27.9 C
Dar es Salaam
Monday, February 26, 2024

Contact us: [email protected]

Lembeli: Siondoki Chadema

Lembeli*Asema hana mpango wa kurudi CCM

*Awavutia pumzi wanaomkejeli kila kona

Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam

SIKU moja baada ya Mbunge wa zamani wa Kahama Mjini, James Lembeli kuibuka katika mkutano wa Rais John Magufuli, amesema hana mpango wa kurudi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Lembeli alijiengua   CCM na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika kile alichodai kuchoshwa na vitendo vya rushwa vilivyokithri  ndani ya chama hicho tawala.

Juzi, akiwa katika mkutano   wa Rais Magufuli uliofanyika Kahama, aliitwa na mkuu huyo nchi   aweze kuwasalimia wananchi.

Alisema: “Iwapo Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli atakisafisha chama hicho basi na mimi ninaweza kurudi katika chama hicho kwa lengo la kuwahudumia wananchi”.

Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa kitendo cha mwanasiasa huyo kuibuka katika mkutano huo, tafsiri yake ni kwamba amerejea ndani ya chama chake hicho cha zamani.

Akizungumza jana na mtangazaji wa Blog ya Kijukuu, Lembeli alisema msimamo wake uko pale pale.

Alisisitiza  kwamba hana mpango wa kurejea CCM mpaka Rais Magufuli atakapoweka sawa mazingira ya chama hicho tawala.

“Msimamo wangu niliutoa pale uwanjani na Rais mweyewe akasikia kwamba siwezi kurudi CCM wakati mazingira bado ni yale yale.

“Na nilisema uwanjani pale unapomkaribisha mtu unategemea jibu la ndiyo au hapana… jana (juzi) nilimwambia Rais hapana, siwezi. Watu wa Kahama wananifahamu zaidi ya mtu mwingine yeyote.

“Msimamo wangu wanaufahamu ni wapi niliko wanapafahamu na ndiyo maana nilipokaribishwa kusalimia umati mkubwa karibu wote waliokuwapo pale walishangilia  kwa nguvu moja bila kujali huyu ni nani wala nani…kwa hiyo msimamo wangu uko pale pale,”alisema Lembeli.

Lembeli ambaye aliongoza Jimbo la Kahama kwa miaka 10, alisema kama angekuwa amemweleza Rais Magufuli kuwa amerudi, angetangaza katika mkutano huo.

“Mimi hizi biashara za watu kuandika vitu vya uongo wanaweza wakaendelea nazo kwa sababu kama ningekuwa nimemweleza Rais kuwa nimerudi angetangaza pale pale,”alisema Lembeli.

Akiwa katika mkutano huo juzi, Rais Magufuli alimtaka Lembeli kurejea ndani ya CCM kwa kuwa chama aliko kwa sasa ndiko walipo mafisadi.

“Wana Kahama tambueni kuwa Lembeli ni rafiki yangu wa siku nyingi na kuwapo kwake hapa ninategemea mabadiliko makubwa kutoka kwake na ninakushauri urudi Tanzania kwani ulikokwenda  umepotea.

“Ninakuomba Lembeli urudi kundini mimi ninakujua unavyowapenda wananchi wako wa Kahama.

“Ukirudi sitakukata mkia kwa sababu  huko ulikokwenda umepotea njia, mimi ndiye mwenyekiti ninayewapinga wasaliti ambao asubuhi wapo CCM, jioni wapo upinzani,”alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles