, kujadili na kuridhia kwa kauli moja taarifa ya Kamati ya Usalama na Maadili juu ya uamuzi wa Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais John Magufuli wa kuwasamehe wanachama walioomba radhi kwake baada ya kukiri mbele yake kufanya makosa ya kimaadili yaliyokidhalilisha chama na viongozi wake mbele ya umma. 

“Halmashauri Kuu ya Taifa pia imeazimia kwa kauli moja na kuelekeza kwamba wanachama, Abdulrahman Kinana, Mzee Yusuf Makamba na Bernard Membe waitwe na Kamati ya Usalama na Maadili ya Taifa ili wajibu tuhuma za kimaadili zinazowakabili kwa mujibu wa katiba ya chama na kanuni ya maadili na uongozi,” ilieleza taarifa hiyo ya Polepole.

Hata hivyo MTANZANIA Jumapili, ilimtafuta Polepole, ili kutaka kujua kama vigogo hao wameshaandikiwa barua za kuitwa lakini hakupatikana yeye wala Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula.

DK. BASHIRU ATOA AGIZO

Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally

Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally ameagiza kuwafukuza wanachama wote watakaovunja umoja ndani ya chama kwa tabia, pamoja na mitindo ya maisha.

Kauli hiyo aliitoa mjini Bukoba mkoani Kagera jana, alipokutana na viongozi wa CCM, ambapo alisema kuwa hawatawavumilia watu wanaotaka kukivuruga chama baada ya kukijenga hasa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

“Siko tayari kuona mtu anavuruga chama, tutawaafukuza mapema tu, maana hao ndiyo wavurugaji. Na ili kukiimarisha kila mmoja anatakiwa kusimamia kanuni ikiwa ni pamoja na kuondoa wote wenye mwenendo mbovu hawafai kuwamo katika chama,” alisema Dk. Bashiru 

Alisema Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), imeshagiza ifanyike tathmini za kubaini wote ambao walivujisha siri za vikao watafutwe mara moja kisha wachukuliwe hatua kali za kinidhamu za chama.

“Nitumie nafasi hii kwa kuwapongeza wanachama wa CCM ambao wanakubali kujitolea bila kusubiri posho hasa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa huo ni mwanga mzuri katika kukijenga chama chetu,” alisema

SARE ZA CHAMA 

Katika hatua nyingine Dk. Bashiru, alisema kuwa katika uchaguzi ujao wa mwakani hakutakuwa na fulana zitakazotolewa bure wala kuchangishwa matajiri na badala yake kila mwanachama atajinunulia sare mwenyewe kwa fedha yake.

“Mjue tu wanachama wenzangu hakuna cha bure hapa mjipange kutafuta pesa wenyewe za kuwalipa mawakala, vocha, vyakula kwa ajili ya vijana ambao watakuwa katika mchakato wa uchaguzi lakini pia wasichague vyakula,” alisema Dk. Bashiru

Mtendaji huyo wa CCM, alisema kuwa hali hiyo haimaanishi watu wasichangie ila iwe kwa usafi na kwa njia za halali zinazotambulika na chama.

Alisema maamuzi ya chama hayafanywi kwenye mitandao ya kijamii bali hufanyika kwenye vikao kwa mujibu wa katiba, kanuni na miongozo ya chama.

“Kuna watu wanachafuliwa kwenye mitandao ya kijamii wakati hawana nafasi ya kujitetea hilo ni kosa kubwa. Mambo ya chama yanafanywa kwa kufuata kanuni na si kupeleka mambo hadharani,” alisema 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here