27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 4, 2023

Contact us: [email protected]

Makala| Alizeti kugeuka tumaini jipya la uchumi Geita?

Na Yohana Paul, Geita

ALIZETI ni miongoni mwa mazao adhimu kwa sasa nchini, hii ni kutokana na kubainika kuwa na faida kubwa kwenye mnyororo wake wa thamani kupitia sekta za kilimo, ufugaji, viwanda na biashara.

Kwa kuliona hilo, Mkoa wa Geita umeanzisha mkakati maalum wa kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti ili kushadadia maendeleo ya kiuchumi sambamba na kupanua uwigo wa ajira kwa makundi tofauti.

Katibu Tawal Msaidizi Uchumi na Uzalishaji mkoani Geita, Titto Mlewa akifafanua juu ya mikakati ya kuinua uzalishaji wa alizeti mkoani hapa.

Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Uzalishaji mkoani Geita, Titto Mlewa akizungumuza na Mtanzania Digital katika mahojiano maalum anaeleza kuwa tayari mipango imeanza kutekelezwa kufikia malengo.

Mlewa anasema malengo ya mkoa kwanza ni kumaliza tatizo la upungufu wa mafuta ya kula kwani mahitaji ni tani 14,001 lakini mpaka sasa hivi mkoa una uwezo wa kuzalisha tani 788.

“Kwa hiyo mradi unalenga kwenda kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula, na tunategemea kuzalisha tani 1,496 (za mafuta ya kula) kwa mwaka huu (2022/23) ambao tunakwenda kuvuna.

“Lakini pia tunataka tuziba lile pengo la malighafi viwandani ambavyo uwezo wake na tunachozalisha kuna uhaba wa asilimia 60 wa malighafi ya viwanda inayotakiwa kuongeza uzalishaji  kwenye kuchakata alizeti.

“Kwa hiyo kusudio letu ni hilo kwenda kupunguza hilo pengo, kwanza ni pengo la mafuta ambayo tunahitaji lakini pili tuweze kuongeza uzalishaji na kukamilisha mahitaji ya viwanda vyetu,” anasema Mlewa.

Kwa mujibu wa Mlewa, tayari wameangalia sababu kubwa zinazowakwamisha wakulima wasijikite kwenye kilimo cha alizeti wamebaini tatizo kubwa limekuwa ni mbegu hivo jitihada zimefanyika kulikabili.

“Kwa mkoa wetu wa Geita, halmashauri zote zimenunua mbegu na zimewapa wakulima hilo ni la kwanza, lakini la pili ni utaalamu kwa hiyo tumejipanga maofisa ughani waweze kuwafikia wakulima.

Anasema kwa msimu huu wa kilimo mkoa umefanikiwa kugawa takribani pikipiki 112 kwa maofisa ughani ili waweze kuwafikia hao wakulima na kufanya mbegu bora ziendane na kilimo bora.

Mlewa anaamini kuwa, mafanikio katika kilimo cha alizeti yatakuwa na tija kubwa katika kuambatanisha unenepeshaji wa mifugo na kudhibiti mlipuko wa gharama za mafuta ya kula na chakula chenyewe.

Hali ya viwanda vya Alizeti

Titto anabainisha, mpaka sasa mkoa umeonekana kuwa na mwamko wa viwanda vya alizeti lakini  vimebainika kukosa malighafi ya kutosha na ndiyo maana mipango imewekwa kuongeza uzalishaji wa alizeti.

“Kwa hiyo mpaka dakika hii alizeti inayozalishwa ni chache kuliko mahitaji ya viwanda, mpaka sasa tuna viwanda 24, kwa mkoa mzima wa Geita ambapo tuna upungufu wa tani 10,000 za malighafi ya alizeti.

“Lakini hadi sasa tuna double refinery (kiwanda kikubwa) kimoja kipo Chato, lakini tumepanga kuongeza nyingine kwenye halmashauri ya mji wa Geita kwa maana hizi single refinery hatuna mpango nazo.

“Tukiongeza uzalishaji ukavuka mahitaji ya viwanda sasa tutaenda kwenye lengo la upande mwingine la kuongeza viwanda,” anasema Mlewa.

Anasema viwanda vyote 24 vina uwezo wa kuchakata tani 14,700 za alizeti ambapo kwa mwaka 2023 mkoa unatarajia kuzalisha tani 4,639 za alizeti na kufanya pengo la malighafi kusalia tani 10,061.

Anasema hadi sasa viwanda  vinatarajia kunufaika na alizeti kutoka kwenye eneo la hekari 11,896 zilizolimwa msimu huu (2022/23) na kuwa na uhakika wa kuzalisha tani takribani 1,496 za mafuta ya kula.

Malengo ya muda mrefu

Anasema malengo ya muda mrefu ni kuwaingiza wakulima wote kwenye jukwaa la mtandaoni, jukwaa ambalo litaonyesha uhalisia wa kiwango halisi cha uzalishaji wa alizeti kila msimu.

Anaeleza, mfumo huo utawasaidia maofisa ughani kutengeneza namna bora ya kufungamanisha uzalishaji wa zao la alizeti sambamba na unenepeshaji wa mifugo.

“Lakini lengo letu jingine kubwa tunataka tukafanye uzalishaji na uuzaji nje ya nchi mafuta ya alizeti na tumeshapata nembo yetu itakayounganisha mafuta yote yanayozalishwa mkoani hapa.

“Sisi kama nchi tunaingia gharama kubwa kuagiza mafuta ya kula kwa hiyo hata tufanyaje ndani ya miaka hii miwili hadi mitatu hatuwezi kutimiliza mahitaji yetu.

“Kwa hiyo tunapambana tuna mipango ya muda mrefu ambayo tutatosheleza ndani ya nchi na sisi kama Geita tukifanya vizuri tutauza kwenda kwenye mikoa mingine,” anabainisha Mlewa.

Mlewa anasisitiza kuwa lengo kuu la kuja na mpango wa mazao ya alizeti ni kutaka kumaliza kabisa suala la uagizaji wa mafuta ya kula nje ya nchi kwa kuwa na uzalishaji imara na kukidhi mahitaji.

“Na dhamira yetu sisi tuwe na uzalishaji ambao ni endelevu na tunataka kwanza tukidhi lile hitaji la tani 14,001 ambalo ni hitaji la mkoa, harafu baadaye tutaweza kuangalia namna gani tunapanua uwigo,” anasema.

Anasema kufikia malengo hayo mkoa wa Geita umeanzisha muundo uitwao ‘Total Solution’ kuanzia eneo la uzalishaji, uchakataji mpaka uuzaji ili kuondoa vikwazo vyote kwenye mnyororo wa thamani wa alizeti.

“Tunatambua ukiwekeza zaidi kwenye uzalishaji ukaacha haya maeneo mengine, lazima kutakuwa na anguko, kwa hiyo tumehusianisha maeno yote matatu, eneo la uzalishaji, uchakataji na uuzaji,” anafafanua Mlewa.

Anasema, hiyo itasaidia kumjengea mkulima uhakika wa soko kabla na baada ya mavuno na hata kumuunganisha mkulima na wachakataji wa mazao kwa ajili ya kumuhakikishia masoko.

“Lengo letu jingine ni kuongeza ajira, kwenye huuu mpango tuna uwezo wa kuzalisha ajira takribani 90,000 pasipo kuangazia eneo la masoko lakini lengo letu ni kufikia mpaka ajira 400,000,” anasema.

Maelekezo ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa

Ili mkoa uweze kufikia malengo yenye tija kupitia kilimo cha alizeti, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Prof. Godius Kahyarara anazielekeza halmashauri zote kuhakikisha zinashiriki kusimamia malengo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Profesa Godius Kahyarara akitoa maelekezo ya ofisi ya mkuu wa mkoa juu ya mikakati ya kuinua kilimo cha alizeti.

Prof. Kahyarara anazitaka halmashauri kubeba jukumu la kutafuta masoko ya mazao ya alizeti ili wakulima wanapovuna wawe na uhakika wa sehemu sahihi ya kuuza kwa tija.

 “Tumenunua mbegu, tumegharamia mbegu, tugharamie na baada ya hapo mavuno yanapelekwa wapi, tumeona kila halmashauri angalau inakiwanda, tunachotoka ni muingiliano wa hivi viwanda.

“Kwani zao hili ni la kimkakati lakini vilevile ni malekezo na ndiyo muelekeo wa nchi, kujitosheleza kwa mafuta ya kula, ni kwa sababu hicho kitu kinawezekana.

“Kwa hiyo kama mkoa sisi tutasimamia, lakini tuhakikishe mbegu zinazopatikana ni mbegu bora, watalaamu mnatasaidia pale ambapo mnaona kuna uwezekano,” anasema Prof. Kahyarara.

Aidha, anazitaka halmashauri zote kuandaa utaratibu mzuri kwa wakulima kupata maarifa ya kile wanachokwenda kukifanya kulingana na mwenedo wa hali ya hewa ya eneo husika.

Prof. Kahyarara anaahidi kuwa mkoa utaanza kwa kufufua viwanda vilivyopo ambavyo havifanyi kazi, na kusimamia kiwanda cha Chato kiweze kupata malighafi ya kutosha kuzalishamafuta.

“Tumesema tuhakikishe kwamba tuna mbegu bora, tunakalenda ya kilimo ambayo inafuatwa, ufuatiliaji kwa mkulima hatua kwa hatua ili kuwezesha uzalishaji wenye tija unafikiwa, Prof. Kahyarara.

Anasema kwa kutumia vikundi vya wajasiliamali vijana, kina mama ma watu wenye ulemeavu ipo nafasi kubwa ya kuongeza uzalishaji na kuwa na uhakika wa ajira kupitia zao la alizeti.

“Hatuwezi kuendelea kulima kwa kutumia mifumo ya kizamani, au viwanda vya teknolojia ya kizamani, tukifanya kazi pamoja kama timu yale ambayo tunaona hayawezekani yatawezekana,” anasema.

Prof. Kahyarara anawashauri maofisa ughani kuwekeza nguvu zaidi kutoa elimu  na kuwafikia wakulima kupitia mitandao kwani ndiyo sehemu ambayo inatembelewa na watu wengi zaidi kwa sasa.

Matarajio ya Wananchi

Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha (Nyabusakama) wilayani Geita, Sakumi Makungu anasema hamasa ya kilimo cha alizeti itawasaidia wakulima kuwa na zao lingine la kimkakati tofauti na zao la pamba.

Anasema mipango iliyowekwa na mkoa inawapa matumaini na huenda ikawainua kiuchumi wakulima wengi kwani tayari wameshuhudia ongezeko la viwanda vya kukamua mafuta ya alizeti.

“Zamani tulikuwa tunalima lakini wakulima hawakuwa wengi, na viwanda vililuwa mbali, tulikuwa tunaondoka zaidi ya kilomita 25 kwenda kupata huduma ya kukamua zao la alizeti.

“Lakini baada ya kupeleka maombi yetu sisi kama ushirika, halmashauri ililiona ikabidi kutusogezea huduma hiyo ya kiwanda cha alizeti na mpaka sasa kiwanda cha alizeti kipo,’ anasema mdau huyo wa kilimo.

Anaongeza, iwapo kutakuwa na usimamizi wa mipango iliyowekwa huenda wakashuhudisa zao hilo linageuka kuwa mhimili wa uchumi kwa wakazi wa Geita na kubadili maisha ya watu wengi. 

Aidha, anabainisha kuwa, changamoto kubwa ni uelewa hafifu miongoni mwa wananchi kuamini kwamba zao la alizeti linachangia udongo kupoteza rutuba na kuharibu mbolea ya asili mashambani hivo elimu iendelee kutolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles