24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

CCM: Ratiba uteuzi wa ndani itolewe

Na Mwandishi Wetu – Dodoma

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeagiza kutolewa mara moja ratiba ya mchakato wa ndani wa uteuzi wa wana CCM wanaoomba kupewa dhamana ya uongozi.

 Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Katibu wa NEC – Itikadi na Uenezi, Humphery Polepole, ilisema Kamati Kuu kwa kauli moja imeridhishwa na kiwango cha maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba.

 “Kamati Kuu imeridhishwa na kuelekeza kutolewa mara moja kwa ratiba ya mchakato wa ndani wa uteuzi wa wana CCM wanaoomba kupewa dhamana ya uongozi katika vyombo vya dola,” ilisema taarifa hiyo.

Ilisema Kamati Kuu (KK) ya Halmashauri Kuu ya Taifa ilikutana katika kikao chake cha kawaida jijini Dodoma jana chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli.

Taarifa hiyo ilisema kamati hiyo ilipokea na kujadili mpango wa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Ilisema kamati pia ilipokea taarifa ya maendeleo ya uandishi wa mwelekeo wa sera za CCM kwa mwaka 2020 – 2030 na kujiridhisha kuwa kazi nzuri imefanyika hadi ngazi ya rasimu ya pili.

“Kamati Kuu pia imepitia kwa mara ya pili taarifa ya uandishi wa Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na imepongeza Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kujumuisha maoni ya wadau mbalimbali na kuelekeza maandalizi ya mwisho ili ilani iwasilishwe katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kwa uamuzi wa mwisho,” ilisema taarifa hiyo.

KUHUSU CORONA

Kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, kamati hiyo ilipokea taarifa ya Serikali na hatua ambazo zimechukuliwa kuukabili kwa mafanikio makubwa nchini.

Taarifa hiyo ilisema kamati baada ya tafakuri ya kina kuhusu taarifa ya Serikali, kwa kauli moja ilimpongeza Rais Magufuli kwa uongozi imara, msimamo thabiti na usioyumba katika kipindi chote cha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

“Kamati Kuu na kwa niaba ya chama, inaendelea kutoa rai kwa umma wa Watanzania kuendelea kuzingatia ushauri na maelekezo ya Serikali na wataalamu wa afya, kumtanguliza Mungu kwa maombi na shukrani na kuendelea kuchapa kazi kwa bidii,” ilisema taarifa hiyo.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,249FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles