26.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Makala| Ni kweli chanjo ya Corona inaathiri uzazi?

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

TANGU kuanza kutolewa kwa chanjo ya Corona duniani, huku kwa Tanzania ikianza Julai 28, mwaka huu, zilikuwapo dhana mbalimbali juu yake, kubwa zaidi yakiwa ni madai kuwa zinaathiri mfumo wa uzazi.

Katika hilo, wapo waliosikika wakivumisha kuwa iwapo mwanamke au mwanamume atapata chanjo hiyo basi atakuwa kwenye hatari kubwa ya kuathiri mfumo wake wa uzazi.

Dk. Emmanuel Tluway anayefanya kazi na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kulia, akifuatiwa na Dk. Arkan Ibwe anayetoa huduma za matibabu kwa raia wa Marekani walioko kwenye maeneo mbalimbali nchini akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 10 wakizungumza Waandishi wa Habari.

Aidha, wapo waliosema chanjo ya Corona itaweza kumsababisha mtu apoteze mwonekano wake wa kibinadamu na kugeuka ‘Zombi’.

Ni katikati ya ukakasi huo ndipo wataalamu wanaofanya kazi na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania wanaibuka na kujaribu kuondosha dhana hizo potofu.

Dk. Arkan Ibwe anayetoa huduma za matibabu kwa raia wa Marekani walioko kwenye maeneo mbalimbali nchini akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 10, anasema taarifa juu ya chanjo kuathiri mfumo wa uzazi si za kweli.

“Niseme tu, jambo hili hilo ni uzushi mtupu ambao unapaswa kupingwa kwa nguvu zote,” anasema Dk. Ibwe na kutupa swali kwa mwandishi wa makala haya akiuliza, ‘unajua kwa nini?’

Naye mwandishi wa makala fupi haya anajibu, ‘sijui, ni maneno ambayo yapo mitaani kwamba ukichanjwa utapata changmoto ya uzazi’.

Dk. Ibwe anacheka na kisha anasema: “Huo ni uzushi tu ambao hata mimi nimeuona kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, watu wakisema kwamba hawawezi kuchanja chanjo ya Corona eti sababu bado hawana watoto au watakosa watoto huko baadaye na mambo mengine mengi.

“Lakini ukweli ni kwamba mfumo wa chanjo kwenye mwili wa binadamu hauingiliani kabisa na ule wa uzazi. Hiyo ni mifumo miwili tofauti kabisa.

“Jambo la msingi ni kwamba wanajamii kujitahidi kutafuta taarifa sahihi kila wakati na kuacha kukumbatia na kuamini uzushi huu wa kwenye mitandao ya kijamii,” anasema Dk. Ibwe.

Pia, anafafanua kuwa chanjo hiyo ya Corona haiwezi kuathiri mwili kiasi cha kusababisha mtu kugeuka mwonekano wake kama ambavyo imekuwa ikizushwa kwenye tovuti na mitandao mbalibali ya kijamii.

“Ndiyo maana hata kwenye changamoto ya damu kuganda ni kutokana na mzio (allergy) ambao anakuwa nao mtu kulingana na chembechembe zilizotumika kutayarisha chanjo hiyo na ndiyo maana tunawashauri watu kumuona daktari.

“Hivyo niwaombe Watanzania wajitokeze kupata chanjo bila kuwa na hofu ya kukosa watoto mbele ya safari,” anasema Dk. Ibwe.

Chanjo inavyofanya kazi

Akizungumzia namna chanjo hiyo ya Corona inavyofanya kazi mwilini, Dk. Emmanuel Tluway anayefanya kazi na Shirika la Misaada la Marekani (USAID), anasema:

“Kazi kubwa ya chanjo kama hii ya Johnson and Johnson ni kuhakikisha inaenda kusisimua au kuamsha kinga ya mwili wako ili ziweze kupambana na virusi hivi vya Corona,” anasema Dk. Tluway.

Je, mtu aliyeugua Corona mawimbi yote matatu na akapona ana haja ya chanjo?

Dk. Tluway anasema mtu aliyeugua Corona mawimbi yote matatu na akafanikiwa kupona bado anastahili kupata chanjo.

“Mtu kama huyo anastahili kupata chanjo ya Corona kwani hiyo ni kielelezo kwamba kinga ya mwili wake imekuwa ikishindwa kukabiliana na kirusi, hivyo anapona na kurejewa na ugonjwa.

“Niwashauri watu wa namna hii kuhakikisha wanafika kwenye vituo kupatiwa chanjo ili kuimarisha kinga zao za mwili,” anasema Dk. Tluway.

Faudhia Omary (31), mfanyabiashara na mkazi wa Mikocheni, Dar es Salaam, anasema hayuko tayari kupoteza kizazi chake na kwamba Mungu atamtetea.

“Binafsi bado kwangu hamjanishawishi, ikizingatiwa kuwa bado sina mtoto na hayo ninayoyasikia ndiyo kabisa. Hawa watu hawaaminiki ndugu yangu, naamini Mungu atanitetea, maana bado sijawaleta wajomba zako duniani, hivyo isije kuwa nikichanja ndio basi tena,” anasema Faudhia.

Kwa mujibu wa Balozi wa Marekani hapa nchini ambaye pia ni daktari wa binadamu kitaaluma, Dk. Donald Wright, anasema ni muhimu kwa Watanzania kupata chanjo ya Corona kwani inapunguza kasi ya maambukizi mapya.

Akitolea mfano nchini Marekani, Dk. Wright anasema zaidi ya asilimia 99 ya vifo vipya vionavyotokana na Corona ni vya watu ambao hawakuchanja. “Ukweli mwepesi ni kuwa chanjo hizi zinaweza kuokoa maisha yako au ya mpendwa wako.

“Ndiyo maana Serikali ya Marekani imeendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha Watanzania wanapata chanjo ya Corona,” amesema Balozi huyo.

Zoezi la chanjo linaendelea kwenye maeneo mbalimbali nchini, huku viongozi mbalimbali wakiwa tayari wameshachanjwa, wakiongozwa na Rais Samia Suluhu.

Dk. Alfreda Onesmo anasema chanjo hiyo haina uhusiano na mfumo wa uzazi hivyo ni uvumi tu kutoka kwa watu wachache ambao wamekuwa wakipotosha watu.

“Ndugu yangu watu wasikudanganye hakuna uhusiano wowote kati ya chanjo hiyo na mfumo wa uzazi, watu waache kupotosha wenzao, ushauri wangu kwa mtu ambaye hataki kuchoma labda kama ana sababu nyingine lakini siyo sababu ya kuathiri uzazi,”amesema Dk. Onesmo.

Upande wake, Kinoro Mjuni makazi wa Dar es Salaam amesema ifike sehemu watu waache kusingiza chanjo kuwa ndio sababu ya kushindwa kushiriki vyema tendo la ndoa.

“”Hakuna kitu kama hicho, binafsi siamini kama chanjo inaweza kukufanya wewe ushindwe kushiriki vema tendo la ndoa, hivyo watu waache kusingizia chanjo kwani tumeona hata juzi hpa Sheikh wa Mkoa wa Dar s Salaam alitwambia kuwa baada ya kupata chanjo mambondani yamechangamka, hivyo watu waache kudanganyana,”amesema Mjuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles