26.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

MAALIM SEIF: SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA INAKUJA

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF),  Maalim Seif Sharif Hamad, amesema pamoja na kwamba alipokonywa haki yake katika Uchaguzi Mkuu uliopita, lakini sasa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inakuja.

Maalim Seif ambaye alikua mgombea urais kupitika CUF katika Uchaguzi Mkuu uliopita, ametoa kauli hiyo ikiwa imepita mwaka mmoja na miezi saba sasa tangu ulipofanyika uchaguzi wa marudio Machi 20 mwaka jana.

CUF kiliususia uchaguzi huo wa marudio kwa kile walichodai kuwa ni batili kisheria na katiba.

Kutokana na hilo, chama hicho kilidai kuwa uchaguzi huo ambao ulitangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha si halali kwa kuwa ule halali ulikwishafanyika Oktoba 25 mwaka juzi na kumalizika kwa amani.

Oktoba 28 mwaka 2015, Jecha alitangaza kuufuta uchaguzi huo kwa kile alichodai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa utaratibu na sheria za uchaguzi hasa kisiwani Pemba.

Akizungumza juzi na wajumbe wa Mkutano Mkuu Wilaya ya Mjini Unguja, Maalim Seif ambaye alipata kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali ya awamu ya kwanza, alisema kuwa mabadiliko yapo na kwamba sasa haki inarudi.

Kauli hiyo pia aliirudia alipohudhuria hafla ya kamati ya vyuo vikuu na taasisi ya elimu ya juu ya Umoja wa Vijana wa CUF (JUVICUF) iliyofanyika katika Hoteli ya Mazsons visiwani humo.

Aliwaambia wanachama hao kuwa siku haki itakaporudi watashangaa na kwamba hawataamini kitakachotokea.

“Nimeshuhudia awamu zote za Serikali ya Mapinduzi na nategemea Inshallah nitaishuhudia awamu ya nane itakayoingia kesho kutwa. Mimi na Zanzibar na Zanzibar na mimi.

“Usilolijua ni sawa na usiku wa giza, mimi niwaambieni kuna mikondo inapita chini kwa chini hapa is very few people (watu wachache) wanaojua katika Zanzibar na mpaka bara mabadiliko yapo ‘babu Ali’ anakwenda zake safari na haki inarudi, Mungu atuweke uhai Inshallah nimesema na nitasema hapa jinsi ambavyo haki itarudi mtashangaa nyote.

“Hapa hakuna hata mmoja anajua…mngekuwa mnajua mambo yanavyokwenda na watu wengine wanataka kujinyonga funika kombe mwanaharamu apite.

“Ndugu zangu niwaambieni ‘babu Ali’ kwaheri, inakuja Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Serikali imara, itakayoanza safari yetu ya kwenda Singapore,”alisema Maalim Seif.

Aliwataka vijana hao kushikamana katika suala la siasa kwake hata yeye hakuwahi kuwa na ndoto ya kuwa mwanasiasa lakini alipoingizwa hadi sasa anashindwa kutoka.

“Sikuwa na ndoto za kuwa mwanasiasa lakini niliingizwa kwenye siasa na mpaka sasa siwezi tena kutoka kwenye siasa,” alisema Maalim.

Awali akisoma risala katika hafla iliyoandaliwa na kamati ya vyuo vikuu na taasisi ya elimu ya juu ya chama hicho, Samha Abdallah alisema lengo la hafla hiyo ni kufanya mahojiano na Maalim Seif juu ya hatima ya chama hicho.

“Tukiwa na maana kwamba zimebakia siku tano tu kutimia miezi mitatu uliyouahidi ulimwengu kwamba katika kipindi hicho haki ya Wazanzibari itakuwa imeshapatikana.

“Uamuzi wetu huu wa kukutana na wewe leo (juzi) hautokani na uchache wa imani yetu kwako bali ni tathimini yetu ya kina juu ya mwenendo wa masuala ya siasa ya nchi yetu.

“Mwisho kabisa, pamoja na mambo mengine, kupitia hafla hii tuna imani kubwa kwamba sisi na umma wa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla tutapata neno litakalotufanya tuondoke hapa na matumaini mapya ya kuiendeleza Zanzibar yenye mamlaka kamili,”alisema Abdallah.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles