28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Majeraha kuhitimisha safari ya Andy Murry kwenye tenisi

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO

MICHUANO ya tenisi ya wazi maarufu kwa jina la (Australia Open), inatarajia kuanza kutimua vumbi leo kwenye mji wa Melbourne katika viwanja vay Melbourne Park.

Hiyo ni miongoni mwa michuano mikubwa duniani katika mchezo huo, kila staa wa tenisi anatamani kupata nafasi ya kuonesha kipaji chake. Baadhi ya mastaa ambao wametawala kwenye michuano hiyo ni pamoja na Andy Murray, Novak Djokovic, Rafael Nadal, Roger Federer na wengine, lakini michuano hiyo inaweza kuwa ya mwisho kwa Andy Murray.

Murray aliwahi kuwa bingwa wa michuano hiyo mikubwa mara tatu pamoja na mataji mengine mengi, lakini nyota huyo mwenye umri wa miaka 31, mwishoni mwa wiki iliopita aliushtua ulimwengu baada ya kuthibitisha kuwa mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo atatangaza kustaafu.

Michuano hiyo inatarajiwa kumalizika Jumapili ya Januari 27, hivyo staa huyo ambaye ameweka rekodi mbalimbali atawaaga rasmi mashabiki zake kutokana na kusumbuliwa na majeruhi ya muda mrefu.

SPOTIKIKI leo imekuwekea michezo ambayo ilimpa majeruhi na kumfanya wiki iliopita kutangaza lengo la kutaka kustaafu.

Juni 9, 2017

Ilikuwa kwenye michuano ya wazi ya Ufaransa (French Open), ambapo Murray alifanikiwa kufika hatua ya nusu fainali, lakini hakuweza kusonga mbele hatua inayofuata baada ya kukubali kichapo kutoka kwa Stan Wawrinka raia wa nchini Uswis.

Murray hakuonekana kuwa sawa katika hatua hiyo na baadae alilalamika kusumbuliwa na tatizo la nyonga. Hata hivyo tatizo lilikuwa la muda mrefu nyuma lakini lilipatiwa ufumbuzi, ila katika mchezo huo hali ikaanza tena.

Juni 27, 2017

Baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwenye michuano ya Queen’s dhidi ya Jordan Thompson, hakutaka kuweka wazi kwa mashabiki wake kwa nini alipoteza mchezo huo, kumbe bado alikuwa na tatizo la nyonga.

Lakini aliamua kufunguka baada ya jina lake kuachwa kwenye mashindano ya Hurlingham Club, hivyo alisema bado anasumbuliwa na nyonga.

Julai 2, 2017

Jina lake liliachwa tena kwenye michuano ya pili ya Hurlingham Club, hivyo aliweka wazi kuwa, ana wasiwasi ya kukosa michuano ya Wimbledon kutokana na maumivu anayoyapata.

Julai 12, 2017

Alishindwa kufanya vizuri kwenye Wimbledon na kushindwa kutetea taji lake, hivyo alitolewa katika hatua ya robo fainali dhidi ya Sam Querrey.

Agosti 26, 2017

Baada ya kutolewa mara mbili na kupoteza nafasi ya kwanza kwa ubora duniani na kumuachia nafasi hiyo Rafael Nadal, Murray alikwenda nchini Marekani kwa ajili ya kushiriki US Open, lakini siku mbili baadae akatangaza kuwa anasumbuliwa na nyonga hivyo hatoweza kufanya vizuri.

 Septemba 6, 2017

Murray alitangaza kurudi nyumbani kwa ajili ya kwenda kukutana na washauri wa tatizo la nyonga na aliweka wazi kuwa, anaweza kuwa nje ya uwanja kwa mwaka mzima lakini anaogopa kufanyiwa upasuaji.

Januari 8, 2018

Murray alitangaza kuwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji katika mji wa Melbourne huko Australia na kudai kuwa, baada ya hapo atakuwa fiti.

Juni 19, 2018

Baada ya kuwa nje ya uwanja kwa siku 342, Murray alirudi viwanjani kwenye michuano ya Fever-Tree Championships dhidi ya Nick Kyrgios, lakini hakuweza kufanya vizuri.

Desemba 27, 2018

Baada ya kupoteza michezo mbalimbali tangu afanyiwe upasuaji, Murray alikuja kuweka wazi kuwa, anapatwa na maumivu huku akiwa anajiandaa kucheza michuano ya Brisbane International pia ikiwa ni sehemu ya kujiandaa na Australian Open.

January 10, 2019  

Alhamisi ya Januari 10, aliondoka kwenye ukumbi wa mikutano wa Australian Open huku akiwa analia akidai kwamba michuano hiyo ya Australia mjini Melbourne itakuwa ya mwisho kutokana na kusumbuliwa na maumivu makali ya mara kwa mara katika nyonga zake.

Anatangaza kustaafu huku akiwa na umri wa miaka 31 na kuwaacha wapinzani wake kama vile Roger Federer mwenye miaka 37 akiendelea kushindana.

Kulia kwake kwenye ukimbi wa mikutano kunaweza kukawa na maana nyingi, moja ikiwa ni kustaafu kabla ya muda ambao aliupanga kutokana na umri, anastaafu huku bado akiwa anaupenda mchezo huo pamoja na mengine mengi, lakini kila kitu kina mwanzo na mwisho, tatizo la nyonga linahitimisha safari Andy Murray kwenye mchezo wa tenisi.

@@@@@@@@@@

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles