25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

MAGWIJI WA SIASA WAMZIKA KINGUNGE

NORA DAMIAN Na LEONARD MANG’OA-DAR ES SALAAM


MAGWIJI wa siasa wamejitokeza kumzika mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru, huku wakimsifu kuwa alikuwa mtu mashuhuri.

Kingunge aliyefariki dunia Februari 2, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akitibiwa, baada ya kushambuliwa na mbwa wake Desemba 22, mwaka jana, alizikwa jana katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya viongozi walimwelezea Kingunge kama mtu muhimu nchini, ambaye hajapata kutokea.

Akitoa salamu za Serikali, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, alisema Kingunge ni miongoni mwa watu waliotoa mchango mkubwa uliosababisha nchi kupata heshima.

“Kingunge ameacha historia kubwa katika nyaraka mbalimbali za Serikali, ni miongoni mwa watu waliotoa mchango mkubwa nchini hadi tukapata heshima kubwa.

“Waliopewa dhamana katika nafasi mbalimbali tujifunze kuweka mbele uzalendo ili kumuenzi Kingunge,” alisema Jafo.

 

BARAZA LA VYAMA

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda, alisema Kingunge alikuwa shujaa wa vitendo vilivyo sanifu na aliyejenga mwelekeo hai wa siasa za Tanzania na ukombozi wa Bara la Afrika.

“Ametuachia ufadhili wa maono na uzalendo, alikuwa shujaa wa kuishi, na imani zake za uzalendo hazikubinuliwa na imani yoyote ile,” alisema Shibuda.

 

WASIRA

Aliyekuwa waziri katika Serikali za awamu nne, Stephen Wasira, alisema Kingunge alikuwa mjenzi wa hoja, aliyeamini hoja zinajibiwa kwa hoja.

“Nilipokuwa Waziri wa Serikali za Mitaa mwaka 1987, nilibahatika kufanya kazi na Kingunge nikiwa chini yake, wakati huo alikuwa na ofisi mbili, Dar es Salaam na Dodoma.

“Aliamini katika nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu, hivyo pale ulikuwa humwelewi alijitahidi kujenga hoja.

“Ni mwanaharakati, lakini ni mshiriki mkubwa katika ujenzi wa Tanzania, tunasikitika kumkosa, lakini hatuna cha kufanya, tunamshukuru Mungu kwa yote,” alisema Wasira.

 

MEMBE

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema ushindi wote ambao CCM imekuwa ikiupata katika chaguzi mbalimbali, kwa kiasi kikubwa ulichangiwa na mwanasiasa huyo.

“Ametuachia vitabu vingi sana, kila ukiangalia ilani za uchaguzi, ilani za chama, miongozo ya CCM, kwa sababu alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, karibu miaka yote anatoa ushauri.

“Yeye ndiye alikuwa anaandika na kuasisi ilani za CCM na ushindi wote uliokuwa unapatikana, alijikita katika masuala ya siasa, hivyo kwa sisi watu wa Mkoa wa Lindi, tumepoteza lulu ambayo ilikuwa inatoa ushauri kwa vijana wote, hasa walioingia katika medani ya siasa. Yeye ndiye alikuwa kungwi wetu na hakujali anamshauri nani,” alisema Membe.

Alisema ili kumuenzi, ni vema kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kutokuoneana, kuzushiana kwa sababu Kingunge alikuwa mkweli na alitekeleza kile alichokiamini.

“Itatuchukua muda kupata shoka la aina hii, ambalo linaacha kila kitu kwa ajili ya kulitumikia taifa ndani ya chama na ndani ya Serikali.

“Alichotuachia katika miaka 41 ya CCM, ni kujenga demokrasia ndani ya Serikali na ndani ya chama, ukitaka kwenda kinyume na mzee Kingunge, kataa suala la demokrasia, hawezi kuwa rafiki yako,” alisema.

 

MANGULA

Makamu Mwenyekiti wa CCM – Bara, Philip Mangula, alisema Kinguge aliamini katika nguvu ya hoja na si kwa kulazimisha.

“Kingunge alishawishi, hivyo viongozi wote tuige mfano huu wa kushawishi badala ya kulazimisha,” alisema Mangula.

 

NAPE

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), alisema Kingunge alikuwa na msimamo, uwezo wa kuthubutu na uzalendo, hivyo ni vema wanasiasa vijana wakaiga mfano huo.

“Jambo kubwa la kujifunza kwa Kingunge ni kuwa na msimamo na kutoogopa kutofautiana na wenzako, hata kama ni wakubwa namna gani, hasa pale ambapo wanafanya jambo ambalo huliamini,” alisema Nape.

 

MAALIM SEIF

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, alisema: “Ni vizuri kuyaenzi yale aliyoyasimamia mzee wetu, alikuwa anachukia uonevu dhidi ya mtu na mtu.”

 

MBOWE

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alisema kwa muda mfupi waliofanya naye kazi, waligundua kuwa alikuwa kiongozi mwenye ushauri mwema, mwenye kupenda kujenga mshikamano.

“Ni kiongozi ambaye kile anachokiamini alikuwa akikipigania bila kujali atapoteza nini upande wa pili, aliheshimu sana muda, kama mlikuwa na ahadi mkutane saa 9, atafika muda huo, ni kiongozi wa tofauti sana.

“Tunaomba viongozi wa vyama vyote tuige kwa viongozi kama hawa, ambao ni nadra sana katika taifa kuwa nao, hawana chuki, hawana visasi kwa watu, wanapenda kusikiliza mawazo ya wadogo, wakubwa, lakini wana misimamo ya kuleta umoja na mshikamano na si kulitawanya taifa na kutengeneza madaraja ya viongozi,” alisema Mbowe.

 

SOPHIA SIMBA

Mwenyekiti wa zamani wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Sophia Simba, alisema itachukua muda kumpata mwanasiasa kama Kingunge ambaye hakuwa mnafiki.

“Ni gwiji la siasa, alijitambua na huwa haropoki, alikuwa akitumia kichwa chake, ameondoka na yale ambayo itatuchukua muda kumpata mwanasiasa kama yeye,” alisema.

 

JENERALI ULIMWENGU

Mwandishi wa habari mkongwe, Jenerali Ulimwengu, alisema Kingunge alikuwa na uwezo mkubwa wa kuchambua masuala na kuyaeleza kwa lugha fasaha inayoeleweka na kila mtu.

“Alikuwa na fikra pevu, alisoma na akajifunza kuwa mchambuzi wa masuala ya kifalsafa, kisiasa na uongozi wa jamii.

“Alikuwa haogopi kutoa msimamo wake kama unawafurahisha ama hauwafurahishi wakubwa, alieleza misimamo yake hata kama Mwalimu Nyerere hakuifurahia, na mwaka 1978 aliwahi kufukuzwa katika jengo la Karimjee akiwa yuko ndani ya Serikali. Tumuenzi kwa kuwa wakweli, kupunguza unafiki na woga,” alisema Ulimwengu.

 

LEMBELI

Aliyekuwa Mbunge wa Kahama Vijijini, James Lembeli, alisema ni vigumu kumwelezea Kingunge kwa sababu aliyaishi maneno yake.

“Vitendo vyake viliendana na maneno yake, sidhani kama kuna kiongozi mwingine ukiacha Mwalimu Julius Nyerere. Mwalimu alikufa masikini na huyu mzee nadhani amekufa masikini.

“Hakuwa na visasi wala kinyongo, hata kwa wale waliomtukana, waliombeza na ndiyo maana amezikwa na umati mkubwa wa watu.

“Watu wa vyama vyote wamekuja, viongozi tuliobaki tutumie historia kuturejesha kwenye mstari,” alisema Lembeli.

 

VIONGOZI WENGINE

Mazishi hayo, pia yalihudhuriwa na Rais Dk. John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, marais wastaafu, Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi.

Wengine, ni Mama Maria Nyerere, Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohamed Gharib Bilal, mawaziri wakuu wa zamani, Joseph Warioba, Dk. Salim Ahmed Salim, Edward Lowassa, Jaji Mkuu mstaafu, Othman Chande, Jaji mstaafu, Mark Bomani na Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma.

Pia walikuwapo Balozi Paul Rupia, Balozi Job Lusinde, Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa, mwanasiasa mkongwe, Dk. Crisant Mzindakaya, Profesa Issa Shivji, Profesa Mwesiga Baregu na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku.

Awali akihubiri katika ibada ya maziko, Katekista George Wilbard wa Parokia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema ili kumuenzi mwanasiasa huyo, ni vema kuishi katika yale aliyoyaamini.

“Ikiwa tunaamini kwamba Yesu alikufa, vivyo hivyo wao waliolala katika Yesu Mungu atawaleta pamoja nao. Maneno haya yadhihirike kwetu leo (jana), tunapomuaga Kingunge, tuna huzuni, tumempoteza na hatutamuona tena.

“Tukitaka kumuenzi ni kuishi yale aliyoyaishi na kuyafanya, kwa kufanya hivyo tutakuwa tunamwombea,” alisema Wilbard.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Vedasto Ngombale (CUF), alisema wamepata pengo kubwa ambalo halitazibika.

 

WASIFU WA KINGUNGE

Msemaji wa familia, Balozi Ali Mchumo, alisema Kingunge alizaliwa Mei 30,1932  katika Kijiji cha  Kipatimo, Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, lakini alikulia Dar es Salaam.

Alipata elimu ya msingi Shule ya Msingi Mchikichini, kisha alijiunga na Shule ya Sekondari African Special na baadae Shule ya Wavulana ya Tabora.

Alisema licha ya Kingunge kuwa na ufaulu ambao ungemwezesha kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda, alikataa kwenda huko na kutaka kwenda kusomea sheria nchini India.

“Wakati akisubiri kwenda huko, aliajiriwa na Idara ya Public Waste (kwa sasa Wizara ya Ujenzi) kama karani, mwaka 1954 Chama cha TANU kilizaliwa na wiki moja baadae alijiunga na chama hicho.

“Ili aelekeze nguvu zake zote katika kupigania uhuru, aliamua kujiuzulu nafasi yake ya ukarani mwaka 1956 na kutumika kama Katibu wa TANU,” alisema Balozi Mchumo.

Historia inaonyesha wakati nchi za Afrika zilipokuwa zikipigania uhuru, Kingunge alishiriki  harakati hizo akiwa mmoja wa vijana wa TANU walioshinikiza kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika.

Katika maisha yake, tangu ujana wake amelitumikia taifa hadi ngazi za juu kabisa.

Alishika nafasi mbalimbali nchini zikiwamo mkuu wa mkoa, mbunge, waziri na mshauri wa rais katika masuala ya siasa kwa nyakati tofauti.

Alijitoa CCM Oktoba, 2015 baada ya kutofurahishwa na utaratibu uliotumika kumteua mgombea urais wa CCM mjini Dodoma Julai mwaka huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,226FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles