23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

MAJALIWA ABAINI MIKUTANO YA KATA HAIFANYIKI

Na Mwandishi Wetu – Dodoma

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema amebaini kuwa kero nyingi za wananchi hazitatuliwi na viongozi wa ngazi ya chini kwa sababu mikutano ya vijiji, kata na mitaa imekuwa haifanyiki kama inavyotakiwa kisheria.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa bungeni juzi wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa sita wa Bunge la 11.

 “Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kumtumikia kila Mtanzania popote pale alipo. Lakini nimebaini baadhi ya kero za wananchi ambazo zingeweza kutatuliwa katika ngazi za wilaya, zinaletwa kwenye ofisi za viongozi wa kitaifa, au zinasubiri ziara za viongozi hao.

“Nawasihi viongozi wa mikoa na halmashauri tembeleeni vijijini na mtatue kero za wananchi huko vijijini, pia  hakikisheni mikutano ya vijiji iliyowekwa kwa mujibu wa sheria inafanyika na maazimio yake yanafika katika vikao halali vya uamuzi. Wabunge, ninyi ni sehemu ya halmashauri zenu, nawasihi toeni msukumo unaostahili,” alisema.

Pia alisema suala la kutotatua kero za wananchi katika ngazi ya Serikali za Mitaa ni kinyume na dhamira ya Serikali ya kuwatumikia wananchi wote bila ubaguzi, ambalo pia ni kinyume na msimamo wa Ibara ya 146 (1) ya Katiba ya Tanzania.

Akinukuu ibara hiyo alisema: “Madhumuni ya kuwapo Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi. Na vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika mpango wa shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika Serikali zao na nchi kwa ujumla.”

Akisisitiza suala hilo, alisema Sheria ya Serikali za Mitaa inaelekeza kuitishwa kwa mikutano mikuu ya vijiji kila baada ya miezi mitatu, pia inatoa fursa ya kuitishwa kwa mikutano ya dharura endapo ipo haja ya kufanya hivyo.

 “Kutokana na msimamo huo wa kisheria na kutokana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kutatua kero za wananchi, suala la utatuzi wa kero za wananchi halitakiwi kuendelea kusubiri ziara za viongozi, badala yake, kero hizo zitatuliwe katika ngazi zinazohusika na zitatuliwe kwa wakati,” alisisitiza.

Alisema watendaji wa kata, vijiji na mitaa hawana budi kuitisha mikutano ya kisheria ya vijiji, kata na mitaa na kusoma taarifa za mapato na matumizi ya miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Aliwataka viongozi na watendaji katika ngazi ya mkoa, wilaya na halmashauri wajenge utamaduni wa kuwatembelea wananchi vijijini na kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili, ikiwa ni pamoja na kuzitafutia ufumbuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles