28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

TUHUMA NZITO

Na JANETH MUSHI

-ARUSHA

WABUNGE wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki na Godbless Lema wa Arusha Mjini, wameeleza jinsi baadhi ya madiwani wao walivyojiuzulu na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Nassari na Lema waliyasema hayo mjini hapa jana walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari, katika ofisi za chama chao, Wilaya ya Arusha Mjini.

Katika mazungumzo yake, Nassari alisema suala la kuhama kwa madiwani wa chama chao limekuwa likiwapa wakati mgumu hasa walipokuwa wakifikria ni kwa jinsi gani madiwani hao wanaweza kuhamia CCM kwa kisingizio cha kumuunga mkono, Rais Dk. John Magufuli.

“Wakati wa Bunge la Bajeti la mwezi Mei, mwaka huu, tulianza kufuatilia na kufanya uchunguzi ambao niliusimamia mwenyewe ukilenga kubaini chanzo cha madiwani hao kuhama.

“Ili kujiridhisha na kuhama kwa madiwani hao, nilitumia vifaa vyangu vya kisasa vya kielektroniki ambavyo nilitoka navyo Uingereza nilipokuwa masomoni hivi karibuni.

“Vifaa hivyo tuliviweka kwenye magari na ofisi za umma na tukafanikiwa kubaini jinsi madiwani hao walivyodanganywa na baadhi ya wateule wa Rais mkoani hapa na kuhama chama chetu.

“Kwa hiyo, leo nimewaita hapa ili kuwathibitishia pasipo shaka, kwamba madiwani wetu waliojiuzulu na kujiunga CCM, kwa madai ya kumuunga mkono Rais Magufuli, si wakweli hata kidogo.

“Nimefanya uchunguzi huu kwa muda mrefu kwa kutumia vifaa vyangu vya kisasa, nawahakikishia Watanzania, kwamba hakuna diwani aliyehama Chadema na kuhamia CCM kwa sababu tu anamuunga mkono Rais na badala yake wamehama Chadema kwa kuunga mkono rushwa.

“Wapo baadhi ya wateule wa Rais ndani ya Mkoa wa Arusha na wilaya zake ambao wamekuwa vinara wa zoezi hilo la kununua madiwani kwa fedha, kuwaahidi vyeo, kuwaahidi ajira na kutoa ahadi nyingine zikiwamo kuwapa makazi ya kuishi.

“Binafsi, sina tatizo na diwani kuhama chama kwani ni haki yake kikatiba ila nina tatizo na jinsi wanavyohama kwa rushwa na kusingizia wanamuunga mkono Rais.

“Katika hili, ushahidi upo na ninao muda mrefu ila nimelazimika kuusema sasa baada ya kuona juzi aliyekuwa Diwani wetu wa Kimandolu, Mchungaji Greyson Ngowi, kuhamia CCM siku ambayo Rais Magufuli alikuwa akitoa kamisheni kwa maofisa wa Jeshi la Wananchi hapa Arusha.

“Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Rais, kuwa  kuondoka kwa madiwani hao kunatokana na rushwa na si kwamba wanamuunga mkono,” alisema Nassari.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, yuko tayari kukutana na Rais, Mkurugenzi wa Takukuru, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa ili awaonyeshe ushahidi usiotia shaka juu ya suala hilo.

“Lakini, natoa siku 14 niitwe na viongozi hao ili niwaonyeshe na kama wasiponiita, nitauonyesha hadharani.

“Kama Rais atakuwa tayari kuuona nitampa kwa sababu alipokuwa akikabidhiwa ripoti ya madini ya tanzanite na almas, alisema ana flash yenye mambo mengi muhimu.

“Rais amekuwa akipambana na kujipambanua anapingana na rushwa iliyopo ndani ya mfumo na iliyo nje ya mfumo. Kwa hiyo, nataka nimuonyeshe rushwa iliyopo ndani ya mfumo kupitia wateule wake kwa sababu hata mimi flash ninayo.

“Kuna watu wanauliza kwanini nimekaa na ushahidi muda mrefu, lakini nasema wazi kwamba, nilihitaji ‘angle’ nzuri ya kuingilia kwa sababu tulijua pale uwanjani kwenye sherehe za kijeshi, madiwani wawili watapokelewa ingawa baadaye alionekana mmoja.

“Kwa hiyo, nasema msije kuhangaika kuja nyumbani kwangu kunipima mkojo au kutafuta bombadier nyumbani, hamtaipata. Hata flash nyumbani kwangu haipo, hii kitu iko Uingereza na kama mkinikamata tu, kuna mtu atabonyeza kitufe, inaruka hewani.

“Kama nitatoa ushahidi ukaonekana si wa kweli, niko tayari kujiuzulu ubunge wangu kwa sababu baadhi ya fedha walizokuwa wakipewa madiwani hao, zilikuwa zikitoka katika halmashauri,” alisema.

Pamoja na hayo, Nassari alishangazwa na madiwani hao waliohamia CCM kupewa ulinzi wakati wabunge hawana ulinzi wowote pamoja na kuwa na majukumu mazito ya kitaifa.

LEMA

Naye Lema, alisema kitendo cha diwani wa Chadema kukaribishwa CCM katika shughuli za kijeshi, kinaonesha vyombo vya ulinzi na usalama vinaisimamia CCM kwa nguvu zote.

“Katika tukio la jana (juzi), mlimsikia Mkuu wa Majeshi akisema wanajeshi wakae mbali na siasa, lakini baadaye Rais akawaunganisha wanajeshi wawe karibu na siasa.

“Unapoona siasa inafanyika mbele ya jeshi,  maana yake ni maelekezo ya kuvitaka vyombo vya usalama visimamie chama tawala kwa nguvu zote na maana yake ni kwamba, tuna hali mbaya kama vyama vya upinzani.

“Kwa hiyo, mimi kama mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, nalaani kitendo kile kilichofanywa uwanjani kwa kuchanganya kazi za jeshi na siasa,” alisema Lema.

Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Arusha, Frida Wikesi, alipoulizwa kuhusu madai ya rushwa yaliyotolewa na Chadema, aliomba afuatwe ofisini kwake leo.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alipoulizwa juu ya madiwani hao waliohamia CCM kupewa ulinzi, alisema suala hilo halipo kwani wanaolindwa ni viongozi wenye sifa za kulindwa pamoja na watu wanaotishiwa maisha.

Hadi sasa, madiwani tisa wa Chadema wamehamia CCM wakiwamo watano wanaotoka Jimbo la Arumeru Mashariki, wawili Arusha Mjini, mmoja anatoka Monduli na mwingine Longido.

 TAKUKURU

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema iko tayari kupokea ushahidi wa mbunge huyo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola, alimtaka mbunge huyo kupeleka ushahidi huo ili waweze kuufanyia kazi.

“Tuko tayari atuletee tu huo ushahidi,” alisema Mlowola.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles