24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Maambukizi ya UKIMWI yazidi kupungua Tanzania, Vijana bado changamoto

*Maambukizi mapya yashuka kutoka 68,000 hadi 54,000

*Idadi ya vifo pia yapungua kutoka 32,000 hadi 29,000

Na Faraja Masinde, Morogoro

Tanzania imepiga hatua katika mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI ambapo takwimu za mwaka 2021 zinaonyesha kuwa maambukizi mapya yamepungua kutoka 68,000 mwaka 2020 hadi 54,000 mwaka 2021.

Sehemu ya washiriki wa Warsha hiyo.

Aidha, idadi ya vifo imepungua kutoka watu 32,000 mwaka 2020 hadi 29,000 mwaka 2021 huku changamoto kubwa ikiendelea kubaki kwa vijana.

Hayo yamebainishwa mjini Morogoro leo Alhamisi Mei 19, 2022 na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania(TACAIDS), Dk. Leonard Maboko kwenye hafla ya kuwajengea uwezo Wahariri na Waandishi wa Habari kuhusu UKIMWI iliyoratibiwa na TACAIDS kwa ufadhili Shirika la Pact Tanzania.

Dk. Maboko amesema kulingana na takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Virusi Vya Uimwi na UKIMWI(UNAIDS), vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wanachangia asilimia 28 ya maambukizi mapya huku kati ya kundi hilo asilimia 73 wakiwa ni vijana wa kike.

“Hali ya maambukizi ya UKIMWI nchini Tanzania inaonyesha kuwa kama nchi tunapiga hatua kubwa, makadirio ya takwimu kwa mwaka 2021 yanaonyesha kwamba maambukizi mapya ni watu 54,000 kwa mwaka huku, upande wa vifo vimeshuka kutoka watu 32,000 mwaka 2020 hadi watu 29,000 mwaka 2021.

“Kwa hiyo matokeo ni mazuri, changamoto tuliyonayo ni vijana hasa tunapozungumzia maambukizi mapya kwani miaka mitano iliyopita tulikuwa tunasema asilimia 40 huku vijana wa kike walikuwa asilimia 80 na sasahivi hali haijabadilika sana kwani takwimu za mwaka 2021 zinaonyesha kuwa maambukizi mapya kwa vijana ni asilimia 28 huku kati yao vijana wa kike wakiwa ni asilimia 73, hii ni hali ambayo bado inatupa changamoto zaidi na nivizuri tuendelee kuweka juhudi katika kuwaelimisha vijana,” amesema Dk. Maboko.

Akizungumzia hali ya vifo vitokanavyo na UKIMWI, Dk. Maboko amesema bado matokea kwa wanaume zaidi ukilinganisha na wanawake nakwamba ndio maana juhudi kubwa zinawekwa ili kuwahimiza kwenda kupima.

“Ndio maana tumeendelea na kampeni kuhakikisha kwamba wanaume wanapima, wanaanza dawa na wanaendelea kutumia dawa zao vizuri kwani wako nyuma ukilinganisha na wanawake na hii ndio itatusaidia kufikia malengo ya kidunia ya sifuri tatu ifikapo mwaka 2030 kwa maana tusiwe na maambukizi mapya, tusiwe na vifo na unyanyapaa kwa sababu ni lengo ya kidunia ndio maana tunaendelea kupambana ili kuelimisha jamii,” amesema Dk. Maboko.

Kuhusu udhibiti wa mlipuko wa VVU amesema bado kazi inaendelea kufanyika kuhakikisha kuwa idadi ya maambukizi mapya ya UKIMWI yanakuwa chini ikilinganisha na vifo.

“Hadi hapo tutakapopunguza idadi ya watu wanaoambukizwa VVU na UKIMWI na kuwa chini ya idadi ya vifo vinavyotokana na UKIMWI ndio maana utaona hata takwimu za mwaka 2021 maambukizi mapya bado yako juu ikilinganishwa na vifo,” amesema Dk. Maboko.

Katika hatua nyingine Dk. Maboko amewaomba waandishi wa habari kuendelea kutoa taarifa kupitia vyombo vya habari namna gani ya kudhibiti mlipuko wa maambukizi mapya ya VVU.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles