31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, December 2, 2023

Contact us: [email protected]

BEKI CHAPECOENSE AWASHAURI WACHEZAJI WAPYA

beki-chapecoense-ee
Helio Neto (kushoto), akizungumza na wachezaji wapya wa Chapecoense

 

CHAPECO, BRAZIL

BEKI wa klabu ya Chapecoense ya nchini Brazil ambaye alinusurika kifo katika ajali ya ndege Novemba mwaka jana, Helio Neto, amewashauri wachezaji wapya wa klabu hiyo kuelekea msimu mpya wa ligi.

Mchezaji huyo alikuwa miongoni mwa watu sita ambao walinusurika na kifo huku watu 71 wakipoteza maisha katika ajali hiyo wakiwamo wachezaji 19 pamoja na viongozi wa klabu hiyo.

Ajali hiyo ilitokea Novemba 28 nchini Colombia, huku wachezaji wa klabu hiyo wakielekea kwenye mchezo wa fainali ya kwanza ya Copa Sudamericana dhidi ya Atletico Nacional, ndipo baadhi ya wachezaji walipoteza maisha huku wakibaki watatu.

Klabu hiyo tayari imesajili wachezaji 27 kuziba nafasi za wachezaji ambao wamepoteza maisha, hivyo wachezaji hao wa sasa wanatarajia kuanza kuonesha makeke yao katika msimu mpya wa ligi kuu na tayari wameanza mazoezi kuelekea michuano hiyo.

Miongoni mwa wachezaji walionusurika na kifo hicho ni pamoja na beki wa kati Helio Neto, ambaye juzi alijitokeza katika chumba cha kubadilishia nguo kwa wachezaji wa klabu hiyo na kuwapa ushauri kuelekea michezo yao.

“Karibu ya wachezaji wote ni wageni katika kikosi hiki, lakini klabu imewaamini na kuwapa nafasi ya kufanya yale ambayo yalifanywa na wale ambao hawapo kwa sasa.

“Tunaamini kuna uwezekano mkubwa wa kufanya hivyo kwa kuwa uwezo upo, kikubwa ni kujiamini kama klabu ilivyo waamini.

“Ni wazi kwamba klabu bado haijakamilika na itakuwa vigumu kukamilika kwa mwaka huu, lakini kikubwa ni kupambana kwa ajili ya kurudisha thamani ya timu.

“Tumieni nafasi mliyopewa kuonesha kuwa ni wachezaji bora, tupo nyuma yenu kuhakikisha klabu inafanya vizuri,” alisema Neto.

Kwa upande wa kocha wa klabu hiyo, Vagner Mancini, amedai kuwa muda uliopo ni mdogo kuweza kufanya maandalizi kikubwa ni kupambana hadi hatua ya mwisho.

“Tuna muda mdogo kufanya maandalizi, muda mdogo wa kuijenga timu, lakini tunatakiwa kupambana kwa ajili ya kufikia malengo yetu,” alisema Mancini.

Mkurugenzi wa klabu hiyo, Rui Costa, amedai kuwa wachezaji ambao wamenusurika na kifo kwenye ajali hiyo ya ndege bado nafasi zao zipo ndani ya klabu endapo hali yao itakuwa sawa.

Wachezaji ambao walibaki ni pamoja na beki wa pembeni Alan Ruschel, mlinda mlango Jackson Follmann pamoja na beki wa kati Neto.

Chapecoense inatarajia kushuka dimbani katika mchezo wao wa kwanza msimu huu Januari 26 wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani dhidi ya Joinville.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles