26.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Butiku kuishtaki CCM

Joseph ButikuNA WAANDISHI WETU

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Serikali imesusia maadhimisho ya 15 ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Hali hiyo imejidhihirisha jana baada ya MTANZANIA kutembelea yaliyokuwa makazi ya Mwalimu Nyerere, Msasani Dar es Salaam na kutokuta chochote kilichokuwa kikifanyika kama sehemu ya maadhimisho hayo.

Licha ya kutokuta dalili yoyote ya maadhimisho hayo, nyumbani hapo kulikuwa na watoto waliokuwa wakifanya usafi.

Waandishi wetu walipotaka kuonana na mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, ili kujua kilichokuwa kikiendelea, mmoja wa walinzi wa makazi hayo alisema hakuwapo wakati huo bali alikuwa amekwenda kanisani kusali.

“Mbona hatukuwa na taarifa za ujio wa mgeni yeyote na wala hakukuwa na taarifa za kufanyika kwa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere hapa nyumbani?

“Lakini pia mama ni mgonjwa na ameshindwa hata kwenda Butiama kwa ajili ya maadhimisho ya kifo cha Mwalimu,” alisema mlinzi huyo.

KIJIJINI BUTIAMA

Kijijini Butiama ambako kulitarajiwa kuwa na maadhimisho ya kifo hicho, nako hakukuwa na chochote kilichofanywa na Serikali.

Kutokana na hali hiyo, hakuna kiongozi yeyote wa Serikali kuanzia ngazi ya mkoa hadi taifa aliyefika nyumbani kwa Mwalimu kwa ajili ya kumbukumbu hiyo.

Katika kuonyesha kuwa haridhishwi na jinsi Serikali inavyomuenzi Mwalimu Nyerere, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, alisema anakusudia kwenda mahakamani kukishtaki Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake kwa kile alichosema wameshindwa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo.

Kwa mujibu wa Butiku, CCM na Serikali yake wametupa maadili ya Mwalimu Nyerere yakiwamo yaliyokuwa katika Rasimu ya Katiba.

Butiku aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Nyerere yaliyofanyika kijijini Butiama bila Serikali kushiriki.

“Katika kipindi cha miaka 23 niliyofanya kazi na Mwalimu, alikuwa akichukizwa na suala la kutofuata maadili ya uongozi kama inavyofanywa leo na viongozi wa CCM.

“Sijawahi kuzungumza jambo hili, lakini leo kupitia kumbukumbu ya maadhimisho ya kifo chake ambapo ni mwaka wa 15 tangu atutoke, nitaangalia namna ya kuwafungulia mashtaka CCM na Serikali.

“Kwa hili wala sitanii, mashtaka haya lazima yatafunguliwa kupitia wanasheria wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa kuwa hatukubaliani na namna anavyoenziwa,” alisema.

Butiku ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali  serikalini, alisema Mwalimu Nyerere alikuwa muumini mkubwa wa maadili na alikuwa akisisitiza uwapo wa usawa kwa watu wote tofauti na ilivyo sasa.

LUKUVI AZUNGUMZA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alipoulizwa na MTANZANIA kuhusu Serikali kutoadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere, alijibu kwa kifupi: “Wewe mwandishi, swali lako limepitwa na wakati, hebu kafanye mambo mengine, kwa sasa niko kwenye mkutano mwingine.”

Pamoja na kutoadhimisha kifo cha Mwalimu Nyerere, jana kulikuwa na sherehe za kitaifa za kuzima mwenge wa uhuru zilizofanyika mjini Tabora.

Katika sherehe hizo viongozi wengi wa kitaifa wa chama na Serikali walikuwapo wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi.

Habari hii imeandikwa na Asifiwe George, Shaban Matutu (Dar) na Shomari Binda (Butiama).

- Advertisement -

Related Articles

4 COMMENTS

  1. ndugu mwandishi Asifiwe George ulichoandika juu ya kutoadhimishwa kwa siku ya Nyerere kwa vitendo, umekosea kwa misingi ifuatayo:
    1. hatua ya serikali kutenga tarehe 14/10 kuwa siku ya kitaifa ya kumbukumbu ya kifo cha baba wa Taifa, ni utambuzi na uadhimishaji wa kiongozi huyo kwa vitendo
    2. ndugu huwezi kufunga hema nyumbani kwa Mwl. aidha butiama au msasani kila mwaka kuadhimisha kifo chake kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unaiweka familia yake katika majonzi kwa kila mwaka, je wewe uko tayari kufanyiwa hivyo au je unafanya hivyo kwa baadhi ya ndugu zako waliyokwisha tangulia kwa muumba au mkuki kwa nguruwe mtamu ila kwa binadamu mchungu??
    ni muhimu kwa sisi waandishi wa habari kuzingatia maadili na tuandike taarifa za kupasha habari na kutuunganisha na tuache kuandika vitu vya uchochezi………….
    3. pamoja na taifa kuadhimisha shughuli hiyo, familia ya baba wa taifa nayo inayohaki ya kuikumbuka siku hiyo kwa namna wanavyoona inafaa mathlan kwa kwenda kanisani kusali au kutembelea au kusaidia yatima na wasiyo jiweza. je unauhakika gani kama Mama Maria alikwenda kanisani kusali ikiwa ni namna yake ya kumkumbuka aliyekuwa mwenzi wake???

  2. Maadhimisho ya siku ya Nyerere yamefanyika Tabora sambamba na uzimaji wa mwenge.Hulielewi hilo.Mama Maria Nyerere umeambiwa na ukaandika ni mgonjwa hivyo asingeweza kwenda Tabora.Huwezi kutenganisha mwenge wa uhuru na Hayati Mwalimu Nyerere.Andika mambo ya manufaa kwa jamii sio taarifa zisizo kuwa na mbele wa nyuma.

  3. Mwenge wa Uhuru na Mwl.Nyerere ni vitu viwili tofauti.Siku ya maazimisho ya kifo cha hayati Mwl.Nyerere ingekuwa vizuri itenganishwe na shughuli za uzimaji wa mwenge. kuziunganisha kwa pamoja hazileti utofauti kwa kiongozi aliyekuwa ametukuka kama Mwl.Nyerere

  4. ndugu mwakalinga, umekosea sana. serikali haikukosea kuunganisha vitu hivyo viwili yaani uzimaji wa mwenge na kifo cha baba yetu wa taifa kwani yeye ndiye muasisi wa shughuli za mwenge pindi ulipopandishwa katika kilele cha mlima Kilimanjaro hivyo siyo vibaya kuunganishwa kwake mara moja moja…

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles