26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Magufuli: Nchi inahitaji rais mkali

g11*Atangaza kiama kwa aliyefungua kesi   kupinga mradi wa maji

*Arusha kombora kwa Kingunge

*Apokewa na CCM, Chadema Ubungo

 

Na Bakari Kimwanga, Dar es Salaam

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema nchi inahitaji rais mkali ili mambo yaende huku akishangazwa na mmoja wa vigogo kufungua kesi kupinga mradi wa maji.

Amesema watu wa aina hiyo watakiona na anamuomba Mungu kwa siki tatu zilizobaki apewe urais kwa vile hao ndiyo ataanza kushughulika nao.

 

Kauli hiyo aliitoa   Dar es Salaam jana kwa nyakati tofauti katika mikutano ya kampeni iliyofanyika   Kigamboni, Mbagala, Temeke, Ubungo na Kinondoni.

Alisema hayuko tayari kuona watu wanaendelea  kupoteza maisha kwa   kipindupindi huku kigogo huyo akikimbilia mahakamani.

Kitendo cha kigogo huyo  kufunga njia ya maji kwa kujenga bomba la majitaka kimesababisha wananchi wa   Dar es Salaam  kupoteza maisha kwa kuugua kipindupindu, alisema.

“Ninajua hapa Temeke kuna mtu amekimbilia mahakamani na kukwamisha mradi wa maji lakini mahakama haitoi haki kwa wakati.

“Zimebaki siku nne ninichague kuwa rais, mtu anachelewesha mradi wa maji kwa kwenda mahakamani ngoja nipate urais. Amejenga juu ya njia ya maji watu wanakufa kwa kipindupindu haki ya Mungu ngoja nipate urais.

“…tunahitaji rais mkali mambo yaende kesi ni lazima iamuriwe kama Serikali tumeshindwa tukate rufaa. Tena huyo mtu aliyefungua kesi ana udugu na mmoja wa wagombea wa Ukawa,” alisema Dk. Magufuli.

Mgombea huyo wa urais alisema  atakapochaguliwa Jumapili atakwenda kuanza na hilo.

“Haiwezekani, haiwezekani, haiwezekani mradi wa maji una manufaa wao wanakunywa maji ya Kilimanjaro wananchi wanateseka. Lakini watu wachache kwa tamaa zao na madaraka yao wanakwamisha.

“Wanasema mimi ni mkali, hapana nina hofu ya Mungu, tunaomba kesi hii iamuriwe kama tumeshindwa tukate rufaa,” alisema Dk. Magufuli

Mgombea huyo wa urais alisema yeye ni mtu wa uamuzi makini anayekuja kuijenga Tanzania mpya na yenye matumaini kwa watanzania wote.

Alisema anashangazwa na watu wanaohangaika na uamuzi mgumu kwani wanaofanya hivyo ni majambazi, wezi na mafisadi pekee.

 

Dk. Magufuli, alisema ataongoza taifa kwa umakini kwa kuleta maendeleo ya kweli.

Alisema anashangazwa na watu wanaopita na kujinasibu kwa kuleta uamuzi mgumu wakati ndiyo walioleta matatizo katika nchi na hata kusababisha kero ya umeme kila kukicha.

“Watakuja wapinzani wetu na kusema eti wanakuja na uamuzi mgumu, jamani uamuzi mgumu hufanywa na majambazi, wezi na wauaji wa watu wenye albino. Inashangaza sana hawa watu msiwakubalie hata kidogo.

“… hivi jana itokee upate mume au mke anayetamba kwa kuwa na uamuzi mgumu si atakunyonga kitandani. Eti atafanya uamuzi mgumu mbona hujinyongi kwa kamba?  Mimi kwangu Magufuli kazi tu,” alisema Dk. Magufuli.

Akizungumzia ujenzi wa daraja la Kigamboni, Dk. Magufuli alisema litakamilika mwezi ujao na wananchi wa eneo hilo watavuka bure ila watu wenye magari ndiyo watakaolipa ada.

 

Alisema yeye ni mtu anayesimamia sheria hivyo katu hawezi kuzivunja   kwa kutoa ahadi za uongo kwa lengo la kutafuta kura za watanzania.

“Daraja la Kigamboni litakamilika mapema mwezi ujao na litakapokamilika wakazi wa Kigamboni watapita bure ila wenye magari watalipia kama ilivyokuwa kwenye kivuko cha pantoni.

“Kigamboni ya sasa imekuwa na maendeleo na kwa sababu mbunge wenu, Dk. Ndugulile (Faustine) ni mfuatiliaji nami nawaomba mumchague ninamuhitaji.

“Alipambana kwa ajili ya yenu na sasa ninasema hapa Rais Jakaya Kikwete amenisaidia sana kwa kuiteua Kigamboni kuwa wilaya nami kazi yangu itakuwa ni kuleta maendeleo ya kweli,” alisema.

Mgombea huyo wa urais alisema kwa mujibu wa sheria, ardhi ni mali hivyo kwa Kigamboni kujengwa mji mpya ni hatua kubwa ya maendeleo.

 

Dk. Magufuli aliwataka wakazi hao kuhakikisha wanasimamia haki zao ikiwamo kumiliki ardhi yao na hata kushirikiana na wawekezaji.

“Ardhi ni mali na hapa Kigamboni sasa mji mpya   wakija wawekezaji kwanza wawape noti na hata mshirikiane pamoja kutokana na ardhi yenu,” alisema.

 

Kombora wa Kingunge

 

Akizungumza bila kumtaja jina, Dk. Magufuli, alisema anashangazwa na baadhi ya watu kueneza maneno ya uongo kuwa anavunja Soko la Mbagala.

Alisema misingi na hofu hiyo ya inatokana na misingi iliyowekwa na waziri wa zamani wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Dk. Magufuli alisema waziri huyo aliongoza wizara hiyo miaka kadhaa iliyopita (Kingunge Ngombale Mwiru),  na sasa amekuwa akipiga debe upande wa pili.

“Kwanza nataka kusema hapa siwezi kubomoa Soko la Mbagala ila ninachotaka kusema tunataka kuliboresha na kulipanua   liendane na mahitaji ya kisasa.

“Mbagala sasa ni jimbo na baadaye inaelekea kuwa wilaya ni lazima iendane na hadhi yake jamani,” alisema

CCM, Chadema wampokea Ubungo

Mgombea huyo wa urais wa CCM alipofika katika Kituo cha Mabasi Ubungo, alisimama na kuwapongeza wafuasi wa vyama vya CCM na Chadema kumpokea.

Alisema hatua ya kupambwa kwa bendera za CCM na Chadema ni ishara nzuri kwake na sasa anaota kuwa anakuwa rais wa awamu ya tano.

“Jiji la Dar es Salaam ambalo lina wakazi wengi unapokuta limepambwa na bendera za CCM, Chadema na CUF nawapongeza sana na hii inaonyesha upendo mkubwa kwangu Magufuli ambaye sasa naota nimeshakuwa rais wa awamu ya tano.

“Maendeleo hayana chama iwe Chadema, CCM, CUF na hata Ukawa mimi kwangu ni kazi tu,” alisema.

 

 

Warioba

 

Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, aliwashangaa watu wanaoendelea kusema CCM imefanya makosa kwenye uteuzi wakati wao walikuwa na mgombea wao.

Alisema badala ya kuona mipango yao imekwama sasa wanaanza kudai CCM imekosa pumzi kuliko wao.

“Eti wanasema CCM imeishiwa pumzi nayasema haya mwaka 1995 nilikuwa mgombea na tulikuwa 17 na haijawahi Halmashauri Kuu kuteua majina zaidi ya matatu.

“Kufanya hivyo ni sawa na kuruhusu vurugu. Sasa leo kuna mtu anatumia zaidi ya saa moja kueleza histori, je kati ya CCM naye yeye nani ameishiwa pumzi?” alisema na kuhoji Jaji Warioba.

 

UVCCM

 

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, alidai hivi sasa kuna vijana wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanaoandaa vurugu ikiwamo ya kuchoma gari la mgombea urais wa Chadema na kuihusisha CCM.

Alisema   CCM inajua mikakati hiyo kama njia ya kutafuta kura za huruma kwa watanzania wakati wameshashindwa uchaguzi.

 

Polisi juu ya paa

 

Jana Jeshi la Polisi liliimarisha ulinzi kwa staili ya aina yake ambako katika mkutano uliofanyika katika Uwanja wa Biafra, Kinondoni, askari  walipanda juu ya majengo ya Chuo Kikuu Huria (OUT).

 

Wakiwa juu ya paa hilo  polisi hao walionekana wakizunguka huku na kule wakiwa na silaha za moto yakiwamo mabomu ya machozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles