24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 29, 2023

Contact us: [email protected]

Louis Emil Shayo: Padri aliyesimama altareni miaka 70

*Atimiza miaka 100, asimulia alivyotaka kupigana na Askofu

Na Upendo Mosha-Moshi

PADRI mkongwe mwenye umri wa miaka 100, Louis Emil Shayo amesimulia namna alivyohudumu katika nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka 70 na changamoto alizopitia na hata wakati fulani kutaka kupigana na mzungu ambaye alikuwa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi kupinga ukandamizaji kwa watawa wa Afrika.

Padri huyo ambaye ametimiza miaka 100 Juni 30, mwaka huu na kufanya tukio la  kumshukuru Mungu  Julai  mosi mwaka huu, katika Parokia ya Mwenge Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Manispaa ya Moshi ni Mwafrika wa 16  kupata upadri Juni 25, 1950.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA Jumapili katika kituo cha  mapadri cha Longuo (nyumba ya kulelea mapadri wazee) Padri  Louis, alisema yeye alizaliwa Juni 06, 1920 katika Kijiji cha Ima Kilema, wilayani Moshi Vijijini.

Akieleza historia fupi ya maisha yake ya utume alisema amepitia changamoto mbalimbali ikiwemo kunyanyaswa na wakoloni.

Alisema  kabla ya nchi yetu kupata Uhuru alifanikiwa kupata upandri ambapo pamoja na mambo mengine alikuwa mstari wa mbele kutetea haki na kupigania maslahi ya watanzania ikiwemo watawa wenzake.

Akiwa Padri alisema ilitokea wakati mmoja alitaka kupigana na Askofu wa Kijerumani  aliyemtaja kwa jina moja tu la Joseph kwa lengo la kupinga unyanyasaji na uonevu.

“Hapo zamani tulifanya kazi kwa ugumu sana kwani wazungu walituchukulia sisi kama watu wachini sana mapadri  wengi tuliishi kwa unafiki mwingi hali haikuwa sawa kabisa…daima wazungu walituona sisi wajinga lakini sikukubali nilishughulika nao kisawasawa,”alisimulia na kuongeza;

“Wananchi wengi hasa wa zamani wananijua kwamba mimi nilipigana na mzungu ambaye alikuwa askofu kipindi hicho na

sikumpiga kwasababu gani nilifanya hivyo kupigania haki na kukataa ukandamizaji,”alisema.

Akielezea kisa hicho, Padri Louis alisema kilitokea mwaka 1953 baada ya kutofautiana na padre mwenzake mwenye asili ya Amerika.

Alisema padri huyo baada ya kutofautiana naye alipeleka maneo ya uongo kwa Askofu wao Joseph ambaye alimwandikia barua akimtaka atoe maelezo lakini hakufanya hivyo.

Anakumbuka siku hiyo hiyo alipoandikiwa barua na kushindwa kuijibu alikutana na Askofu huyo ambaye alimshambulia kwa maneno ya kibaguzi na yeye kujibu hali iliyosababisha kutaka wapigane.

Alisema ingawa hakupigana naye na wala hakuchukuliwa hatua yeyote kwa sababu alionewa hadi pale walipoondoka  lakini watu wengi hasa wale wa zamani wanajua kwamba alipigana na Askofu huyo.

FAMILIA YAKE

Padri Louis alisema katika familia yao walizaliwa watoto tisa kati yao wakiume walikuwa watano na  wakike wanne ambapo mapadri walikuwa yeye pamoja na mdogo wake aitwaye Padri Apolnary Shayo.

Alisema yeye amefanya utumishi wa upadri kwa zaidi ya miaka 70 na mdogo wake aliyefariki akiwa na umri wa miaka 88  alikuwa padri kwa zaidi ya miaka 50 katika Jimbo katoliki la Moshi mkoani  Kilimanjaro.

“Kwenye familia yetu watano wamekwisha fariki akiwemo mdogo wangu huyo aliyekuwa padre amefariki mwaka mmoja na nusu uliopita na tulikuwa tukiishi wote katika nyumba hii ya mapadri,”alisema.

Padri Louis ambaye licha ya kuwa na umri mkubwa anatumia vifaa ya kisasa kama simu na iPad na amekuwa akipata habari mbalimbali katika mitandao ya kijamaii kama whatsApp na Facebook.

Padri huyo maarufu kama ‘Babu’ pia amekuwa akisoma pasipo kutumia miwani na macho yake bado maangavu, mwili wake ni mkakamavu na muda mwingi amekuwa akiutumia kujisomea vitabu vya dini na kupiga soga na ni mcheshi kweli kweli.

Hii hapa ni sehemu ya mahojiano kati ya mwandishi wetu na Padri Louis.

Mwandishi: Historia yako ikoje tangu uanze utume wa kuwa Padri hadi sasa?.

Padri Louis:Nilizaliwa Juni 30 mwaka 1920 katika Kijiji Cha Ima Kilema,Moshi Vijijini.

Mwandishi:Safari yako ya Upadri ilianzaje?

Padri:Nilianza safari hii septemba 9 mwaka 1932 nikiwa na umri wa miaka 11 ambapo nilijiunga na Shule ya Seminari ya Kilema nikitokea  darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kilema.

Mwandishi: Ilikuwaje baada ya kuanza kusoma seminari?

Padri: safari hiyo haikuwa rahisi kwani tulikuwa vijana 20 ambapo 19 walikuwa na umri wa miaka 18 Mimi peke yangu ndio nilikiwa mdogo.

Mwandishi: wewe na wenzako mlikubaliwa wote kusoma seminari?

Padri: Hapana wote walifukuzwa ila mimi kwasababu nilikuwa mdogo walinionea huruma na kipindi hicho seminari ya Kilema tu ndio ilikuwa ikifanya mitihani ya serikali ya kikoloni.

Mwandishi:baadae ikawaje?

Padri: Niliendelea na masomo yangu hadi nilipo padrishwa mwaka 1950 kabla ya nchi yetu kupata Uhuru ambapo nilikuwa mwafrika wa 16 kupadrishwa pale Kondoa.

Mwandishi: Je katika darasa lenu mlikuwa wangapi na wangapi walifanikiwa kupata upadrisho?

Padri: Tulikuwa Waafrika 40 na ni mimi peke yangu na kijana mmoja tulipata upadrisho ilikuwa ni ngumu sana kuwa padri kipindi hicho.

Mwandishi: Baada ya kupata upadri ulianza kazi hiyo mwaka gani?

Padri: Kazi rasmi ya utume nilianza mwaka 1951 ambapo nilitumikia parokia mbalimbali Jimbo la Moshi.

Mwandishi: Baada ya kupadrishwa na kuwa padri watu walikuchukuliaje haswa wakoloni kipindi hicho?

Padri: Kwa upande wa Waafrika ilikuwa ni jambo la kujivunia sana ila wenzetu wazungu ubaguzi ulikuwa juu sana na tuliishi kwa unafiki mkubwa, ukweli na haki havikuwepo.

Mwandishi: wazungu (wakoloni)walikuwa wanakuonaje?

Padri: Walituona wajinga na kutunyanyasa wakati fulani niliitwa na padri mwenzangu wa kizungu na kuniamuru nikae na kusimama kila wakati nilikataa na kuondoka.

Mwandishi: Ulichukulije hali hiyo ya unyanyasaji?

Padri: Nilikuwa mkali sana na sikutaka ujinga kuna wakati watu walisema nilipigana na askofu wa kizungu wanasema hivyo ila sikupigana nae tu sikutaka sisi tuteseke nilipinga ukandamizaji.

Mwandishi: Je ni tukio gani baya zaidi ambalo lilowahi kukutokea na zuri zaidi wakati ukiwa  katika kazi yako hii ya kitume?

Padri: Siwezi kusema jambo baya zaidi wala zuri zaidi ila nimepitia mengi magumu sana.

Mwandishi: Kitu gani unakikumbuka wakati huo?

Padri: Nilikuwa padri wa kwanza kujua kompyuta kipindi hicho na nilienda Zambia kusoma uandishi wa habari ila sikuufanyia kazi.

Mwandishi: Mbali na kujifunza kompyuta nini kingine ulijifunza?

Padri: Nilijifunza kilatini na Kifaransa…kilatini naongea Kama ninavyoona Kiswahili kwani ulikuwa kama huwezi kuzungumza huwezi kuwa padri kwani ibada ilikuwa ikiendeshwa kwa lugha hiyo…kuendesha ibada Kiswahili iliruhusiwa mwaka 1971.

Mwandishi: Ni tofauti gani unayoiona kwa mapadri wa sasa na wa zamani na unatoa ushauri gani kwao?

Padri:  Mapadri wa sasa utandawazi unaharibu lazima wawe waangalifu na  muhimu wazingatie maadili na wakubali kupokea mambo mazito yanayoumiza mioyo yao bila kulaumu na kutoa sadaka.

Mwandishi: Kuna tofauti gani ya malezi ya sasa na zamani?

Padri: Tofauti ni kubwa sana kwani wazazi wetu walitulea kwa maadili, mimi siwezi kuwafikia pamoja na kusoma kwangu kote.

ANAVYOZUNGUMZIWA

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha mapadri Longuo, Padri Deodatus Bahati, alisema kituo hicho kina hudumia mapadri 13 wazee akiwemo  Padri Louis.

Akimzungumzia Padri huyo mkongwe, Padri Bahati alieleza kuwa licha ya kuwa mzee kuliko wote bado yupo makini katika mambo anayoyafanya na kwamba ni mtu mwenye kumbukumbu imara.

“Babu ni mtu wa kipekee kwani yupo makini katika kusikiliza na kutoa uamuzi ni mtu mwenye upendo, mnyenyekevu ambaye pia anakemea maovu na licha ya umri wake bado anapenda kukosolewa,”.

Aidha alisema licha ya kuwa mzee pia amekuwa akijitoa kwa jamii na watu wenye kipato cha chini katika kuwawezesha kiuchumi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuwapatia mitaji ya kufuga kuku wa nyama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,259FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles