24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif: Vyovyote iwavyo tutashiriki uchaguzi

Mwandishi wetu –Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema chama chake kimebaini kasoro na vikwazo 10 vinavyotatiza kuwepo kwa uchaguzi huru na wa haki, lakini kitakwenda kwenye uchaguzi kwa namna yoyote ile.

Akizungumza na wanahabari Dar es Salaam jana, Maalim Seif alisema duniani kote kipindi cha Uchaguzi Mkuu ni kipindi cha kipekee cha kuamua kuijenga nchi au kuibomoa na kwamba ni vyema Serikali iheshimu umuhimu wa kusimamia uchaguzi huru na wa haki.

Alisema chama chake kimeainisha vikwazo 10 vinavyokwamisha uchaguzi huru na wa haki na kuiomba Serikali kuviondoa.

 “Uchaguzi unaoiacha nchi salama na tulivu ni lazima ufanyike kwenye mazingira ya haki, uhuru, na uwazi. Kinyume chake, chaguzi huzaa uhasama, chuki na machafuko katika taifa. ACT Wazalendo tunapenda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 uwe wa kuijenga badala ya kuibomoa Tanzania.

“Tunahitaji kuwa na uchaguzi utakaowaacha Watanzania wakiwa na furaha na matumaini baada ya kutekeleza haki na wajibu wao wa kidemokrasia wa kuchagua viongozi wanaowataka.

“Kwa bahati mbaya, ikiwa imesalia miezi miwili tu kuelekea kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu, mazingira ya kisiasa nchini hayatoi taswira ya uchaguzi unaoweza kuiacha nchi yetu salama,” alisema Maalim Seif.

VIKWAZO VINAVYOKWAMISHA UCHAGUZI HURU

Akitaja vikwazo alivyoeleza kuwa vinakwamisha uchaguzi huru na wa haki, Maalim Seif alidai cha kwanza ni kutokuwapo kwa tume huru za uchaguzi kwa kuwa kwa muundo wake, tume zote mbili, yaani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), zinaonekana kuwa ni tume za rais badala ya kuwa tume huru za uchaguzi.

Alisema mwenyekiti na mkurugenzi wa NEC na ZEC wanateuliwa na rais (Rais wa Muungano na wa Zanzibar), ambao pia ni Mwenyekiti wa CCM na Makamu Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa Zanzibar na katika ngazi ya halmashauri, wasimamizi wa uchaguzi ni wakurugenzi ambao kwa asilimia kubwa sana ni makada wa CCM.

Maalim Seif alisema kikwazo cha pili ni hujuma katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kwamba Serikali haijayafanyia kazi mapendekezo ya wapinzani ya kuufuta uchaguzi huo wa mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba mwaka jana.

Alidai kuwa uchaguzi huo umesababisha kuwepo kwa viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji ambao hawana uhalali wa kisheria wala wa kisiasa, kwa sababu hawakuchaguliwa na wananchi.

“Kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu, ni wakati mwafaka kwa mamlaka zinazohusika kutathmini kosa hilo la kihistoria,” alisema Maalim Seif.

Alitaja kikwazo cha tatu ni hujuma kwenye uandikishwaji wapigakura Zanzibar.

Alidai kuwa uandikishwaji umetawaliwa na hujuma za makusudi zenye lengo la kuhakikisha kuwa maelfu ya wananchi wananyimwa haki yao ya msingi ya kupiga kura.

“Kikwazo cha nne ni hujuma kwenye ugawaji wa majimbo Zanzibar… ZEC imetangaza kupitia upya idadi na mipaka ya majimbo ya uchaguzi baada ya kuongeza majimbo mwaka 2015 kutoka 50 na kuwa 54.

“Sasa wamepanga kukata upya majimbo ili kuisaidia CCM… Taarifa za uhakika za ndani ya ZEC zinaonyesha mipango yake kwa kushirikiana na CCM inalenga kuyapunguza kutoka 54 waliyoyaongeza mwaka 2015 na kurudi 50, lakini katika muundo tofauti na uliokuwepo kabla ya mwaka 2015.

 “Ni vipi na kwanini mwaka 2015 waliongeza majimbo manne mapya kisiwani Unguja, lakini leo wanapanga kurudisha majimbo 50, wapunguze majimbo mawili kutoka Pemba ambako hawakuongeza jimbo? Haya yote yanathibitisha njama ovu zinazoratibwa na ZEC katika kuhakikisha kuwa uchaguzi unahujumiwa,” alidai Maalim Seif.

Alitaja kikwazo cha tano ni hujuma kwenye kanuni za uchaguzi.

“NEC imeanza mchakato wa mabadiliko ya kanuni na kwa mujibu wa rasimu za kanuni hizo, kukaribisha waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa ni suala la hiyari na mawakala wa vyama vya siasa hawatapewa nakala za viapo ambavyo miaka yote vimetumika kama sehemu ya utambulisho katika vituo vya kupigia kura.

“Haki ya mawakala kupewa nakala za matokeo ya uchaguzi imefanywa kuwa ni suala la hiyari, na kwamba msimamizi wa uchaguzi anayo hiyari ya kuwapatia mawakala nakala za matokeo ya uchaguzi iwapo zitakuwepo za kutosha,” alisema Maalim Seif.

Alitaja kikwazo cha sita ni vyombo vya dola kuamua kuwa mawakala wa CCM, badala ya kusimamia dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao kwa kutenda haki kwa raia wote.

Maalim Seif alitaja kikwazo cha saba ni utawala wa umma kutumika kisiasa.

“Ikiwa ni miaka 28 tangu Tume ya Jaji Nayalali kutoa mapendekezo ya kutenganisha utawala wa umma na siasa, bado nafasi za wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zimeendelea kutumiwa na chama tawala kukibeba kuliko kuwa watumishi wa Watanzania,” alisema.

Alitaja kikwazo cha nane ni vyombo vya habari vya umma kwa fedha za walipakodi ambao ni wananchi, kujigeuza midomo ya CCM badala ya kusimamia uwajibikaji.

“Kikwazo cha tisa ni sheria 40 za ukandamizaji zilizotajwa na Tume ya Nyalali ambazo ilipendekeza ama zifutwe au zifanyiwe marekebisho makubwa kabla ya mfumo wa vyama vingi haujaanza kazi rasmi hapa nchini.

“Lakini kwa makusudi kabisa, na kwa kutambua kuwa sheria hizo 40 za ukandamizaji zingeinufaisha CCM na kuvikandamiza vyama vya upinzani, Serikali za CCM zilikataa kutekeleza pendekezo hilo la Tume ya Nyalali, badala yake sheria kandamizi zimeongezeka katika miaka mitano ikiwemo Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria za Uchaguzi hazikusalimika,” alisema Maalim Seif.

Alitaja kikwazo cha 10 kuwa ni mahakama zisizo huru akidai katika miaka ya karibuni kwa kiwango kikubwa uhuru wa mahakama umetikisika na kutumika kukandamiza haki badala ya kutoa haki.

Alidai kwa sasa hata pale baadhi ya majaji na mahakimu walipoonyesha uthubutu wa kusimamia uadilifu na kulinda utawala wa sheria, Mahakama ya Rufaa ambayo ndiyo mahakama ya juu kabisa imekuwa ikitengua maamuzi hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles