25.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 29, 2022

Contact us: [email protected]

Lishe ilivyomulikwa na ilani za vyama

Na FARAJA MASINDE

KWA mujibu wa wataalamu wa afya, kuna uhusiano mkubwa kati ya lishe bora na afya.

Kama hiyo haitoshi, maambukizo ya magonjwa huongeza mahitaji ya nishati lishe, hivyo iwapo mtu ataongeza ulaji wa vyakula vyenye virutubisho vingi, atakuwa na afya na lishe bora pia mwili wake utakuwa na nguvu siku zote.

Ripoti hiyo inabanisha kuwa mtu mwenye lishe bora anakuwa na uwezo wa kupambana na maambukizo mbalimbali, kwani mfumo wa kinga una nguvu ya kupambana na maambukizo ya magonjwa kutokana na uwapo wa virutubisho vya akiba na hivyo mwili unaweza ukapambana na magonjwa vizuri ukilinganisha na mtu mwenye lishe duni.

Lakini pamoja na maelekezo hayo ya kitaalamu bado suala la uhakika wa lishe bora imekuwa ni changamoto kwa baadhi ya watu nchini Tanzania.

Jambo la kushtua zaidi ni kwamba kwa kiasi kikubwa wanaokumbwa na changamoto hiyo ni wale walioko kwenye mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula (Big 5s).

TAKWIMU

Ripoti ya Utafiti wa Hali ya Lishe nchini ya mwaka 2018, iliyozinduliwa Juni 2019 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar kwa kuratibiwa na Kituo cha Chakula na Lishe (TFNC), inaonyeshakupungua kwa wastani wa kitaifa wa udumavu kutoka asilimia 34.7 mwaka 2014 hadi 31.8 mwaka 2018 kiwango ambacho hata hivyo bado ni kikubwa kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kulingana na ripoti mpya ya UNICEF na WHO kiwango cha udumavu kinaonekana kuwa kikubwa kwenye mikoa 15 kati ya 26 ya Tanzania Bara.

Baadhi ya mikoa hiyo na viwango vyake kwenye mabano ni pamoja na Ruvuma (41.0%), Iringa (47.1%), Rukwa (47.9%), Kigoma (42.3%), Njombe (53.6%) naSongwe (43.3%).

Kulingana na ripoti hiyo, inakadiriwa kuwa mwaka 2018 watoto milioni tatu walio chini ya umri wa miaka mitano walikuwa na udumavu nchini.

Pia katika kiwango cha kitaifa, asilimia 3.5 ya watoto wenye umri wa miezi 0-59 waligundulika kuwa na utapiamlo na asilimia 0.4 walipatwa na utapiamlo mkali dhidi ya asilimia 3.8 na 0.9 ya mwaka 2014.

Kwa Tanzania Bara, matokeo ya utafiti yalionyesha kiwango cha utapiamlo kinachozingatiwa kiko chini katika mikoa  saba kati ya 26 ya Kilimanjaro, Mtwara, Lindi, Rukwa, Mara, Njombe na Songwe.

Kulingana na ripoti hiyo ya mwaka 2018, kuna takribani watoto 440,000 wenye utapiamlo na watoto 90,000 wenye utapiamlo mkali nchini Tanzania.

Hivyo, ni dhahiri kuwa watoto ndiyo wamekuwa wahanga wakubwa wa ukosefu wa lishe bora.

Kwani iko bayana kwamba lishe duni ni chanzo kikubwa cha magonjwa na vifo vya watoto hapa Tanzania, Lishe duni hudumaza ukuaji wa watoto kimwili na kiakili na hivyo kupunguza uwezo wa kufanya vizuri shuleni, pia hupunguza ufanisi katika maisha ya utu uzima.

Lishe bora na huduma zingine za msingi kama elimu na afya ni haki ya kila mtoto kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, lakini mara nyingi mamilioniya watoto kwenye nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania wamejikuta wakikosa haki hii hususan lishe bora kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa mujibu wa UNICEF ambayo mwaka huu inasherehekea miaka 55 tangu kuwapo kwake nchini, inasema hali hiyo  inaweka afya za watoto hatarini, pia njia panda mustakabali wao.

Zipo lawama ambazo zinaelekezwa kwa wazazi moja kwa moja kuwa wamekuwa wakijipendelea zaidi kuliko watoto wao kwa kula vyakula ambavyo ni vizuri kuliko vile wanavyowapatia watoto wao kando kwenye suala la lishe na hata kushindwa kuhudhuria masomo kwa sababu hiyo huku wengine wakishindwa kumudu lishe bora kulingana na hali ya kipato.

Nchini Tanzania, mwaka 2020 ni mwaka wa Uchaguzi na tayari Watanzania wameshapiga kura ya kuwachagua rais, wabunge na madiwani katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28 na tayari mshindi ameshapatikana.

JE, ILANI ZINASEMAJE KUHUSU LISHE?

Pamoja na kukamilika kwa hatua hiyo muhimu, shauku yangu imekuwa ni kujua ni kwa namna gani ilani za vyama hivi zilisema nini kuhusu lishe na ni kwa namna gani zitatekeleza mpango huo katika kuhakikisha kuwa Watoto wa Tanzania wanakua kwenye mstari mnyoofu.

CUF

Ilani ya Chama Cha Wananchi (CUF) yenye kurasa 167 katika sehemu yake ya kwanza (1.3) inayoeleza juu ya Kutokomeza njaa na kuhakikisha lishe bora kwa wajawazito na watoto, imeanisha kama ingeingia madarakani, namna ambavyo  ingepambana na lishe katika kipindi cha 2020-2025.

Katika ukurasa wake wa 9 wa ilani hiyo, imeeleza juu ya ‘Kutokomeza Njaa kwa Wote na Kuhakikisha Lishe Bora kwa Wajawazito na Watoto.’

Kama kingeingia madarakani, kinasema “Kingehakikisha kuwa kila mwananchi anakuwa na uwezo au kuwezeshwa kupata milo mitatu kwa siku. Hatua za makusudi zitachukuliwa kuhakikisha kuwa wajawazito na watoto wachanga wanapata lishe bora itakayowasaidia watoto kujengeka vizuri katika viungo vya mwili, kinga ya mwili na ubongo, ili waweze kushiriki kikamilifu katika kujielimisha na kujiendeleza,” inabainisha ilani hiyo.

CUF haijaishia hapo kwani imeendelea katika Ukurasa wa 124 wa ilani hiyo na kueleza lishe kwa wanafunzi.

“Utafiti unaonyesha kuwa watoto wenye njaa hawafundishiki, huu ndio msimamo na mtazamo wa CUF siku zote. Serikali ya umoja wa kitaifa chini ya CUF kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya na kamati za shule itahakikisha kwamba watoto wa shule za msingi wanapata walau mlo mmoja kamili wa chakula kikuu kinachopatikana katika eneo husika, wakati wanapokuwa shuleni. Watoto wanaokosa lishe bora hawajengi kinga ya mwili na ubongo wao haukuwi vizuri,” inaeleza ilani hiyo ya CUF japo haijapambanua mbinu itakazotumia kufanikisha mpango huo.

CHADEMA

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho nacho kilikuwa kinasaka ridhaa ya kuingia madarakani, katika ilani yake yenye  kurasa 98, kimebainisha katika sehemu ya Nane inayoeleza juu ya kujenga kilimo, uvuvi na ufugaji.

Chadema katika ukurasa huo wa 58, wa ilani yake imeeleza namna ambavyo kingekabiliana na lishe duni nchini;

“Lengo kuu la kukuza sekta ya kilimo ni kuwa na chakula cha kutosha na kukabiliana na lishe duni pamoja na kuhakikisha kuwa kilimo kinaleta tija kibiashara na hivyo kuchangia katika kuongeza pato la taifa.

“Serikali ya Chadema ilitarajia kuimarisha teknolojia ya kilimo ili kukuza,  uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao, Serikali ya Chadema kwa kushirikiana na sekta binafsi itahakikisha kwamba inaweka mkakati wa muda mfupi kwa ajili ya uzalishaji, uhifadhi, usambazaji na soko la kutabirika la mazao ya wakulima nchini.

Aidha, katika ukurasa wa 37 wa ilani hiyo, unaozungumzia mpango wa maendeleo wa miaka mitano katika elimu umefifisha sekta ya elimu.

CCM

Chama Cha Mapinduzi ambacho kimeingia madarakani kwa awamu ya pili ya Serikali ya Awamu ya Tano, kimekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 50, katika ilani yake yenye kurasa 303, imefafanua namna kitakavyoendelea kupambana na changamoto ya lishe nchini.

Eneo la lishe ni moja ya yale yaliyowekwa katika mambo muhimu yatakayozingatiwa katika kutekeleza vipaumbele vikuu vya ilani hiyo ambayo yameainishwa katika ukurasa wa tano.

Katika kipengele (C) inasema kuwa; italeta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi:

“Kuhakikisha uzalishaji unaongezeka katika mazao ya chakula, mifugo na uvuvi kwa ajili ya kujitosheleza kwa chakula na lishe bora,” inasema sehemu ya ilani hiyo.

Aidha, ilani hiyo ya CCM katika ukurasa wa 35 kifungu namba 37 cha ilani hiyo kinasema;

“Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kusimamia mapinduzi ya kilimo ili kuhakikisha kinaendelea kuwa chenye tija na kinachotumia teknolojia ya kisasa. Aidha, chama kitahakikisha kuwa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) inaendelea kutekelezwa na kutoa mchango mkubwa katika usalama wa chakula, pato la taifa, maendeleo ya sekta ya viwanda na huduma kwa kutekeleza maeneo makuu manne (A mpaka D) yafuatayo;

“(e) Kuhamashisha kilimo cha mazao lishe (nutritional-sensitive) ili kupunguza udumavu kutoka asilimia 32 hadi asilimia 24 na kupunguza ukondefu ili kuendelea kuwa chini ya asilimia 5 kiwango ambacho kimewekwa na Shirika la Afya Duniani,” inaeleza ilani hiyo.

Aidha, katika ukurasa wa 139 wa ilani hiyo unaozungumzia hasa eneo la lishe, unasema kuwa;

“Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, CCM kitaendelea kuhakikisha kuwa lishe bora inaendelea kuwa kipaumbele ili wananchi waweze kuwa na afya bora na maisha mazuri na pia waweze kuchangia kuwepo kwa nguvu kazi imara na yenye tija kwa Taifa ambayo inaweza kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi. Ili kufikia malengo hayo, Chama kitaelekeza Serikali kutekeleza yafuatayo:

“Kutekeleza mikakati ya kupunguza idadi ya watoto chini ya miaka mitano wenye udumavu na kukonda kwa kasi kubwa. Kufanya tathmini ya kila mwaka kuhusu hali ya lishe na tathmini maalum kila baada ya miaka mitano na hatimaye kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha kwamba Taifa linakuwa na wananchi wenye afya bora na uwezo wa kuchangia ipasavyo katika shughuli za maendeleo ya Taifa lao.

“Kuhakikisha hakuna ongezeko la uzito uliozidi kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano na kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na uzito pungufu yaani chini ya uzito wa kilogramu 2.5 ili iwe chini ya asilimia 50,” inasema ilani hiyo na kuongeza katika kipengele (E) kuwa;

“Kuongeza uzalishaji na usambazaji wa mbegu na mazao ya kilimo yenye viini lishe vingi, mbogamboga, matunda, mazao ya mifugo na uvuvi pamoja na uhamasishaji na uelimishaji wa ulaji wa vyakula hivyo, Kuimarisha uhusiano wa wadau wa lishe na sekta binafsi katika kuzalisha bidhaa za vyakula viliyoongezewa virutubishi, Kupanua wigo wa uelimishaji na uhamasishaji wa masuala ya lishe kupitia majukwaa mbalimbali ili kuelimisha juu ya mitindo bora ya maisha na kuzuia ongezeko la uzito uliozidi na kiriba tumbo na kuongeza na kuwajengea uwezo wataalam wa afya kwa ajili ya kutoa huduma za lishe katika ngazi za mikoa, halmashauri pamoja na vituo vya kutolea huduma za afya,” inaeleza ilani hiyo ya CCM.

Hata hivyo, kikiwa chama kilichokuwa madarakani kwa muda mrefu, CCM inasema katika kipindi kilichopita kimefanikiwa; Kuimarisha huduma za lishe za wajawazito na wanawake wanaonyonyesha, vijana balehe, watoto wachanga kwa kuhakikisha elimu sahihi ya lishe inawafikia.

“Kuongeza uwekezaji katika masuala ya lishe kwa halmashauri nchini kutenga Sh 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano kutoka kwenye vyanzo vyake vya mapato ya ndani ili zitumike kutekeleza afua za lishe.

“Kuimarisha usimamizi wa masuala ya lishe kwa kuanzisha Kamati Elekezi za Kitaifa ambazo zimesaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa afua za lishe; Kuimarishwa kwa uratibu wa masuala ya lishe katika ngazi ya Kitaifa, Mkoa na Halmashauri kwa kuanzisha kitengo cha lishe katika Ofisi ya Rais –TAMISEMI.

“Kuimarisha huduma za matibabu ya utapiamlo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na jamii ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo watoaji wa huduma hizo na kuhakikisha upatikanaji wa mahitaji mfano chakula dawa na vifaa vya kutathmini ya hali ya lishe.

Hizo ni ilani za baadhi ya vyama ambavyo vyote viliomba ridhaa ya kuchaguliwa kuongoza Tanzania katika kipindi cha miaka mitano ijayo na ahadi juu ya yale yatakayofanyika katika kuhakikisha kuwa inasimamia suala la lishe na kupunguza suala la udumavu na utapiamlo.

Tayari uchaguzi Mkuu umeshafanyika hivyo ni suala la kusubiri ni kwa namna gani chama kilichofanikiwa kutwaa dola kitakavyotekeleza ahadi hiyo katika kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na kizazi chenye lishe bora kwa manufaa ya hapo baadaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,444FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles