25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

CCM, Ukawa wapiga jaramba

ukawa hawaNa Pendo Mangala, Dodoma

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, juzi alitumia muda  mwingi kutoa elimu kwa wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho wanaokutana   Dodoma, juu ya umuhimu wa Katiba inayopendekezwa.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kamati hiyo kiliiambia MTANZANIA  kwamba katika kikao hicho, Rais Kikwete aliwaeleza wajumbe kwa kina jinsi Sheria ya Madiliko ya Katiba inavyoshindwa kueleza kwa kina kuhusu upigaji kura ya maoni. Alisema hatua ya kukosekana tafsiri nzuri na sahihi ya sheria hiyo  imeifanya Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuandaa muswada wa sheria utakaowasilishwa katika kikao cha Bunge la Jamhuri linalotarajia kuwa na kikao chake Novemba mwaka huu.

Katika sheria hiyo, Ibara ya 38, inasema ‘baada ya rais kutangaza kura ya maoni kupitia Gazeti la Serikali, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ndani ya siku 14  kutatangazwa kura ya maoni’. Sheria hiyo inasema:   “Baada ya tangazo hilo, NEC na ZEC kwa pamoja watatangaza siku ambayo kura ya maoni itafanyika, muda wa upigaji kura ya maoni na muda wa kuelimisha na kuhamasisha wananchi kupiga kura ya maoni juu ya Katiba inayopendekezwa”.

Katika sheria hiyo kifungu kidogo cha tatu  kinasema ‘ndani ya siku 21 baada ya NEC na ZEC kutoa tangazo lao msimamizi wa uchaguzi wa kila jimbo la uchaguzi  atawataaarifu wananchi wa eneo analohusika nalo kuhusu utaratibu wa uendeshaji wa kura za maoni’. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema  kikao cha Kamati Kuu pamoja na mambo mengine, kilijadili kwa kina mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba   na hali ya siasa nchini.

Alisema  kamati hiyo ilijadili jinsi ya kushinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa na namna ya kukitoa chama kilipo kwa sasa na kukisogeza mbele. “Chama kinajikita katika kujadili hoja, mchakato wa Katiba, jinsi ulivyoisha na Katiba iliyopendekezwa ambayo ni nzuri. Kwa hiyo  hatuoni mantiki ya vikao vyetu kuwajadili watu, ” alisema.   Nape pia alitangaza uteuzi wa makatibu wa CCM wa wilaya 27 ambao wameteuliwa na Kamati Kuu ya CCM  kujaza nafasi zilizokuwa wazi.

Chadema na Kanda ya Ziwa Wakati hayo yakiendelea, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho kinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), leo kinatarajia kuanza ziara katika mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa  kuwahamasisha wananchi wasiikubali Katiba inayopendekezwa. Taarifa hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, alipozungumza na waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, ziara hiyo itaongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (BAWACHA) ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee. Alisema ziara hiyo inafanyika kama sehemu ya maagizo ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana Dar es Salaam  juzi.

“Ziara hiyo ya siku 20 itaanzia jijini Mwanza na itakwenda mpaka Ukerewe, itafika Sengerema na baadaye itawasha moto Shinyanga na Kagera. “Ziara itawahusisha viongozi wakuu wa Chadema na itaratibiwa na BAWACHA na ina lengo la kuwaeleza wananchi upungufu wa Katiba inayopendekezwa  waipigie kura ya hapana wakati wa kura ya maoni,” alisema Dk. Slaa.

Kuhusu Bunge Maalum la Katiba lililomalizika hivi karibuni, Dk. Slaa alisema Kamati Kuu ya Chadema haikuridhishwa na Bunge hilo kwa vile lilitawaliwa na ukiukwaji wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. “Bunge Maalum lilijigeuza Tume na lilianza kukusanya upya maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya wakati kazi ilikwishafanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Utaratibu wa kupiga kura juu ya Katiba inayopendekezwa kwa njia ya kifungu kwa kifungu uliondolewa na badala yake kura zilipigwa kwa ujumla wa sura za rasimu, yaani kura zilipigwa kwa sura 10 za mwanzo na baadaye kwa sura tisa za mwisho. ‘Kura za maruhani,’ yaani wajumbe wa Ukawa kutoka Zanzibar na za Wazanzibari wengine waliojitoa na ambao hawajulikani majina yao hadi sasa zilihesabiwa kuwa kura halali za ndiyo, hii ilikuwa balaa,” alisema.

Dk. Slaa alitoa mfano wa Mjumbe wa UKAWA, Maulida Komu, ambaye alitajwa kwenye gazeti la Serikali lililotangaza majina ya wajumbe wa Bunge Maalum kuwa anatoka Zanzibar lakini aligeuzwa na kuhesabika kuwa anatoka Tanzania Bara wakati Zakia Meghji wa CCM aliyetangazwa kwenye Gazeti la Serikali kuwa anatoka Tanzania Bara alihesabika kuwa anatoka Zanzibar na hivyo kupiga kura ya ndiyo kama Mzanzibari.

CUF Kanda ya Kusini Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, anaendelea na ziara yake katika mikoa ya kusini ambako aliendelea kuwasisitizia umuhimu wa kuikataa Katiba inayopendekezwa. “Tume ya Warioba licha ya kukusanya maoni ya wananchi pia ilipendekeza muundo wa serikali tatu uliokataliwa na Bunge Maalum la Katiba. “Kwa kuwa mchakato mzima ulijaa utata, nawaomba wakati wa kura ya maoni utakapofika msiipigie kura ya ndiyo kwa sababu Katiba hiyo imejaa maoni ya CCM,” alisema Profesa Lipumba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles