25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

NIMR waja na dawa ya asili inayotibu tezi dume

Na CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

TIBA: Mtafiti wa NIMR katika bandala Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Abel Mdemu akiwaeleza wateja jinsi dawa ya asili ya Tezi dume inavyotumika katika Maonyesho ya 43 ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) jana.PICHA:IMANI NATHANIEL

TAASISI ya Taifa ya Utafiti Magonjwa ya Binadamu (NIMR), imesema imeboresha dawa inayotibu tezi dume aina ya Persivin ambayo imeonyesha ina uwezo mkubwa wa kutibu maradhi hayo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa  (DITF), kwenye banda la Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Mtafiti NIMR, Abel Mdemu, alisema dawa hiyo imeonyesha ina uwezo mkubwa kutibu uvimbe wa tezi dume.

“Dawa hii walikuwa awali wakitumia waganga wa tiba asilia, tangu mwaka 2013 tumeifanyia utafiti kwa kuiongezea thamani na kuboresha ili iweze kutumika,”alisema Mdemu.

Alisema utafiti wa awali umeonyesha wagonjwa wengi waliotumia dawa hiyo, walirudi tena kwao wakiwa na vyeti vilivyoonyesha kuwa wamepona.

“Dawa hii imeonyesha uwezo mkubwa na wengi waliyoitumia wamepona, dozi yake ni ya miezi mitatu na tunaiuza kwa Sh 360,000,”alisema Mdemu.

Mdemu alisema wanapobaini tezi dume ina dalili za saratani, huchanganya na dawa Persivin na nyingine ya Nimregenin ili kutibu.

Alisema mchanganyiko huo pia, umetoa matokeo mazuri ambapo baadhi ya wagonjwa wamepona.

Alisema dawa hiyo hutengenezwa kwa miti ya asili na imejipatia soko kubwa kuliko dawa nyingine.

Mdemu alisema Serikali tayari ipo kwenye mchakato wa kuleta mitambo ya kisasa ambayo itasaidia dawa hiyo kuzalishwa kwa wingi.

Alisema kinachowakwamisha kuanza kuisambaza dawa hiyo ni kwa sababu ya hawana miundombinu ya uzalishaji iliyokidhi viwango vya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Alisema Shirika la Afya Duniani (WHO), limetoa mwongozo wa Dawa za asili kabla ya kuingia sokoni hivyo wanafuata taratibu hizo.

“Dawa zinatibu magonjwa mengi ambayo Serikali inanunua kutoka nje hivyo kukamilisha kwa dawa hi kutaondoa mzigo kwa Taifa,”alisema Mdemu.

Alisema COSTECH wameisadia taasisi hiyo Sh. bilioni 400 kuboresha miundombinu ya maabara lengo ya kuchunguza ubora wa dawa.

Mdemu alisema Nimr iliamua kufanya tafiti za ugonjwa huo kwa sababu ya kasi yake ambapo wanaume wenye umri kati ya miaka 40 hadi 60 ndio wako kwenye hatari zaidi.

“Wakifika umri wa miaka 70 hadi 80 ndipo dalili za ugonjwa zinaanza kuonekana,”alisema Mdemu.

Alisema Marekani wana dawa kama hiyo ya asili anbayo inaitwa Saw Payments ambayo kwa mwaka wanaiuza zaidi ya dola milioni 25.

Akizungumza na MTANZANIA Kaimu Ofisa Habari wa COSTECH, Deusdetit Leonard, alisema wameisadia NIMR kuonyesha maonesho yao ambapo pia wataandaa maonyesho ya kuwakutanisha waganga wa tiba mbadala ili wapate elimu ya umuhimu wa kuwa na hatimiliki na ubunifu.

Saratani hatari nchini

Februari mwaka jana, Serikali ilisema kila mwaka wagonjwa wapya 50,000 wa saratani za aina mbalimbali hugundulika.

Ilisema kwa mujibu wa takwimu ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), saratani zinazoongoza ni pamoja na saratani ya kizazi (asilimia 32.8), saratani ya matiti  (asilimia 12.9), saratani ya ngozi (asilimia 11), kichwa na shingo (asilimia 7.6) na matezi (asilimia 5.5).

Zingine ni saratani ya damu (asilimia 4.3), saratani ya kibofu cha mkojo (asilimia 3.2), saratani ya ngozi (asilimia 2.8), saratani ya macho (asilimia 2.4) na saratani ya tezi dume asilimia 2.3.

Kwa upande wa wanaume ni saratani ya ngozi (asilimia 24), saratani ya koo (asilimia 16), saratani ya tezi dume (asilimia 10) na saratani ya matezi (asilimia tisa).

Kwa wanawake, saratani zinazoongoza ni saratani ya mlango wa kizazi (asilimia 54), saratani ya ngozi (asilimia 19), saratani ya matiti (asilimia 14) na saratani ya koo (asilimia nane).

Tafiti za Chama cha Saratani cha Marekani (ACS) na cha Afrika Kusini (CANSA) zimebaini kuwa, mwanamume mmoja kati ya sita hupata saratani ya tezi dume katika uhai wake. 

Kutokana na takwimu za mwaka 2010 za dunia nzima, malaria iliua watu 500,000, kifua kikuu watu milioni 2.1, Ukimwi watu milioni 1.8 na saratani watu milioni 9.9.

Kila mwaka wanaume 46,500 wanabainika kuwa na saratani ya tezi dume nchini Uingereza huku 11,000 wakifariki dunia kutokana na maradhi hayo.

Saratani ya tezi dume ni nini?

Saratani hutokea wakati chembe chembe za uhai au seli katika sehemu fulani ya mwili zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili na kutengeneza vijiuvimbe vidogo vidogo.

Kwa kawaida seli huwa zinajigawa, kupevuka na baadaye kufa kwa kufuata taratibu za mfumo wa mwili. Lakini seli za saratani hazifuati mfumo huo.

Badala ya kufa, zenyewe huishi muda mrefu kuliko chembe chembe za kawaida na wakati huo huo huendelea kutengeneza seli nyingine na kuwa uvimbe wa saratani.

Tezi dume hutokea katika mwili wa mamalia wa kiume pekee pale seli katika kiungo hicho zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili hapo ndipo mtu hupata saratani ya tezi dume.

Ugonjwa huu pia hujulikana kama saratani ya kipofu cha mkojo. Kuna visababishi vingi vinavyochangia mwanaume kupata saratani ya tezi dume.

Kwanza kabisa ni umri. Nafasi ya kupata saratani ya tezi dume huongezeka sana hasa ukifikia umri wa karibu miaka 50 na kuendelea.

Nasaba ni kihatarishi kingine ambapo wanaume wenye historia ya tatizo hili kwenye familia zao, yaani wale ambao mmoja wa ndugu zao wamewahi kuugua ugonjwa huu huwa katika hatarini ya kupata kansa hiyo kutokana na kurithi jeni za ugonjwa huo.

Suala jingie ni lishe ambapo wanaume wanaopenda kula nyama na walaji wa chakula chenye kiasi kikubwa cha mafuta hasa ya wanyama huwa katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume wisho

Katika hatua zake za awali, dalili za saratani ya tezi dume hazitofautiani na zile za kuvimba kwa tezi dume . Dalili hizo ni pamoja naKupata shida wakati wa kuanza kukojoa, kutiririka kwa mkojo baada ya kumaliza kukojoa, kukojoa mkojo wenye mtiririko dhaifu.

Wanaume wanashauriwa kufanyiwa uchunguzi kwa kuwa imegundulika kuwa wanaume wengi wakiziona na kuzihisi dalili hizo huona soni kwenda kumwona daktari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles