29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Magufuli gumzo mitandaoni Kenya.

MAGUFULI+PHOTO+KochiNAIROBI, KENYA

KATIKA siku chache zilizopita, Rais   Dk. John  Magufuli amekuwa akitamba kwenye mitandao ya jamii nchini Kenya.

Habari zinasema  wananchi wengi wazalendo wameonekana kuvutiwa na uchapakazi wake ndani ya wiki kadhaa tangu aliposhika madaraka.

Dk. Magufuli ameonyesha kutekeleza  kaulimbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ ambayo sasa  inafananishwa na ile ya ‘Kusema na Kutenda’ ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Kauli hiyo ya Kenyatta,  Wakenya wameibadilisha kuwa ‘Kusema na Kutema’ kutokana na kile wanachosema kuendelea kwa maovu katika serikali yake.

Kwa sasa nchini Kenya gumzo kubwa mitaani ni zimwi la ufisadi ambalo limegeuka kuwa wimbo mitaani.

Kwa mujibu wa baadhi ya vyombo vya habari vya Kenya, uchapakazi wa Dk. Magufuli  umetuma ujumbe mzito kwa Kenya ambayo inakabiliwa na visa vingi vya ufisadi katika Serikali ya Rais Kenyatta na naibu wake, William Ruto.

Katika kipindi cha mwezi mmoja tangu alipotwaa madaraka, Dk. Magufuli amefanya  mabadiliko makubwa katika uongozi wa serikali aliyoikuta.

Dk.  Magufuli amekwisha kupiga marufuku safari za nje za mawaziri na viongozi wengine waandamizi serikalini na hata katika mashirika ya umma, akitaka mabalozi wa Tanzania katika  nchi husika kuiwakilisha serikali yake huko.

Kwa hatua hiyo Dk. Magufuli amefanikiwa kupunguza matumizi ya fedha za umma kwa   safari na fedha hizo kuelekezwa kufanya mambo mengine ya kuisaidia jamii.

Rais huyo wa awamu ya tano pia alipunguza bajeti ya awali ya Sh milioni 250   iliyokuwa imetengewa sherehe za kupongezana  wabunge walioshinda uchaguzi, hadi kuwa  Sh milioni 15.

Fedha zilizobakia zilitumwa kuboresha mahitaji ya Hospitali Kuu ya Taifa ya Muhimbili kwa kununulia zaidi ya vitanda 300.

Hiyo ilikuwa ni baada ya Rais huyo kufanya ziara ya kushtukiza hospitalini humo na kuwakuta wagonjwa wamelala  chini kutokana na ukosefu wa vitanda.

Vilevile aliifuta bodi ya wakurugenzi wa hospitali hiyo kwa utendakazi duni akiwamo aliyekuwa Daktari Mkuu Dk. Hussein Kidanto ambaye alirejeshwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Siku chache zilizopita, Dk. Magufuli alipunguza ujumbe wa watu 50 waliotakiwa kusafiri nje ya nchi kuiwakilisha Tanzania kwenye mkutano wa Jumuiya ya Madola   hadi kufikia watu wanne.

Hatua hiyo iliokoa Sh milioni 700   ambazo zingetumiwa na wajumbe hao kugharamia safari hiyo.

Juzi, Dk. Magufuli alitangaza kufuta sherehe za mwaka huu za maadhimisho ya siku ya Uhuru  Desemba 9   na kutaka fedha zake zitumike kwa mambo mengine muhimu.

Haya yakiwa ni baadhi tu ya vitu alivyovifanya, Wakenya wamepagawishwa naye na kusababisha  kuwa gumzo mitandaoni na kuonekana ‘Top in Town’:

Miongoni mwa yanayojadiliwa mitandaoni ni

Fifi: Uhuru Kenyatta anahitaji kujifunza mawili matatu kutoka kwa mwenzake wa Tanzania, Magufuli.

Shadie: Yaani aliyofanya Magufuli ofisini chini ya mwezi mmoja tangu aingie madarakani, yanazidi aliyofanya Uhuru kwa   miaka miwili na nusu tangu awe ofisini.

MafisiPope: Wakati Magufuli akiwa kwenye hali ya kuchapa kazi kwa vitendo wakati ndiyo siku yake ya pili ofisini, kwa Uhuru imepita miaka mitatu lakini bado yupo ‘bizi’ akiunda kamati akitaka zimweleze cha kufanya.

Collins Fabien: Rais Uhuru amekuwa akipiga domo tangu 2013 wakati Rais Magufuli amekuwa akichapa kazi kwa wiki tatu sasa.

Wakati Watanzania wakiamka kuyakuta makubwa aliyoyafanya Magufuli, Wakenya tunaamka kuyakuta yale aliyoahidi Uhuru.

Haya   ni baadhi tu ya maoni ya Wakenya katika kipindi hiki ambacho serikali ya Jubilee ya Rais Uhuru Kenyatta inakumbwa na kashfa ufisadi za kila aina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles