Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu wa zamani,Edward Lowassa amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali pamoja na taasisi za dini kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani Morogoro.
Alisema hayo jana,wakati wa ibaada maalumu ya shukrani ya Askofu Jacob Mameo Ole Paulo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Morogoro ya kutimiza miaka 25 ya ndoa na 25 ya uchungaji.
Ibada iliyofanyika Usharika wa Bungo, Morogoro mjini, iliongozwa na Askofu Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Fredrick Shoo
Lowassa ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2015, aligombea urais kupitia muungano wa upinzani kabla ya kurejea CCM mwaka huu, alisema hali ya vurugu kati ya wafugaji na wakulima mkoani humo sasa ni shwari.
“Zamani ilikuwa ukifungua vyombo vya habari, unasikia migogoro ya wafugaji na wakulima Morogoro.
“Sasa hali ni shwari, ninawaomba viongozi na waumini wote tuendelee kuuombea mkoa huu uzidi kuwa na Amani na mshikamano”
Alisema Askofu Ole Mameo amekuwa kielelezo kizuri cha kujichanganya na watu na kutatua matatizo yao na kwamba ni mfano mwema kwa viongozi wa kanisa na kiserikali pia.
Aliipongeza Serikali ya Mkoa wa Morogoro kwa kusimamia vyema suala la utunzaji wa mazingira.
“Serikali ya Mkoa wa Morogoro kwa utunzaji mzuri sana wa mazingira. Hongera sana mkuu wa mkoa, viongozi na watendaji wote,”alisema.
Askofu Dk. Shoo alisema Askofu Mameo amekuwa mstari wa mbele katika usuluhishi wa migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani humo.
“ Amani siku zote, imekuwa kipaumbele katika kazi yake yote,”alisema,
Ibada hiyo, iliudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na kidini mkoani humo.