23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Magufuli amnanga Lissu kwao

Pg 2 mpaka 3*Amwita mtukanaji na mkwamishaji miradi ya maendeleo

*Diana Chilolo amgeuka Lowassa, asema hana washauri

Na Bakari Kimwanga, Ikungi

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, jana aliwasili Jimbo la Singida Mashariki ambalo mwakilishi wake bungeni aliyemaliza muda ni Tundu Lissu (Chadema) na kuwataka wapiga kura wa jimbo hilo kutomchagua tena kwa sababu ana lugha chafu.

Dk. Magufuli, ambaye alifanya mkutano wake wa kwanza Wilaya ya Ikungi mkoani Singida uliohudhuriwa na umati mkubwa, alisema amekwenda kufanya mkutano wa kampeni katika jimbo hilo kwa sababu anataka wapigakura wamchague mgombea ubunge wa CCM aliyemtaja kwa jina la Jonathan Njau, ambaye ni mkweli na ana uwezo wa kuleta maendeleo ya kweli.

Alisema Lissu hapaswi kuchaguliwa tena kwa sababu ameshindwa kuwasaidia wananchi wa jimbo hilo kupata maendeleo ya kweli kwa kushindwa kusimamia miradi mingi ya jimbo hilo kutokana na misimamo yake iliyochangia kuwaumiza wapigakura wake.

“Ninasema wana Ikungi na Watanzania kwa ujumla tunahitaji kujenga nchi kwa kutumia rasilimali zetu ambazo zitamnufaisha kila Mtanzania, ila kwa hapa kwenu mmeteseka kwa sababu ya aina ya mbunge mliyemchagua. Ni bora kukosea jambo lingine au hata kuoa lakini sio kuchagua, kwani haya ndiyo yanawafanya mteseke. Mnachagua mbunge ambaye kazi yake ni kuwatukana mawaziri na hata zinapojadiliwa bajeti wanatoka nje.

“Waziri naye ni binadamu, hana moyo wa chuma wa kuvumilia matusi, je, kwa hali hii anaweza kuleta maendeleo kwenu. Hapana msifanye makosa kwa kuchagua wabunge wa matusi na kutoka nje,” alisema Dk. Magufuli

Dk. Magufuli alijigamba mbele ya wapiga kura hao kuwa yeye ni ‘tingatinga’ la maendeleo na amedhamiria kujenga Tanzania mpya yenye uchumi wa viwanda pamoja na kukuza ajira kwa vijana kupitia sekta hiyo.

Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, alisema anazijua na ana mbinu za kupambana nazo, huku akitolea mfano changamoto zinazowakabili wauguzi na madaktari, ikiwemo ukosefu wa vifaa tiba.

“Kule Chato kuna daktari alilazimika kufanya upasuaji kwa kutumia chemli na alifanikiwa kuokoa maisha ya watu wengi kweli, sasa ni wajibu wa Serikali ya Awamu ya Tano kuyaangalia haya na kuyapatia ufumbuzi wa uhakika,” alisema Dk. Magufuli.

Aidha, Dk. Magufuli alisema anaijua mipango inayofanywa na baadhi ya watu wanaotaka kujigawia maeneo muhimu ya uchumi na aliwaonya kuwa wanapaswa kujiandaa kuondoka wenyewe.

Aliitaja baadhi ya miradi inayolengwa na wale aliowaita mafisadi kuwa ni reli, gesi na umeme.

Diana Chilolo

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Singida, Diana Chilolo, ambaye alipewa fursa ya kuzungumza kwenye mkutano huo, alieleza kushangazwa na uamuzi wa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na vyama vya NCCR- Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na National League for Democracy (NLD) vinavyounda Umoja wa Katiba ya  Wananchi (Ukawa) Edward Lowassa, aliyeukamia urais kama maji.

Chilolo ni mmoja wa makada wa CCM ambao awali walikuwa katika kambi ya Lowassa, lakini katika mkutano wa jana alieleza kumshangaa kwa kuonyesha udhaifu pale alipokihama CCM na kujiunga na Chadema.

“Lowassa amekosa mshauri na kama angekuwa naye asingechukua fomu ya urais, maana ukimwangalia unamuona hayuko sawa, lakini pia amekuwa akitajwa katika kila udhaifu wa ufisadi na Lissu alikuwa ni moja wa watu waliokuwa wakimsema, sijui leo amemsafisha na nini.

“Muogope kiongozi asiyekubali matokeo, mimi nilikuwa mgombea kura zangu hazikutosha, bado nipo imara na ninatafuta kura za CCM kwa rais, wabunge na madiwani na sijayumba,” alisema Chilolo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles