23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

MABADILIKO YAJA ELIMU YA MSINGI

Na Kulwa Karedia


* Yaweza kuwa mwisho wa darasa la sita, masomo yapunguzwa

ndalichakoSERIKALI imefanya mabadiliko makubwa katika mitaala na mfumo wa elimu ya msingi, MTANZANIA imebaini.

Habari za uhakika  kutoka vyanzo vya kuaminika na kuthibitishwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, zinasema mabadiliko hayo ambayo utekelezaji wake unaanza leo, yatagusa aina ya masomo yatakayofundishwa kuanzia darasa la tatu.

Kwa mujibu wa habari hizo, upo uwezekano wa elimu ya msingi ambayo imekuwa ikitolewa kwa miaka saba, ikapunguzwa na kuwa miaka sita kwa wanafunzi walioko  darasa la tatu hivi sasa.

Habari hizo, zinasema masomo yatakayofundishwa kuanzia leo ni Kiswahili, Hisabati, English, Maarifa ya Jamii, Uraia na Maadili, Sayansi na Teknolojia na somo la dini.

Lakini pia kutokana na mabadiliko hayo, Serikali imeongezea masomo mawili ya ziada kwa wanafunzi wa darasa hilo ambayo ni Elimu ya Sanaa na Michezo na Vilabu vya Masomo ya Usajariamali (Shughuli za uzalishaji mali).

“Utaona  idadi ya masomo imepungua kutoka 10 ya awali mpaka 6, haya ni mabadiliko makubwa katika madarasa haya, naamini yataleta mapinduzi kwa wanafunzi wetu.

“Si hicho tu, bali kuna masomo mapya yameingizwa, utaona kuna somo la uraia na maadili na ya shughuli za ujasiriamali..mitaala hii inaonekana itafungua ukurasa mpya wa elimu yetu,”kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho kilisema kuanzia sasa wanafunzi hao watakuwa wanaingia shuleni asubuhi na kuruhusiwa saa 6:20 mchana.

“Mbali ya hilo, tayari kuna walimu shuleni kwetu wamepewa mafunzo ya namna ya kuanza kufundisha mitaala hii mipya, tena wametakiwa kukaa kituo cha kazi miaka miwili bila kuhama,”kilisema chanzo chetu.

 

KAULI YA SERIKALI

Akithibitisha kuwapo mabadiliko hayo, Naibu Katibu Mkuu Wizara Elimu (Msingi), Dk. Leonard Akwilapo  alisema wanafunzi wanaoguswa na mabadiliko hayo ni wale walioanza elimu ya msingi mwaka 2015 na mwaka jana walikuwa darasa pili na darasa la tatu mtaala wao unalenga waishie darasa la sita.

“Kimsingi kuna maandalizi tunatakiwa tuyafanye maandalizi ya kimtaala yamekamilika, tunaangalia maandalizi ya miundombinu ndiyo tunayafanyia kazi hapo ili tutoke na ‘statement’ kamliki.

“Kwa hiyo siwezi kuconfirme (kuthibitisha) kwa sababu tunajalidiliana katika uongozi wa juu na wizara yetu pamoja na Tamisemi kuangalia je miundombinu itakuwa imekaa vizuri?

“Yaani wakati wale wanafika darasa la sita ili wote waende ‘form one’ na tuwe na madarasa mawili pale yote yanakwenda form one, kwa hiyo tunajiandaa sasa hivi na tunataka  tutoe nyaraka ambazo zitatoa maelekezo namna ya kutekeleza, kwa hiyo ni matarajio yetu yaende namna hiyo.

“…siwezi kuconfirm sasa hivi mpaka yatakapokuwa tayari na uhakika wa miundombinu itakapokuwa tayari kuwapokea,” alisema.

Alipoulizwa kama taarifa za kuwapo walimu waliopewa semina kwa ajili ya mitaala mipya, akiri kufanyika kwa semina hizo.

“Yaaah tumewapa semina walimu wawili katika kila shule wa darasa la tatu na la nne na tumetoa mafunzo kwa walimu 22,950 kwa hiyo kimsingi ni kama mwalimu mmoja kwa kila shule, lakini kuna shule zimetoa walimu wawili kwa sababu zipo 16,000 na mia kidogo…ina maana kuna shule zimetoa walimu zaidi ya mmoja kwa sababu ya idadi ya wanafunzi kama ni wengi, lakini shule zote zilitoa walimu zipo zilizotoa mmoja zingine wawili wawili.

Alipoulizwa kama darasa la saba halitakuwapo rasmi kama wakikamilisha maandalizi, Dk. Akwilapo alisema. “eeeh kama tutakamilisha maandalizi hayo tutatangaza, kimsingi ni kwamba wanafunzi hao ukumbuke  walianza na mtaala mpya ule ambao ulianza na masomo ya kusoma, kuandika na kuhesabu yaani KKK kwa darasa la kwanza na la pili tulitoa masomo ya tehama sijui sayansi, yote sasa yanaanzia darasa la tatu.

“Tulisema darasa la kwanza na la pili, wanafunzi wafundishwe kusoma, kuandika na kuhesbu kwa kuwa mahiri wanaingia darasa la tatu wanatumia stadi hizo ili kuyaelewa masomo sayansi, jiografia, tunaingiza uraia na maadili.

“ Sasa maana yake ni nini, baada ya darasa la kwanza na pili kuwa wameimarishwa kuwa mahiri katika kusoma, kuandika na kuhesabu, wanapoingia darasa la tatu wanatumia stadi hizo ili tunaingiza masomo na huo mtaala unaozungumza umeishia darasa la sita.

“Lakini utakuwa flexible kama miundombinu yetu bado kuna mahitaji muhimu tunaweza kuspendi mwaka mmoja, ila lengo ni hilo,”alisema Dk. Akwilapo.

Kuhusu walimu kuhama, Dk. Akwilapo alisema Serikali ingependa kuona walimu wanakaa kwenye vituo vya kazi kwa sababu wamepewa mafunzo.

“Tungependa wakae katika kituo hicho kwa sababu tumewapa mafunzo kwa ajili ya kituo hicho, lakini wanaweza wakahama kwa sababu tuna uwezo wa kufundisha wengine… maelekezo ni kwamba wakifa kule shuleni wenyewe wanakuwa wakufunzi kwa wenzao, si wao wanaweza kufanya mambo haya shule nzima, kuhama si sheria kama ya Mungu, wanaweza kuhama.

Kuhusu shule binafsi kutumia mitaala hiyo, Dk. Akwilapo alisema tayari shule hizo zimepewa mtaala mpya ambao umeandikwa kwa lugha ya Kiingereza na tayari wamepewa mafunzo.

Alipoulizwa tena kama nia ya Serikali ni kufuta darasa la saba, Dk. Akwilapo alisema. “Matarajio yako namna hii, lakini ule mtaala ni flexible wanaanza na mtaala mpya ambao umethibitishwa,” alisema.

 

CWT

Akizungumzia mabadiliko hayo, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alieleza kushtushwa na taarifa hiyo huku akitaka kupewa muda wa siku mbili ili alizungumzie jambo hilo.

“Hayo ni mabadiliko makubwa na ni mshtuko…ndio nasikia kwako sijasikia wala kuona popote. Naomba unipe muda wa kutulia kama siku mbili halafu nitapata cha kuongea,”alisema Mukoba.

Kwa upande wake mdau kutoka taasisi binafsi ya elimu, Benjamin Nkonya alisema mabadiliko hayo yapo katika sera ya elimu ya mwaka 2014.

Kutokana na hilo, Nkonya alikiri kwamba wapo walimu ambao wamekwishaanza mafunzo kwa ajili ya mabadiliko hayo.

“Lakini katika mabadiliko hayo sisi kama wadau wa shule binafsi tulipinga kwamba wanafunzi wa darasa la kwanza na pili wasisome kiingereza. Lakini baadaye tukakubaliana na sera ikatamka kwamba shule inayo uhuru wa kuchagua lugha sasa wasije wakapindisha.

“Sisi shule zetu za binafsi Kiingereza ni kuanzia chekechea. Pia tunapinga hili la wanafunzi kwenda sekondari bila kufanya mtihani, tunapinga kwa nguvu zote kwa sababu kipimo cha mwanafunzi ni mtihani,”alisema Nkonya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles