MTIKISIKO BUNGENI

0
828

Mwandishi wetu, Dar es Salaam


IKIWA ni takribani miezi miwili tangu Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2018/19 ianze kutekelezwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia na makamu wake, Jitu Soni, wamejiuzulu nafasi zao.

Ghasia ambaye ni Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM) na Soni (CCM-Babati Vijijini), walitangaza uamuzi wao jana mjini Dodoma, huku wakiacha maswali mengi miongoni mwa wanajamii.

Spika wa Bunge Job Ndugai, alipotafutwa kuthibitisha taarifa hizo  alisema, “naomba mpigie Katibu (Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai) atakupa majibu, niko kwenye kikao kwa sasa.”

Kagaigai alipotafutwa alisema ni kweli viongozi hao wa kamati wamejiuzulu lakini hajui ni kwa sababu gani.

“Ni kweli wamejiuzulu ila sababu bado sijajua, ni wao wanajua, ni siri yao labda uwapigie wenyewe uwaulize,” alisema Kagaigai.

Ghasia alipopigiwa  simu yake ilikuwa ikiita bila kujibiwa wakati Jitu Soni  alipatikana lakini akasema atafutwe jioni saa 11 kwa kuwa alikuwa kwenye kikao na  Spika.

Hata hivyo, jioni alipotafutwa  simu yake ilikuwa haipokelewi.

Baada ya taarifa za viongozi hao kujiuzulu  kusambaa, Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe, kupitia ukurasa wake wa Twitter aliandika, “Nimesikitishwa sana na uamuzi huu. Kamati ya Bajeti ya Hawa Ghasia ilikuwa imeanza kurejesha heshima ya Bunge. Ndiyo siasa za zama hizi. Asante sana Hawa kwa kazi uliyofanya.”

Baadhi ya watu wameuhusisha uamuzi huo na namna kamati hiyo ilivyochuana na Serikali wakati wa kupitisha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018/19.

Sheria hiyo ilizua mvutano mkali kuhusu kifungu  kilichotaka fedha za mauzo ya korosho nje ya nchi (export levy), zote ziende Mfuko Mkuu wa Serikali, tofauti na awali ambako ni asilimia 35tu iliyokuwa ikipelekwa huko na asilimia 65 ikienda mfuko wa kuendeleza sekta ya korosho.

Kundi jingine pia limesema kuna baadhi ya sheria ambazo kamati hiyo imeonekana kuzipinga wakati huu ambao Bunge linatarajiwa kukaa wiki ijayo kupitisha sheria mbalimbali.

Katika Bunge lililopita, Ghasia alionekana kuwa mbogo juu ya sheria hiyo ya fedha, hali iliyofanya kamati hiyo kukaa mara kadhaa na Serikali kuijadili lakini mpaka mwisho Serikali ilishikilia msimamo wake.

Julai 3 baada ya Bunge kupitisha sheria hiyo na Bajeti Kuu ya Serikali, Rais John Magufuli alisema  ilipangwa watimuliwe  uanachama wabunge wa mikoa ya Lindi na Mtwara iwapo wangekwamisha Sheria ya Bajeti ya mwaka 2018.

Rais Magufuli alisema hata kama Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, naye angekuwamo katika kupinga mapendekezo ya Serikali, angetimuliwa.

Mjadala wa sheria hiyo na ule  wa korosho kwa ujumla wake, ulihusisha pia  Sh bilioni 200 ambazo wabunge wa kusini walidai Serikali imezikusanya lakini haijazirejesha kwa wakulima.

Hatua hiyo iliwafanya wabunge wa mikoa ya Kusini kuungana na wanaotoka mikoa mingine inayolima korosho kuibana Serikali, huku baadhi ya wabunge wa CCM wakisema mabadiliko na kutolipwa kwa fedha hizo kutakiua chama hicho katika mikoa hiyo.

Majimbo ya mikoa ya Kusini yako 18, Mtwara ikiwa nayo 10 na Lindi manane.  CCM inaongoza kwa kuwa na majimbo 11 huku upinzani inayo saba. Ukijumlisha na wabunge wawili wa viti maalumu, mmoja wa Lindi na mwingine wa Mtwara wanakuwa 13 wa CCM.Wakati Bunge la Bajeti likiendelea, Ghasia pia aliwatuhumu baadhi ya wabunge aliosema walikuwa wamepangwa kwa ajili ya kuwazomea waliokuwa wanatetea zao la korosho.

“Kuna wabunge wamekaa vikao, wameandaliwa waje kutudhalilisha wabunge tunaowatetea wakulima.

“Wabunge wote tuna haki sawa za kutetea wananchi wetu, anayetoka katika pamba atetee pamba, anayetoka katika madini atatetea madini yake na anayetoka katika korosho atatetea wa korosho.’

“Niwahakikishie wakulima wanaolima korosho wabunge wao tutapambamba na hata haki isipopatikana ila tutawatetea. Tunaambiwa sisi wabinafsi, korosho inalimwa kwa kiwango kikubwa na mikoa miwili au mitatu lakini tulipokaa katika kamati tukakubaliana na kwenda mikoa 17,”

“Leo tunaambiwa sisi wabinafsi, kuna watu wanakuja kusimama wanasema wanaijua korosho kuliko sisi. Mimi utafiti wangu wa shahada ya kwanza na ya pili unahusu korosho. Leo mtu anakuja humu anasema anaijua korosho na ninasema kila mtu atetee lake na wananchi mjiandae kuwasikia,” alisema.

Baada ya Ghasia kumaliza kuchangia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama, alisema Serikali haina nia ovu na suala la korosho na haina nia ya kuwanyanyasa wakulima wa zao hilo.

Katika ufafanuzi wake kuhusu mvutano huo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, alisema jambo hilo lisiligawe Bunge.

Aliwataka wabunge kusubiri hoja zitakazotolewa na Serikali wakati ikijibu jambo hilo.

Katika kupitisha Sheria ya Fedha, Kamati ya Ghasia ilitaka Serikali kutofuta kifungu cha 17A cha Sheria ya Sekta ya Korosho  kuruhusu ushuru unaotokana na mauzo ya korosho ghafi nje ya nchi kuingizwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Ghasia akisoma taarifa yake alisema asilimia 65 ya ushuru wa korosho unapaswa kuachwa ili fedha hizo zipelekwe katika mfuko wa bodi ya korosho kupitia Wizara ya Kilimo.

Alisema kwa upande wake Serikali inapendekeza kufuta kifungu cha 17A cha Sheria ya Tasnia ya Korosho sura 203 lengo likiwa ni kuondoa utaratibu uliopo sasa wa mgawanyo wa mapato yanayotokana na mauzo ya korosho nje ya nchi (export levy).

Alisema kwa utaratibu wa sasa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, zinaenda asilimia 35 na asilimia 65 zinapelekwa mfuko wa kuendeleza sekta ya korosho.

“Kwa kuwa majukumu ya kuendeleza zao hilo yamehamishiwa kwenye bodi ya korosho, kamati inapendekeza fedha kwa ajili ya kuendeleza zao la korosho zipelekwe bodi ya korosho kwa mgawanyo utakaokubalika kati ya serikali na wadau wa korosho…………

Kwa Habari Kamili 

JIPATIE NAKALA  YAKO YA GAZETI LA MTANZANIA!!

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here