29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli ampigia debe Mrema

MTZ IJUMAA new1.indd*Asema akishindwa atamtafutia kazi nyingine

 

NA BAKARI KIMWANGA, VUNJO

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema kama wananchi wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro hawataki kukichagua chama hicho katika nafasi ya ubunge, ni bora wamchague mgombea wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema.

Dk. Magufuli, alitoa kauli hiyo jana, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika mji mdogo wa Himo.

Alisema pamoja na kutaka Mrema achaguliwe, anahitaji zaidi achaguliwe mgombea wa CCM, Innocent Shirima.

Dk. Magufuli alisema Mrema ni mwanasiasa wa kweli na mwenye uchungu kwa wapiga kura wake wakati wote.

Aliwataka wananchi wa Vunjo, wasikubali kumchagua mgombea wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, kwa kile alichodai kuwa ni mtu mvurugaji kila sehemu, ikiwamo ndani ya chama chake.

“Kama mnaona kuichagua CCM ni kosa, mleteni Mrema (Augustine), lakini namtaka Innocent Shirima. Siku zote Mrema alikuwa mkweli na mpambaji bungeni.

“Kama mtaichagua CCM, Mrema nitamtafutia kazi…mzee Mrema sitamwacha kutokana na rekodi yake ya utendaji kazi katika nchi hii, kama wapo ndugu zake wakamweleze.

“Msimlete mwingine ambaye anasema hakuna kilichofanyika hapa Himo. Je, huko nyuma kulikuwa na benki? Mwambieni akaimarishe chama chake cha NCCR-Mageuzi, ameua chama chake na sasa aje kuua jimbo? Hii hapana, kataeni,” alisema Dk. Magufuli.

Akiwa njiani kuelekea wilaya za Mwanga na Same, Dk. Magufuli alilazimika kusimamisha msafara wake na kusalimiana na Mrema ambaye alikuwa amesimama njia panda ya Himo.

Akizungumza na wananchi baada ya kusalimiana na Dk. Magufuli, Mrema alisema anamshukuru mgombea huyo wa urais kwani amemsaidia kujenga barabara nyingi katika Jimbo la Vunjo.

“Jamani rais wetu ni Magufuli, naomba wote tumchague mchapakazi, ametujengea barabara nyingi katika jimbo letu,” alisema Mrema.

Naye Dk. Magufuli, alisema anashangazwa na watu wanaohangaika kufanya kampeni, wakati yeye ndiye rais ajaye kutokana na uamuzi wa Watanzania.

“Nawaambia, Magufuli ndiye rais ajaye, wale wanaohangaika kutaka kupoteza kura zao kwingine wajue hivyo.

“Hamna sababu ya kupoteza kura zenu, mchagueni Magufuli kwa kura nyingi na kutokana na wingi huu wa watu nawaambia sitawaacha…nawahakikisha nitaleta maendeleo ya kweli,” alisema.

Dk. Magufuli, alisema Serikali yake itakuwa ya viwanda ambavyo vitachochea kukuza ajira kwa vijana.

Alisema kama atachaguliwa, atahakikisha anawatumikia Watanzania kwa uadilifu wa hali ya juu pamoja na kusimamia vema rasilimali za nchi.

Awali akiwa wilayani Rombo, Dk. Magufuli aliwataka wananchi wa jimbo hilo kutompa ubunge mgombea wa Chadema, Joseph Selasini, kwa sababu ameshindwa kuondoa kero ya maji.

“Selasini mnampenda, lakini hatoshi ubunge, mwambieni safari hii ‘No water, no Selasini’, haiwezekani Ziwa Chala ambalo lipo hapa Tarakea upande wa Kenya kuna maji, ninyi hamna kitu… mchagueni Samora Kanji wa CCM,” alisema.

Dk. Magufuli alisema yeye ni gari jipya linalopambana na magari manne mikweche.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles