25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Lori la mafuta laleta maafa Dar

lori la mafutaNA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

WATU wanne wamefariki dunia na wengine 21 kujeruhiwa vibaya, baada ya lori lililokuwa limebeba mafuta ya petroli kuanguka na kuteketea kwa moto katika eneo la Mbagala Rangitatu.

Hali hiyo ilizua taharuki na vilio kwa wakazi wa eneo hilo na maeneo jirani, baada ya idadi kubwa ya watu kujeruhiwa vibaya kutokana na moto huo ulioanza saa 6 usiku.

Watu wengi walijeruhiwa baada ya kwenda kuchota mafuta yaliyokuwa yanamwagika wakiwa na ndoo, vidumu vya lita tano na vyombo vingine bila kuchukua tahadhari.

Chanzo chetu kimepasha kuwa lori hilo aina ya Scania lenye namba T 347 BXG na tela T 464 CSR mali ya Kampuni ya MOIL ya Mwanza, lilikuwa limebeba lita 38,000 za mafuta ya petroli.

Wakizungumza na MTANZANIA jana asubuhi, mashuhuda waliokuwapo eneo la tukio walisema moto huo ulilipuka usiku wa kumkia jana, baada ya lori hilo kuanguka likiwa katika harakati za kukwepa gari jingine.

MTANZANIA lilishuhudia umati mkubwa wa watu ukiwa umelizunguka lori hilo ambalo lilikuwa limeteketea kwa moto pamoja na nyumba mbili zilizopo jirani.

Nyumba moja ambayo ilikuwa na maduka iliteketea yote wakati nyumba ya wageni ya United States iliungua baadhi ya sehemu.

Wakati MTANZANIA likiwa eneo hilo lilishuhudia moto ukiendelea kuwaka katika moja ya maduka yaliyokuwamo kwenye nyumba hiyo.

Wakati hali ikizidi kuwa tete, polisi waliimarisha ulinzi kwa kuzuia watu waliokuwa wamefurika eneo hilo wasisogelee tena lori hilo.

Mmoja wa mashuhuda, Bakari Seleman alisema tukio hilo lilitokea baada ya lori hilo kuanguka wakati dereva alipokuwa akijaribu kulikwepa gari jingine.

“Yule dereva wa lori alikuwa anajaribu kulikwepa gari jingine lililokuwa likitokea Kongowe ambalo liliingia ghafla barabarani,” alisema Seleman.

Alisema baada ya lori hilo kuanguka halikuleta madhara yoyote na kwamba dereva alitoka salama na kuwatahadharisha watu wasilisogelee.

“Dereva alikuwa amesimama kwenye kichuguu akawaaambia watu wasisogee kwa sababu gari limebeba mafuta ya petroli, lakini baada ya muda lilikuja kundi la vijana wakiwa na mifuko ya plastiki na madumu wakaanza kuchukua mafuta,” alisema.

CHANZO CHA MOTO

Shuhuda mwingine, alisema baadhi ya vijana walikuwa wakichota mafuta na kuyahifadhi katika nyumba ya kulala wageni iliyokuwa jirani.

Alisema moto huo ulianza kulipuka baada ya muuza chipsi katika nyumba hiyo ya kulala wageni kupita na dumu la mafuta jirani na jiko.

“Yule muuza chipsi alitoka kwenda kuchukua mafuta na wakati anarudi akapita na dumu palepale jikoni ndipo moto ukalipuka. Alianza kuungua sehemu mbalimbali za mwili wake, akawa anakimbilia kwenye vyumba.

“Kule kwenye vyumba ndiko kulikokuwa kumehifadhiwa madumu mengine, kwahiyo alipofika maeneo yale moto ukaongezeka zaidi kuwaka, akaungua vibaya na kupoteza maisha,” alisema.

Shuhuda mwingine ambaye ni mmoja wa wafanyakazi wa nyumba hiyo ya kulala wageni (aliomba asitajwe jina), alisema baadhi ya pikipiki na baiskeli zilizokuwa nje ya nyumba hiyo ziliteketea kwa moto.

“Hapa nje kulikuwa na pikipiki kama tisa hivi na baiskeli zimeteketea kabisa,” alisema shuhuda huyo.

KAULI YA POLISI

Akizungumza na MTANZANIA, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Nyigesa Wankyo, alisema katika ajali hiyo mtu mmoja alifariki na wengine 19 kujeruhiwa. Ingawa hadi jana jioni watu wanne walikuwa wamefariki.

Alimtaja marehemu kuwa ni Masoud Masoud mkazi wa Charambe na kati ya majeruhi, 18 ni wanaume na mwanamke mmoja.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni gari kuacha njia na kupinduka.

MGANGA MKUU

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Dk. Amani Malima, alisema alipokea maiti moja na majeruhi 21.

“Majeruhi 15 walihamishiwa Hospitali ya Muhimbili baada ya hali zao kuwa mbaya na sasa wamebaki majeruhi sita,” alisema Dk. Malima.

Alisema majeruhi hao wameungua sehemu mbalimbali za miili yao, zikiwamo za siri na usoni.

MUHIMBILI

Ofisa Uhusiano Msaidizi wa Hospitali ya Muhimbili, Dorice Ishenga, alisema kati ya majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo, watatu walifariki dunia na wengine wanaendelea kupatiwa matibabu.

“Wamebaki majeruhi 12 madaktari wanaendelea kupambana ili kuokoa maisha yao,” alisema Ishenga.

Matukio ya aina hii yameripotiwa kutokea mara kadhaa nchini. Mwaka 2007, watu kadhaa walipoteza maisha kwa ajali ya moto walipokuwa wakichota mafuta mkoani Mbeya.

Februari 5, mwaka huu lori la mafuta lililipuka eneo la Mlima Sekenke mkoani Singida ambapo watu wanane walifariki dunia wakichota mafuta.

Nchini Kenya, zaidi ya watu 90 waliokuwa wakichota mafuta kutoka kwenye lori la mafuta lililopinduka katika mji wa Molo walifariki dunia kwa kuungua vibaya mwaka 2000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles