31 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

Lowassa: Tumieni kura zenu vizuri

3(4)>> Aonya polisi, asema atawapeleka ICC

>> Ashangaa fedha kupelekwa bandari ya Bagamoyo

 

NA FREDY AZZAH, TANGA

MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amewataka Watanzania kutumia vizuri kadi zao za kupigia kura kwa kumchagua yeye kwani watakuwa wamefanya uamuzi wa busara ambao hawataujutia.

Lowassa aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Indian Ocean, eneo la Donge jijini Tanga, huku akisema fedha zilizopelekwa kujenga Bandari ya Bagamoyo, atazipeleka kuimarisha Bandari ya Tanga.

Mkutano wa Lowassa jijini Tanga ulikuwa ni wa pili baada ya ule wa kwanza uliopangwa kufanyika kwenye viwanja vya Tangamano, kuvunjika kutokana na watu kuwa wengi na baadhi yao kuzimia kwa sababu ya kukosa hewa.

“Kura yako ni kura ya uamuzi, ukiitumia vizuri utakuwa umefanya uamuzi mzuri, ukiitumia vibaya, utakuwa ni uamuzi mbaya.

“Tatizo kubwa la Tanga ni ajira na linatokana na viwanda kufa na kufilisiwa, bandari haina kazi ingawa hivi karibuni fedha nyingi zilipelekwa katika Bandari ya Bagamoyo.

“Fedha zile zingeletwa Bandari ya Tanga zingesaidia siyo Tanga tu bali nchi nzima.

“Fedha zimepelekwa Bagamoyo sijui kwa mkataba gani, Serikali yangu ikiingia madarakni, tutaangalia uwezekano wa kufuta mkataba huo na kuzileta fedha hizo Tanga kutengeneza Bandari ya Mwambani,” alisema Lowassa.

Katika hatua nyingine, alisema Jeshi la Polisi, linawanyanyasa wananchi, jambo alilosema litawapeleka kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

“Wakati tunaanza kampeni, nilisema tutakuwa shwari, tutakuwa waungwana, lakini polisi hawajawa waungwana hata kidogo, kwani wamewanyang’anya vijana bodaboda zao, wamewazuia njiani, mambo ambayo si lazima hata kidogo.

“Napenda kuwatahadharisha tena polisi, mchezo wanaofanya si mzuri, na utaratibu huo utawapeleka ICC, tutawashtaki katika Mahakama za Kimataifa, nawaonya waache vijana hawa wafanye kazi zao,” alisema Lowassa.

Akinadi sera zake, Lowassa alisema mambo yatakayofanya Watanzania kutojutia uamuzi wa kumchagua, ni pamoja na kupata elimu bora na bure kuanzia darasa la awali hadi chuo kikuu.

“Sitaki kusikia mtoto wa Kitanzania ambaye hajasoma kwa sababu tutatoa elimu kwa wote bure bila ada wala michango, pia haki na masilahi ya walimu nitazingatia.

“JKT (Jeshi la Kujenga Taifa), tutaliboresha ili lichukue vijana wengi na wakitoka pale wawe wanaweza kuajiriwa popote pale, watafundishwa stadi mbalimbali zitakazowasaidia kwenye maisha yao,” alisema Lowassa.

 

SUMAYE

Naye Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, alisema CCM inaonyesha kila dalili ya kung’ang’ania madaraka. Kutokana na hali hiyo, aliishauri ikubali kuondoka ili iache nchi ikiwa salama.

“Safari hii lazima waondoke mapema kabisa, Dar es Salaam kwa muda mrefu kuna kipindupindu, kama hawawezi kumaliza hata hicho wanaweza nini?

“Wanaweza tu mambo mengine, nchi imejaa rushwa na pia wameshindwa kuleta fedha zilizofichwa nje ya nchi. Fedha zilizoibwa na kufichwa nje, lazima zirudi.

“Tunahitaji machafuko yasitokee, tunahitaji uchaguzi wa huru na haki, waambieni tunataka uchaguzi wa huru na haki kwa sababu tutawashinda.

“Nasikia kuna wazee wanaandaliwa waende Dodoma waseme wamekaa kwenye jamii yao na wameona Lowassa hatakiwi, wataita wazee na vijana kumtukana Lowassa ili ionekane hapendwi, lakini wajue Lowassa anapendwa kwa sababu historia yake inambeba.

“Wasije wakalazimisha wananchi wafanye mabadiliko nje ya sanduku la kura, waache wananchi wafanye biashara mapema, nimejitahidi wakati mwingine kuamka saa tisa usiku kutafakari kwanini CCM ibaki madarakani, lakini siipati.

“Tarehe 25 mwezi huu, kila mtu achukue kalamu yake kutoka nyumbani akapige kura,” alisema Sumaye.

Wakati huo huo, mgombea ubunge Jimbo la Tanga Mjini kupitia CUF, Mussa Mbaruku, alisema licha ya Lowassa kupata kura zaidi ya 180,000 za watu waliojiandikisha kwenye jimbo hilo, suala la Bandari ya Tanga ni vema akalifanyia kazi ili liwakomboe wananchi wake.

Alisema pia kuwa wananchi wa jimbo hilo wanapata vitisho kutoka Jeshi la Polisi pamoja na viongozi wa mkoa na jiji hilo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles