25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI ATOA SABABU TANO ZA KUMUENZI NYERERE

 

Na Andrew Msechu

RAIS Dk. John Magufuli ametaja sababu tano za kumfanya amuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, huku akitaka pia wake za viongozi kujifunza kwa mama Maria Nyerere, ambaye amedai amekuwa mfano wa kuigwa kwa kutojikweza.

Akizungumza na wananchi wa Butiama, Rais Magufuli alisema mji huo una historia ya pekee kwa kuwa Nyerere alizaliwa hapo na kukulia hapo, kisha kusomea hapo kabla hajaenda mikoa mingine na hata baada ya kufariki dunia alizikwa hapo.

 

SABABU ZA KUMUENZI NYERERE

Rais Magufuli alisema Nyerere anastahili sifa kwa kuwa hakuwa mtu wa kujikweza na aliyependa kusuluhisha migogoro ya ndani na nje.

Alisema Nyerere anastahili kuenziwa kwa sababu mbali na kuleta uhuru wa nchi, alisaidia kwa kiasi kikubwa kuasisi na kusababisha muungamo wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania ambayo sasa inaheshimika duniani hadi leo.

“Lakini zaidi Mwalimu Nyerere alishiriki kusaidia kupatikana uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika ambazo leo zinajivunia kazi yake aliyoifanya. Huyu ni shujaa aliyewatumikia Watanzania na hatimaye akaamua kupumzika Butiama.

“Watu wa Butiama wanaweza kuliona hilo ni jepesi na inawezekana wengine wakabeza, lakini wana bahati kuzaliwa hapa na wakumbuke kwamba historia ya kweli ya taifa la Tanzania ndipo ilipoanzia,” alisema.

Rais Magufuli alisema kutokana na heshima ya Baba wa Taifa, atahakikisha ndoto yake (Nyerere) ya ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Stigler’s Gorge iliyokuwepo tangu mwaka 1975, ataitimiza na mradi huo utakapokamilika utaitwa Nyerere Gorge lengo likiwa ni kumuenzi mwasisi huyo wa taifa.

 

AMZUNGUMZIA MAMA MARIA

Akimzungumzia mama Maria Nyerere, alisema mjane huyo wa Mwalimu ni mama tofauti ambaye tabia yake haijabadilika tangu alipokuwa na Nyerere hadi leo, tofauti na baadhi ya wake wa viongozi wengine ambao alisema wakati mwingine hata kuwasogelea unaogopa.

Alisema ni matumaini yake kwamba akina mama wengi watajifunza tabia yake, kwa kuwa kuna wengine hata akiolewa tu na mwendesha daladala anabadilika, mwingine akipata mtu mwenye duka tu hasalimu majirani, lakini mama Nyerere amekuwa mama wa taifa.

“Wake wa viongozi wengi wanatakiwa wajifunze kwako. Nimeona wake wa viongozi wengi, wengine hata huwezi kuwagusa ila wewe uko hivyo hivyo, kama ulivyoletwa na Mungu duniani na ni kwa sababu ya malezi mazuri, ndiyo maana ninajivunia kuzungumza kwa heshima kubwa nikiwa hapa Butiama,” alisema.

Awali, Rais Magufuli alieleza kushangazwa na mji huo wa Butiama kwamba pamoja na sifa zote za kuwa kitovu cha historia ya taifa, bado hakuna maji ya uhakika.

Alisema kwa kujali na kuheshimu historia ya Butiama, atahakikisha kunakuwa na maji ya uhakika na barabara za uhakika.

Alikumbushia agizo lake la kuhakikisha Shule ya Msingi Mwisenge ambayo alisoma Mwalimu Nyerere inakarabatiwa na kujengewa uzio.

Alimwagiza Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo kuhakikisha anafanya kila liwezekanalo, hata kama ikiwa ni kuhamisha fedha kutoka maeneo mengine ili shule hiyo ikarabatiwe.

Alimweleza mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhakikisha anamaliza matumizi ya Sh milioni 400 kabla ya kuomba nyingine.

 

MIGOGORO YA ARDHI

Akizungumzia migogoro ya ardhi katika eneo hilo, Rais Magufuli alieleza kusikitishwa nayo akisema Mwalimu Nyerere alikuwa mtu wa kusuluhisha matatizo kama hayo na kwamba akifufuka leo atawashangaa watu wa Mara.

Alisema katika Wilaya za Butiama, Bunda na Serengeti kuna vijiji vinagombania mipaka wakati viko katika mkoa mmoja wa Mara, pia ipo migogoro baina ya vijiji vilivyo katika wilaya moja na migogoro ya mtu na mtu.

“Mambo mengine yanashangaza, kuna migogoro baina ya vijiji vilivyo katika wilaya na mkoa mmoja, kwanini wananchi wenyewe wasizuie kutokea kwa migogoro hii, mbona Baba wa Taifa alizuia migogoro mingi na hadi sasa taifa linaheshimika kwa kazi yake ya kusuluhisha na kumaliza migogoro ndani na nje?” alihoji.

Aliwaagiza viongozi wakiwamo wakuu wa wilaya wakae na maofisa ardhi na kuhakikisha migogoro hiyo inamalizika kabla haijafika kwake na kwamba iwapo kiongozi ataendelea kuwapo katika eneo lenye migogoro maana yake ameshindwa kutawala.

Alisema kwa kuwa wamepewa vyombo vyote vya ulinzi na usalama, sheria ya ardhi na madaraka kwa mujibu wa katiba, hivyo wasikubali kukaa mahali ambako migogoro inaedelea kuwapo na kuwafanya watu washindwe kufanya shughuli zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles