24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Takukuru yataifisha nyumba walizojimilikisha watumishi

Benjamin Masese-Mwanza

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza imewapokonya waliokuwa watumishi wa Shirika la Tanesa majengo manne yaliyojengwa na Serikali ya Uholanzi na kuanza mchakato wa kuyakabidhi Serikali ya Tanzania.

Majengo hayo yaliyopo kiwanja namba 32, kitalu ‘W’ eneo la Kapripoint jijini Mwanza, yalikuwa yakitumiwa na shirika hilo lililokuwa linajishughulisha na mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Stenga, alisema majengo hayo yana thamani ya Sh milioni 420.

Alisema mradi huo ulikuwa ukitekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Uholanzi na kwamba baada ya mkataba kuisha mwaka 2012, Serikali ya Uholanzi ilitoa maelekezo ya mgawanyo wa mali zilizokuwa zikitumika katika mradi huo yakiwamo magari na nyumba.

“Serikali ya Uholanzi ilielekeza magari yachukuliwe na wafanyakazi, lakini majengo manne yalipaswa kukabidhiwa Serikali ya Tanzania.

“Baada ya wenye mradi kuondoka, baadhi ya wafanyakazi wa Tanesa walifanya mchakato wa kinyemela na kujimilikisha na kuanza kupangisha watu na fedha zote zilikwenda mifukoni mwao.

“Baada ya taarifa hizi kutufikia, tulianza kuzifanyia kazi na tumejiridhisha nyumba hizo zilikuwa zikimilikiwa kinyemela na mapato yake yalikuwa yakiwanufaisha watu wachache,” alisema Stenga.

Kamanda huyo alisema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote waliohusika, huku wakiendelea na mchakato wa kuzikabidhi nyumba hizo serikalini.

“Mpaka sasa tunafuatilia taratibu za kubadilisha umiliki kutoka kwa waliokuwa watumishi wa Tanesa na kuwa mali ya Serikali ya Tanzania, pia hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa na pengine fedha zote walizojipatia watazirudisha,” alisema Stenga.

Katika hatua nyingine, Stenga alisema Takukuru imefanikiwa kuokoa Sh milioni 30.67 na kudhibiti upotevu wa Sh milioni 74.8 kati ya Oktoba na Desemba mwaka jana.

Alisema Sh milioni 30.67 zilizookolewa katika miradi mbalimbali ya maendeleo zimehifadhiwa katika akaunti maalumu ya Serikali iliyopo Benki Kuu (BoT).

Stenga alisema Sh milioni 74.8 zilizodhibitiwa katika sekta ya kilimo  zimerejeshwa kwa wakulima wa pamba waliodhulumiwa malipo yao katika vyama vya ushirika vya msingi (Amcos) Wilaya za Magu na Sengerema.

Aliwataka wanachama wa vikundi na vyama vyote kuchukua hatua dhidi ya viongozi wao pale inapobainika kukiuka maadili ya utendaji.

Alisema pia ndani ya miezi mitatu wameweza kuchunguza miradi 16 ya maendeleo katika wilaya zote za Mkoa wa Mwanza yenye thamani ya Sh bilioni 21.2 ikiwamo ya ujenzi, elimu, afya, maji na mingine na kwamba iliyo na mapungufu wameelekeza irekebishwe haraka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles