23 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

RC Kafulila aagiza kuondolewa Meneja RUWASA Wilaya ya Maswa

*Ni baada ya kushindwa kusimamia miradi ya maji

*Akerwa kupewa takwimu za uongo na RUWASA

 Na Samwel Mwanga,Maswa

“Natoa agizo kwa Meneja wa Ruwasa mkoa wa Simiyu huyu Mhandisi wa Ruwasa wilaya ya Maswa aondolewe abadilishwe kwa kuwa hawezi kusimamia miradi mikubwa ya maji kama hii na utekelezaji huo ufanyike siku ya Jumatatu, Mei 23 mwaka huu,”-Kafulila.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila ameagiza kuondolewa kwa Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(Ruwasa) Wilaya ya Maswa, Mhandisi Lucas Madaha kutokana na kushindwa kusimamia miradi ya Maji iliyoko wilayani humo.

Tenki la maji linalojengwa na Ruwasa kwenye Kijiji cha Sulu wilayani ya Maswa Mkoa wa Simiyu(picha na Samwel Mwanga).

Kafulila amefikia uamuzi huo baada ya kufanya ziara ya kutembelea baadhi ya miradi ya maji inayotekelezwa na Ruwasa na kutoridhishwa na usimamizi wa miradi hiyo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji lakini usimamizi wake umekuwa wa kiwango cha chini kutokana na baadhi ya Watendaji kuwa na uwezo mdogo wa usimamizi.

Amesema alichogundua baada ya kutembelea miradi ya maji inayojengwa kwenye vijiji vya Isanga, Sulu, Masanwa, Kizungu na Inenwa katika wilaya hiyo amebaini kuwa Wakandarasi waliopewa kazi za ujenzi wa miradi hiyo hawasimamiwi ipasavyo na Ofisi ya Ruwasa wilaya ya Maswa.

“Natoa agizo kwa Meneja wa Ruwasa mkoa wa Simiyu huyu Mhandisi wa Ruwasa wilaya ya Maswa aondolewe abadilishwe kwa kuwa hawezi kusimamia miradi mikubwa ya maji kama hii na utekelezaji huo ufanyike siku ya Jumatatu, Mei 23 mwaka huu.

“Ruwasa badilikeni katika usimamizi wa miradi hii ya maji ambayo inapata fedha nyingi toka serikalini ni vizuri Wahandisi wa hawa Wakandarasi mnaowapa kazi za mamilioni haya fedha za walipa kodi, msiwaache wafanye wenyewe tu wasimamieni,” amesema Kafulila.

Amesema kuwa Ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo  kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ngazi ya wilaya iwe inafanya ziara ya kutembelea mara mbili kwa mwezi mmoja kuona utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo hiyo ya maji.

Kafulila pia amesikitishwa na kitendo cha ofisi ya Ruwasa mkoa huo kumpatia takwimu za utekelezaji wa miradi hiyo ikiwa tofauti na takwimu ambazo amezikuta kwenye maeneo ya utekelezaji wa mradi na hivyo kuleta sintofahamu.

“Ofisi ya Ruwasa mkoa takwimu nilizonazo mimi hapa ni tofauti na ambazo nimezikuta huku kwenye miradi hali hii inaleta sintofahamu hivyo tuwe na takwimu ambazo ni sahihi kwa pande zote mbili,” amesema Kafulila.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles