31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

BUNGE LAMWAGA NYARAKA MATIBABU YA LISSU

Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM

BUNGE la Tanzania kwa mara ya kwanza limeweka wazi uthibitisho wa stakabadhi za malipo ya Sh milioni 43 zilizochangwa na wabunge na kutumwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa ajili ya matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwapo kwa mvutano baina ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ofisi ya Bunge na Hospitali ya Nairobi.

Kutokana na mvutano huo, jana Bunge lililazimika kuweka hadharani vielelezo vya malipo hayo na kusisitiza kuwa fedha hizo zimetumwa.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari, Elimu kwa Umma na Mawasiliano cha Bunge, ilieleza kuwa fedha hizo zilitumwa katika akaunti ya Hospitali ya Nairobi.

“Tunapenda kusisitiza kuwa fedha zilizochangwa na wabunge kwa ajili ya kusaidia matibabu ya mheshimiwa  Lissu zimetumwa katika Hospitali ya Nairobi anakopatiwa matibabu.

“Fedha hizo zimetumwa kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), sawa na Sh 1,977, 120.58 ya Kenya kulingana na viwango vya kubadilishia fedha vya BoT kwa siku hiyo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Risiti ya malipo hayo inaonyesha fedha hizo zilitumwa Septemba 20, mwaka huu, kupitia tawi la BoT la Dodoma kwenda Benki ya Barclays, tawi la Hurlringham, akaunti namba 0451155318 yenye jina la Kenya Hospital Association.

MVUTANO WA MALIPO

Wiki iliyopita Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa licha ya wabunge kukatwa posho zao lakini fedha hizo zilikuwa bado hazijatumwa.

“Fedha hizo hadi leo (Septemba 22) hazijafika bado zinashikiliwa kwa nia zisizojulikana licha ya kwamba zilichangwa na wabunge nikiwemo mimi,” alisema Mbowe.

Hata hivyo muda mfupi baada ya kauli hiyo, Ofisi ya Bunge ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari na kusema kuwa fedha hizo zilitumwa tangu Septemba 20 mwaka huu.

Licha ya ufafanuzi huo, Hospitali ya Nairobi alikolazwa mbunge huyo nayo ilisema kuwa haijapokea fedha zozote kutoka Bunge la Tanzania hadi kufikia juzi jioni.

Mkuu wa Mahusiano ya Umma wa KHA inayomiliki hospitali hiyo, Catherine Njoroge, aliiambia televisheni ya K24 kwamba malipo yalikuwa bado hayajafika kwenya akaunti yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles