27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

KIBAMBA: NCHI HAINYOSHWI KWA KAMBA WALA PIMAMAJI

Na ARODIA PETER -DAR ES SALAAM

JUKWAA la Katiba Tanzania (Jukata), limemwandikia barua Rais Dk. John Magufuli ya kuomba kukutana naye ili wampe ushauri wa mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba, alisema wanakusudia kumweleza na kumshauri Magufuli umuhimu wa mahitaji ya kupatikana kwa Katiba mpya kuliko wakati mwingine wowote ili imsaidie katika kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Pia Jukata inafanya maandalizi ya kuratibu mkutano mkuu wa kitaifa ikiwa ni njia mojawapo itakayotumika kukamilisha mchakato wa Katiba mpya,” alisema.

Kibamba alisema ni zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu Magufuli aingie madarakani, lakini hakuna taarifa rasmi ya Serikali kuhusu dira na mwelekeo wa mchakato wa Katiba mpya licha awali kusitishwa ili kupisha shughuli za uchaguzi.

Alisema kwa kipindi hiki ambacho Serikali ipo katika mchakato wa kuandaa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/2018, ni lazima suala la Katiba lipewe nafasi kwa sababu miaka miwili ijayo nchi itakuwa inajiandaa kuingia katika uchaguzi, ukiwamo ule wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2020 na hakuna muda mwingine wa kumalizia mchakato huo ulioachwa na Serikali ya Awamu ya Nne.

Pia alisema wanamwomba Magufuli avunje ukimya kwa kuwaeleza Watanzania mwelekeo wa kupata Katiba mpya kabla robo ya kwanza ya mwaka huu haijaisha.

Alisema wao bado wanaamini tamko la Magufuli kupitia hotuba yake alipozindua Bunge mwaka juzi, kwamba anafahamu kuna kiporo cha Katiba mpya kilichoachwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

“Kwa maneno yake, ni wazi rais aliahidi kuhakikisha Tanzania inapata Katiba mpya katika kipindi chake cha uongozi, hii itamsaidia katika juhudi zake za kutatua changamoto zinazoikabili nchi.

 “Nia yetu ni njema kwamba rais ndiye pekee atakayeondoa mkwamo huu wa Katiba, hivyo tunaamni tukikutana naye tutaweza kujadiliana naye na tutamshauri umuhimu wa mchakato huo na hofu iliyopo miongoni mwa wananchi, huku kila mtu akiishi kwa kubashiri na kujiuliza maswali na wengine wakikata tamaa.

“Unaposema unanyoosha nchi sawa. Lakini hatuwezi kunyoosha nchi kwa kamba au kwa pima maji, nchi inanyooshwa na Katiba. Inawezekana kwamba ni suala la bahati mbaya washauri wa rais kuhusu Katiba na sheria hawajafanya kazi yao sawasawa kuhusu hili,” alisema Kibamba.

Kuhusu mkutano mkuu wa kitaifa, alisema utajumuisha asasi mbalimbali za kiraia, Serikali na wasomi waliobobea katika michakato ya kidemokrasia kutoka nje na ndani na watafanya uchambuzi na kushauri mwelekeo mpya kutoka hapa tulipo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles