25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA KUZINDUA KAMPENI MONDULI LEO

Na JANETH MUSHI, MONDULI


WAZIRI Mkuu mstaafu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa, Edward Lowassa, leo anatarajia kuzindua kampeni za mgombea ubunge wa chama hicho, Jimbo la Monduli.

Chama hicho kimemsimamisha Yonas Laizer, baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Julius Kalanga, kujiuzulu na kuhamia CCM.

Mbali na kuzindua kampeni hizo, Lowasa ndiye atakayekuwa Mwenyekiti wa Kampeni za mgombea huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana wilayani hapa, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema Taifa (Bavicha), Patrick ole Sosopi, alisema kampeni hizo zitazinduliwa katika Kata ya Mto wa Mbu.

Ole Sosopi ambaye pia ameteuliwa na Kamati Kuu ya Chadema kuwa Operesheni Kamanda katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Septemba 16, mwaka huu, alisema wengine watakaoshiriki katika uzinduzi huo ni pamoja na baadhi ya wabunge japokuwa viongozi wengine wakuu wa chama hicho, wanatarajiwa kushiriki katika kampeni hizo kwa siku tofauti.

Pamoja na hayo, Ole Sosopi alitumia nafasi hiyo kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kusimamia uchaguzi huo kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa na kwamba hawatakubali jambo lolote lifanyike kinyume na taratibu.

“Nitumie fursa hii kuisihi NEC, kwamba Chadema ni chama cha siasa na tunajua taratibu na sheria. Katika uchaguzi huu, tunaiomba NEC iache ‘double standards’ na hili tunalieleza mapema kabisa japo hatujaona tatizo lolote.

“Kutokana na mazingira ya kisiasa yalivyo katika nchi yetu, hatutaweza kuvumilia, yaani kama kuna jambo lolote linatokea kinyume cha sheria, hatutaona aibu ama hatutakuwa na hofu yoyote ya kuchukua hatua ambazo tunaona zinaweza kutusaidia kutetea haki yetu.

“Tunaiomba NEC isimamie uchaguzi isipendelee chama chochote cha siasa na taratibu zozote zinazopaswa kufanyika, wadau wakubwa katika uchaguzi ni vyama vya siasa vyenye wagombea na ikitokea kuna jambo, tuitane kwenye vikao tufanye maamuzi,” alisema Ole Sosopi.

Kuhusu Jeshi la Polisi, aliliomba jeshi hilo ambalo ndilo linalosimamia amani kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, visiingilie uchaguzi huo kwa kukipendelea chama kimoja.

“Katika chaguzi za hivi karibuni tumeshuhudia polisi wanavyoshiriki kwenye uchaguzi ndiyo maana tunasema sisi Chadema  ‘we are not fighting against police kwa sababu tuna imani na Jeshi la Polisi, lakini hatuna imani na utendaji kazi wa Jeshi la Polisi kwa sababu ya namna ambavyo wakati mwingine wanatufanya.

“Hapa Monduli, hatutegemei kuona magari mengi ya kutisha watu, huu ni uchaguzi wa kidemokrasia watu wanahitaji kupiga kura, lakini siyo kuonyesha nguvu kubwa.

“Pia, hatutegemei polisi waendeleze double standard zake, hii ni Monduli na ina historia yake na siasa yake na watu wanajitambua, tunatoa onyo kwa vyombo vyote vinavyohusika na uchaguzi huu visiingilie, waturuhusu wanasiasa tufanye siasa na mwisho wa siku wananchi watakwenda kuamua,”alisema

Kwa upande wake, mgombea ubunge ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Lepurko, alisema katika kipindi cha miaka miwili iliyobaki, akichaguliwa kuongoza jimbo hilo vipaumbele vyake vitakuwa ni maji ambalo bado ni tatizo kwa wananchi wa jimbo.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles