Majambazi yakibipu lazima yapigiwe  

0
910

HAIWEZEKANI, haiwezekani na haitawezekana kamwe wahalifu wenye mawazo yaliyochakaa kupokonya furaha ya Watanzania  katika taifa huru lililobeba sifa kemkemu duniani kote kuwa ni kisiwa cha amani.

Tukio lililotokea Ijumaa ya Septemba 2 mwaka huu, Lushoto mkoani Tanga, kwamba watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wapatao 15 wakiwa na silaha wamevamia Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa na kuchoma mabweni kwa lengo la kuangamiza wanafunzi na kisha kumuua mlinzi halafu kutokomea kusikojulikana, linatia ganzi.

La kujiuliza, inawezekana vipi mwanadamu anayejua maumivu ya mwili kwamba hata ukichomwa na mwiba huwa ni shughuli pevu anataka kuwateketeza kwa moto binadamu wenzake wasio na hatia?

Nini lengo kuu la wahalifu hawa kufika chuoni na kuanza kujadiliana mbinu watakayotumia ili kuutoa uhai wa wanafunzi ambao kimsingi walikuwa wanasoma kwa ajili ya kulisaidia taifa letu?

Mwendelezo wa mauaji ya kinyama unatia kisirani kwa wananchi wenye moyo wa upendo na Huruma, maana ni hivi majuzi tumeshuhudia Polisi wetu wanne wakiuawa baada ya majambazi kuvamia tawi la Benki ya CRDB lililopo Mbanda, wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam.

Je, nani hakumbuki tukio la Mei 19 mwaka huu, ambapo kundi la watu wanaokadiriwa 15 walivamia Msikiti wa Masjidi Rahman ulioko Ibanda Relini Mtaa wa Utemini Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana, Mwanza na kuwaua watu watatu kwa kuwakata kwa mapanga na kujeruhi baadhi ya waumini waliokuwa wakiswali kwenye msikiti huo?

Haya ni matukio machache kati ya mengi ambayo yameendelea kufanyika katika nchi yetu kwani tumeshuhudia magari yakitekwa na majambazi hasa katika mikoa iliyoko mipakani, benki zimekuwa zikitekwa kwa lengo la kupora fedha bila kusahau wafanyabiashara wanaoendesha miamala ya fedha na vitendo vya ubakaji.

Hata hivyo, pamoja na mbwembwe nyingi za wahalifu hawa ambao wanafikiri wao hawatakufa, bado vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko macho masaa 24 ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kuonja asali ya uhuru wao, jambo la msingi ni kuvipa ushirikiano.

Ushirikiano ninaouzungumzia si wa kubeba silaha au kujichukulia sheria mkononi, bali ni ule wa kutoa taarifa za uhalifu kwa haraka iwezekanavyo katika eneo husika na kwa wakati sahihi.

Ni ukweli usiopingika kwamba pamoja na kuwepo uwezekano wa wahalifu wasiojulikana kutoka maeneo ya mbali hususan nje ya nchi,  lakini asilimia kubwa ya wahalifu huwa wanajulikana kwa wakazi wa eneo husika kwani mara nyingi huwa ni ndugu, jamaa na marafiki zetu.

Pia inasemekana Watanzania ukarimu wetu ndio unaotuponza maana tuko wepesi kuwafurahia, kuwafadhili na kuwaambia siri hata watu ambao hatujui wametoka wapi na wanafanya nini.

Toa taarifa Jeshi la Polisi endapo kuna mtu au watu mnaowatilia mashaka katika mienendo yao hata kama ni maarufu, tajiri, viongozi/wanasiasa.Wananchi mkiwa vijiweni, sokoni, safarini, mitaani, makanisani na misikitini pakijitokeza mgeni mkamtilia shaka toa taarifa mapema.

Miongoni mwa majukumu makubwa ya Serikali pamoja na vyombo vyake vya ulinzi na usalama ni kuhakikisha watu wake wanakuwa salama, lakini ikumbukwe kuwa vyombo hivi havitumii ramli au nguvu ya miujiza kubaini uhalifu, bali huhitaji ushirikiano wako.

Ni ujinga kumfuga chui wakati ukijua siku moja atakurarua wewe, familia yako na mifugo yako na ni upumbavu kumlea chatu wakati ukielewa ipo siku atakumeza mzima.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here