23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Manispaa Tabora yapitisha bajeti Sh bil 52

Allan Vicent-Tabora

HALMASHAURI ya Manispaa ya Tabora imepitisha bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/21 ambapo Sh bilioni 52.7 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Hayo yalibainishwa na Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Joseph Kashushura, katika kikao cha wataalamu, watendaji na wadau mbalimbali wa maendeleo kilichofanyika jana.

Alisema Sh bilioni 4.7 zinatarajiwa kupatikana kutoka vyanzo vyake vya ndani na kutumika kwenye miradi ya maendeleo (Sh bilioni 2), mishahara (Sh milioni 14.3), mapato ya bajeti fungwa (Sh milioni 263) na matumizi mengine (Sh bilioni 2).

Kashushura alisema halmashauri hiyo inatarajia kupokea ruzuku kutoka Serikali Kuu Sh bilioni 48.01 na kati ya hizo Sh bilioni 41 zitatumika kwenye mishahara, Sh bilioni 5 miradi ya maendeleo na Sh bilioni 1 matumizi mengine.

Akifafanua vipaumbele vya bajeti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bosco Ndunguru, alisema wametenga Sh milioni 200 kuanza ujenzi wa shule mbili za kidato cha tano na sita.

Alisema shule zitakazopandishwa hadhi na kuwa na kidato cha tano ni Shule ya Sekondari Nkumba iliyopo Kata ya Uyui na Chang’a iliyopo Kata ya Tumbi nje kidogo ya manispaa hiyo.

Alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kulipa fidia kwa wenye migogoro ya muda mrefu ambapo wametenga Sh milioni 50 kukarabati matundu ya vyoo vya shule za msingi na kununua taulo za watoto wa kike ambazo wametenga Sh milioni 84.

Alisema pia wametenga Sh milioni 200 kuendeleza ujenzi wa jengo la utawala, Sh milioni 70 kununua hekta 140 za uwekezaji.

“Vipaumbele vingine ni kutoa mikopo kwa vikundi ya kina mama, vijana na wenye ulemavu, ambapo tumetenga Sh milioni 445 na kuendesha shughuli za lishe katika manispaa ambapo tutatumia Sh milioni 117,” alisema Ndunguru.

Shughuli nyingine zitakazofanyika ni kuwezesha ulipaji mishahara ya vibarua wa mazingira (Sh milioni 108), utekelezaji miradi mbalimbali katika kata zote 29 za manispaa (Sh milioni 580) na kutekeleza miradi katika ngazi ya wilaya (Sh bilioni 1).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles