25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Madawati yasifunike madai ya walimu

MadawatiNa Markus Mpangala

MWALIMU Theresia Mushi ni miongoni mwa vijana wenye mtazamo mpana kuhusu suala la elimu hapa nchini tangu akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na sasa kazini, ambapo anasema kuwa ili kufanikisha kuleta mazingira bora ya sekta ya elimu ni pamoja na kuhakikisha walimu wanakuwa sehemu ya upatikanaji wa huduma bora na stahiki kwa shule zote za msingi na sekondari.

Alisema: “Kuleta madawati shuleni ni kukabiliana na wimbi kubwa la wanafunzi, vyumba vipo na madawati yanahitajika, lakini ni muhimu vile vile kuwahusisha walimu kama wadau na waandaaji wa taifa kupitia sekta ya elimu. Kwa hiyo walimu wanatakiwa kukamilishiwa mambo muhimu yanayojenga mazingira bora ya elimu.”

Aliongeza: “Ni lazima vitendea kazi, majengo, madai ya walimu yafanyiwe kazi hiyo ni maana ya kuwahusisha walimu katika kazi hii.

Walimu wana madai mengi makubwa yaliyolimbikizwa, makato mengi, lakini hayatatuliwi kwa haraka kama ilivyo kasi ya upatikanaji wa madawati kote nchini,”

“Tunahimiza wadau kuchangia madawati, lakini Serikali haiambiwi iharakishe kutatua madai ya walimu,” alisema.

Pamoja na mambo mengine mwalimu huyo bado anaamini ipo nafasi kwa Serikali na wadau wa elimu kuhakikisha mambo yanabadilika sasa si kila mara kungojea ahadi ambayo haina maana yoyote.

Serikali inaweza kuondokana na kukabiliwa na madeni ambayo yamekuwa yakizalisha malimbikizo na kuifanya kuwa isiyo na uwezo wa kutatua changamoto za watumishi wake wa sekta ya elimu.

Je, ni kweli kasi ya upatikanaji wa madawati haiwezi kuwa sawa na utatuzi wa madai ya walimu? Je, ni kweli kwamba Serikali imeshindwa kabisa kuyatatua madai ya walimu pamoja na kuboresha sekta ya elimu?

Hayo ni sehemu ya maswali ya kujiuliza na kutafiti. Lakini majibu haraka hayakosekani. Kwanza tunafahamu kuwa mpango wa kutafuta madawati na kuyapata ni kuziba pengo la wingi wa vyumba vya madarasa vilivyojengwa katika mpango wa Shule za Sekondari za Kata.

Pili, mpango wa kusaka madawati ya kutosha unatokana na wimbi la wanafunzi waliojiunga katika shule za sekondari za kata na shule za msingi kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Jambo la tatu ni mpango wa kutoa elimu bure kuanzia ngazi ya shule ya msingi umesababisha wimbi kubwa la wanafunzi huku shule zikiwa na uwezo mdogo kukabiliana na suala hilo.

Matokeo ya mambo hayo yanasababisha changamoto ya uhaba wa madawati ambayo sasa inafanyiwa kazi. Hata hivyo, wakati hilo linatatuliwa bado swali linakuja kama ambavyo Mwalimu Mushi alivyosema, kuwa madawati yanapopatikana ni lazima yaendane na utatuzi wa kero za walimu.

Mathalani, tunakusanya madawati ya kutosha na kuyapeleka shuleni. Tunafika shuleni hakuna vyumba vya kutosha kuweka madawati hayo na kujikuta mengine yakiwekwa nje. Vile vile tunapeleka madawati shuleni lakini tunajikuta mazingira yake si rafiki, majengo mabovu, walimu ni wachache na hawakidhi haja ya wanafunzi.

Tunakutana na mazingira ambayo yanachangia wanafunzi kutopenda elimu huku baadhi ya mikoa kama ya Kanda ya Ziwa wakitangazwa kuacha masomo na kwenda kuolewa ama kupachikwa mimba na mafataki.

Serikali inaweza kujidanganya kwamba ili kukabiliana na changamoto kwenye sekta ya elimu ni kuhakikisha wanafunzi wanaketi mahali pazuri ama wanakuwa na majengo mazuri na yenye ubora wa hali ya juu.

Lakini vyote hivyo haviwezi kukamilisha ubora wa elimu kama walimu hawatakuwa sehemu ya upatikanaji wa ubora huo. Kwa hiyo ili ubora wa elimu ukamilishwe tunarudi palepale kwamba walimu wanatakiwa kulipwa stahiki zao.

Walimu wanatakiwa kupewa haki zao za msingi. Vile vile Serikali inatakiwa kufahamu kuwa wapo walimu ambao wanafundisha shule nzima kutokana na uhaba wa walimu.

Mara ngapi tumesikia kuwa mwalimu mmoja anafundisha madarasa saba ya shule ya msingi? Mara ngapi tumesikia mwalimu mmoja anafundisha masomo tofauti na yale anayomudu kwenye shule za sekondari?

Tunapeleka madawati, lakini hayatakamilisha ubora wa elimu kama walimu wataachwa au kupuuzwa madai yao ambayo ni chachu ya kupata ubora wa elimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles