22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Slaa: Magufuli anafaa kuwa rais

Dr-Slaa-4Na Khamis Mkotya, Dar

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa, amempigia debe mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, akisema kuwa anafaa kuwa rais wa awamu ya tano.

Dk. Slaa amedhihirisha hisia zake hizo juzi usiku wakati akihojiwa katika kipindi maalumu kilichoandaliwa na kurushwa na Kituo cha Televisheni cha Star TV.

Dk. Slaa ambaye alizungumzia masuala mbalimbali, alisema anamuunga mkono Dk. Magufuli kwa kuwa ni mgombea pekee aliyeonesha ujasiri na dhamira ya kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi kuliko wagombea wengine.

Mwanasiasa huyo ambaye amestaafu siasa za vyama, alisema Magufuli anafaa kuwa rais, kwani amediriki kutangaza vita dhidi ya walarushwa, wezi na mafisadi bila kujali atanyimwa kura.

“Baada ya kusikiliza na kuhudhuria mikutano mingi ya kampeni, kwanza lazima tujiulize tunataka rais wa aina gani?, mwenye vigezo vya aina gani? Hiyo ndiyo maana halisi ya kampeni.

“Mkutano wa kampeni unamaana kubwa, hatuendi kwenye kampeni kufanya mbwembwe au kucheza muziki, tunakwenda pale kupima sera na kuwapima wagombea.

“Kwangu mimi nahitaji rais mwenye vigezo vya kupambana na rushwa, katika wagombea urais wote wanane sioni mgombea mwenye uwezo wa kupambana na rushwa zaidi ya Magufuli.

“Sisemi kwamba Magufuli ni msafi sana na yeye anazokasoro zake, lakini katika wagombea wote wa urais mwenye vigezo vya kupambana na rushwa  Magufuli anafaa,” alisema.

 

Ajenda ya ufisadi

Dk. Slaa alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepoteza ajenda ya ufisadi ambayo ilikipa umaarufu.

“Katika kampeni za mwaka huu, chama changu Chadema kimeacha ajenda ya rushwa. Hata nyimbo za hamasa za kupinga rushwa na ufisadi hazisikiki tena.

“ACT-Wazalendo ni kama wanairithi Chadema kwenye ajenda ya rushwa. Nampongeza Zitto  (Zitto Kabwe) na chama chake yuko commited (amedhamiria).

“Magufuli anasisitiza kuwa anapiga vita rushwa, sijaona jambo hilo kwa Chadema. Ukiwa mchafu huwezi kukemea rushwa.

“Dk. Magufuli anasema ataanzisha mahakama maalumu za rushwa na ukimtazama anaaminika, sijawahi kusema Magufuli ni msafi, lakini ana nafuu kati ya wagombe wengine.

“Tulimpinga Rais Kikwete mwaka 2010 alipowashika mikono Mramba, Chenge na Lowassa kuwanadi majimboni mwao watuhumiwa wa rushwa. Magufuli haogopi kupoteza kura kwa kukemea ufisadi na kusema atawafunga wala rushwa, Magufuli ni jasiri,” alisema.

Dk. Slaa ambaye ametangaza kustaafu siasa za vyama alitofautiana na viongozi wenzake katika chama chake kuhusiana na kuwapokea wanachama waliotoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao amewaita makapi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles