27.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Madiwani watakiwa kutumia vizuri siku zilizobaki kabla Uchaguzi Mkuu

Sheila Katikula – Mwanza

MADIWANI wa Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza wametakiwa kutumia vizuri siku zilizobaki kabla ya Uchaguzi Mkuu kwa kufanya maendeleo katika kata zao ili waweze kuchaguliwa tena na wananchi.

Rai hiyo ilitolewa juzi na Meya wa Manispaa hiyo, Renatus Mulunga, wakati wa kikao cha mapendekezo ya mpango wa bajeti kwa mwaka 2020/21.

Alisema ni vema kutumia siku zilizobaki vizuri kwa kufanya maendeleo katika kata zao ili wananchi waweze kuwachagua tena kwa kishindo.

“Nawaomba mtumie vizuri siku zilizobaki kwa kuleta maendeleo katika kata zenu, kila kiongozi anatambua kuwa mwaka huu tunafanya uchaguzi, hivyo ili kupata nafasi hii ni lazima kujituma kwa wananchi na bajeti hii haijabagua, kila mtu itamfikia kwenye eneo lake,” alisema Mulunga.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Shukrani Kyando, alisema mwaka huu wananchi wameandaa misingi 82 kwa ujenzi wa madarasa.

Alisema wananchi hujenga msingi na mbunge huleta matofali ya kujengea huku halmashauri ikimalizia kwa kupaua na kuezeka madarasa husika.

Alisema mbunge wa Ilemela alileta mifuko ya saruji 1,800 ambayo itasaidia kupatikana kwa tofali zaidi ya 50,000 lengo ni kuhakikisha changamoto ya madarasa inakwisha katika halmashauri hiyo.

“Tunamshukuru mbunge kwa kuleta mifuko ya saruji 1,800 ambayo itasaidia kupatikana kwa matofali mengi, na sisi kama halmashauri tumenunua mashine za kufyatulia ili kwenda na kasi ya elimu bila malipo, wanafunzi waweze kusoma katika mazingira mazuri,” alisema Kyando.

Alisema mwaka jana halmashauri hiyo ilifanikiwa kukamilisha maboma ya madarasa 32 ambapo kati ya hayo Serikali Kuu ilileta fedha za madarasa 10 na mengine walishirikiana na wananchi.

“Mwaka huu kuna maboma yaliyokamilika 33, halmashauri imepeleka Sh milioni 128 kwenye kata zote kwa ajili ya kuezeka na umaliziaji wa madarasa hayo kwa kushirikiana na ofisi za kata ili waweze kusimamia na kukamilisha kwa wakati,” alisema Kyando.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,903FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles